Saturday, November 9, 2013

WALEMAVU KATAVI WAPOKEA MSAADA WA MIL 52
























 Katavi
KAMPUNI ya uwindaji ya Tanzania Big Game Safaries Ltd  imekabidhi baiskeli ya walemavu kwa walemavu 150 walioko katika mkoa wa Katavi zenye thamani ya shilingi million 52.5 ikiwa ni mchango wao katika jamii kutokana na faida wanayopata katika shughuli za uwindaji na utalii mkoani Katavi

Akikabidhi vifaa  hivyo  kwa  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda, mwakilishi wa kampuni hiyo, Rose Bekker alisema Kampuni ya Big Game imekuwa ikitoa msaada kwa wana jamii mbali katika maeneo wanayofanyia kazi za uwindaji kila mwaka tangu 2005 ambapo mpaka sasa kampuni hiyo imeshakabidhi baiskeli za walemavu za kisasa zipatazo elfu tatu katika maeneo mbali mbali hapa nchini

Alisema kampuni yake pia imekuwa ikiwekeza katika ujenzi wa madarasa, ujenzi wa makanisa, vifaa vya shule na misaada kwa walemavu kwa kushirikiana na asasi isiyo ya kiserikali ya Conservation Foundation Trust Fund (CFT) ya jijini Arusha

Alisema taasisinyake inawasiliana na asasi ya Kimarekani ya Wheel Chair Foundation katika matengenezo ya baiskeli kwa ajili ya walemavu kwa gharama ya shilingi laki tatu na nusu (350,000/=) 

Katika hotuba yake mgeni rasmi wa hafla hiyo fupi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mpanda, Enock Gwambasa alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na tabia mbaya ya unyanyapaa kwa walemavu katika jamii hali inayosababisha baadhi ya walemavu kuishi kwa sononi kubwa

Aliwataka walemavu kujiona kuwa nao ni sehemu ya jamii na hivyo wana uwezo wa kuzalisha mali ndani ya jamii ikiwa watajengewa uwezo wa kufanya kazi hizo, wasibweteke washiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii kama vile kupiga vita ujangiri kwa kutoa taarifa serikalini za uwepo wa majangiri katika maeneo yao

Jumla ya walemavu 150 walikabidhiwa baiskeli zenye thamani ya shilingi laki tatu na  nusu sawa gharama yote kufikia shilingi milioni 52.5 zote zikiwa zimetolewa na Tanzania Big Game Safaries kama mrejesho wa faida kwa jamii inayozunguka maeneo wanayofanyia kazi zake.

Mmoja wa waliopata msaada huo ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka huu katika shule ya Sekondari ya Mwangaza, Kashindie Kisamvu licha ya kushukuru kwa msaada huo aliiomba serikali kuangali suala la miundombinu katika maeneo ya maofisini na madarasani kwani hakuna sehemu ya mlemavu kuingia 

Alisema vyoo vya shule havimfai kabisa mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo alipokuwa akisoma shuleni Mwangaza alipobanwa na haja alikuwa akilazimika kuomba ruhusa kwenda nyumbani kwao kwa lengo la kujisaidia na kurudi tena shuleni hali iliyokuwa ikimsababishia kupoteza muda mwingi na vipindi vya masomo 

“Nilikuwa Napata shida sana shuleni kwani madarasani hakuna sehemu ya kuingia kwa baiskeli, ofisini hakuna na vyooni nako hakuna pia sehemu ya kupita mlemavu, nilikuwa nikibanwa na haja nalazimika kuomba ruhusa kwenda nyumbani kujisaidia ndipo nirudi tena shuleni, nikuwa nachelewa vipindi vingi sana na nilikuwa naathirika sana kitaaluma” alisema Kashindie