Tuesday, December 8, 2009

DC MPANDA ALIA NA WALA RUSHWA YA MIFUGO

Na Willy Sumia, Mpanda


SERIKALI za vijiji na kata katika wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa zimeagizwa kuhakikisha zinasimamia kanuni na sheria za ardhi katika maeneo yao ili kuzuia uwezekano wa kuibuka kwa migogoro ya wakulima na wafugaji wilayani humo.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Mpanda Kanali John Antonyo Mzurikwao alipokuwa akizungumza katika vikao vya pamoja na serikali za mitaa za vijiji na kata katika tarafa za Mpimbwe na Inyonga wakati za ziara ya kukagua maendeleo ya miradi na makabidhiano baina ya serikali za vijiji zilizopita na zilizoingia madarakani.

Kanali Mzurikwao amesema chanzo kikubwa cha migogoro baina ya wafugaji na wakulima ni viongozi wa vijiji husika ambao wamekuwa wakipokea rushwa ya mifugo ya ng’ombe au mbuzi hushindwa kumuelekeza vizuri mfugaji wapi kwa kuchungia kisheria na kumuacha akae eneo ambalo haruhusiwi na matokeo yake ni migogoro.

Kutokana na kuingia madarakani kwa serikali mpya za vijiji na vitongoji mkuu huyo wa wilaya amewataka viongozi walioingia madarakani kusimamia kwa karibu idadi ya mifugo na eneo la malisho lililopo katika maeneo yao.

Wakati huo huo mkuu wa wilaya ya Mpanda kanali John Antonyo Mzurikwao ameziagiza Halmashauri wilayani humo kutoa mafunzo elekezi ya uongozi kwa viongozi wote wa serikali za vijiji na mitaa walioingia madarakani kutokana na kukamilika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa ili viongozi hao waweze kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu bila kuvuka mipaka yao ya utendaji.

Kanali Mzurikwao amesema mafunzo hayo yanatakiwa kutolewa kabla ya Januari 2010 na kila atakayehudhuria mafunzo hayo atatakiwa kuandika kwa mkono wake taarifa ya mafunzo atakayojifunza ili kujiridhisha kama kweli wameelewa mafunzo hayo.

MWISHO