Tuesday, October 22, 2013

UNYANYAPAA UNACHANGIA MAENDELEO DUNI- ASASI

BARAZA  la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini
(NACOPHA) limeelezea jinsi vitendo vya unyanyapaa wanavyofanyiwa watu
wanaoishi na VVU na baadhi ya watu katika jamii vinavyoathiri ufanisi
wao wa utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo katika jamii.

Akifungua mkutano wa uchaguzi wa kuunda Baraza la viongozi wa watu
wanaoishi na virusi vya ukimwi  liitwalo KONGA uliofanyika juzi mjini
Namanyere katika halmshauri ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa Makamu
mwenyekiti wa NACOPHA, Deo Chrispin Mlori mwishoni mwa wiki alisema
waathirika wa ukimwi nao pia wana haki na fursa sawa  ya  kuchangia
nguvu zao kwa ajili ya maendeleo ya jamii

Alisema kuanzishwa kwa Baraza hilo la kitaifa lililoundwa kisheria
kwenye mkutano wa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini
uliofanyika mwishoni mwa mwzi Agost jijini Dae es salaam na baadae
kuagizwa kuundwa kwa mabaraza ya wilaya zote nchini ambayo yataitwa
KONGA  kwa lengo la  kukabiliana na unyanyapaa na ubaguzi unaotokana
na hali ya kuishi na VVU

Makori aliwaambia wajumbe hao kuwa KONGA zitakazoundwa katika kila
halamshauri zitashirikiana na viongozi wa halmashauri husika katika
kuweka msukumo katika kuratibu na kusimamia uwezeshaji tiba mafunzo na
misada kwa watu wanaoishi VVU na kupinga dhuluma zinazokiuka utu wa
mtu  kwa kuunganisha mitandao mbalimbali inayotekeleza program za
ukimwi

Alisema baraza la kitaifa limeunda timu maalumu itakayoratibu uundwaji
wa KONGA katika halmashauri zote za mikoa ya Rukwa na Katavi tayari
zimeshaunda uongozi wao isipokuwa halmashauri tatu bado hazijafanya
uchaguzi ambazo alizitaja kuwa ni Kalambo mkoani Rukwa na Halmashauri
za Mlele na Nsimbo katika mkoa wa Katavi.

Wajumbe wa uchaguzi huo walielezwa na mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Nkasi Peter Mizinga  ambaye ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu
wa uchaguzi huo kuwa halmashauri ya wilaya ina wajibu wa kushirikiana
na viongozi wa KONGA hizi katika kuhakikisha kuwa watu wanaoishi na
VVU na wengineo wasiokuwa na virusi kuzuia kuenea kwa maambukizo mapya
ya VVU.

Alisema halamshauri ya wilaya ya Nkasi itaanda utaratibu
utakaowashirikisha viongozi wa baraz a la wilaya katika kutoa mafunzo
kwa njia ya mikutano semina na makongamano yatakayokuwa yanaendeshwa
katika maeneo mbalimbali kuanzia ngazi za vijiji kata hadi Tarafa na
hata kwenye vikao vya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo

Mratibu wa ukimwi katika halmashauri hiyo Filbert Msapila
aliwahahakikishia wajumbe wa kikao hicho na viongozi wake kuwa
ushirikiano wao na halmashauri utawezesha kujenga uwezo wa Taasisi za
watu wanaoishi na VVU ili waweze kumsaidia  mtu mmoja mmoja na au
familia zao kupitia program zao ikiwa ni pamoja na kutokomeza suala la
unyanyapaa.

Katika uchaguzi huo  Edinatha Matandiko alichaguliwa kwa kura zote 21
za wajumbe kuongoza baraza la viongozi 10 wa KONGA ya wilaya ya Nkasi
aliposimama kuwashukuru wajumbe alisisitiza umuhimu wa mitandao yote
inayojihusisha na ukimwi chini ya BARAZA la kitaifa na KONGA za wilaya
kusimamia kulinda na kuteteta haki za watu wanaoishi na virusi vya
ukimwi katika jamii na kuwa na mikakati endelevu ya kukabiliana na
maambukizo mapya
Mwisho.

Tafsiri
NACOPHA-National Council of People Living with HIV/AIDS
KONGA-ni chombo cha juu ndani ya halmashauri ya wilaya manispaa au
majiji kinachojihusisha na usimamizi na uratibu wa masuala na shughuli
za watu wanaoishi na VVU

WATATU WAFARIKI KWA MAUAJI MMOJA AJINYONGA KWA KANGA


WATU watatu wamefariki dunia katika mazingira tofauti katika mkoa wa Katavi akiwemo mwanamke aliyejinyonga kwa kanga yake mwenyewe kutokana na msongo wa mawazo unaotokana na ugonjwa wa akili

Ndugu Dereva Kuliwaliwa (47) mkulima wa amepotza mke wake, Lemi Bundala (42) aliyejinyonga kwa kanga yake mwenyewe Oktoba 19, 2013 katika kijiji cha Kapalala wilaya ya Mlele mkoani Katavi kutokana na kinachodaiwa kuwa ni msongo wa mawazo unaosababishwa na maradhi ya akili aliyokuwa akiugua kwa muda mrefu marehemu

Habari kutoka kijijini hapo inadai kuwa marehemu kabla ya kujinyonga alikuwa akitibiwa maradhi ya akili katika hospitali ya wilaya ya Mpanda wakati huo huo akitibiwa kwa tiba za jadi kijijini hapo

Inadaiwa kuwa mpaka mauti yanamfika marehemu alikuwa akiishi kwa mama yake mzazi aliyetajwa kwa jina la Marry Lubigisa (65) ambapo siku hiyo mume wa marehemu alifika nyumbani kwa mama mkwe ili kumjulia hali mkewe ndipo mama mzazi wa marehemu aliingia katika chumba alichokuwa akilala marehemu kwa lengo la kumuita aweze kutoka nje kusalimiana na mumewe lakini muda huo marehemu hakuwemo chumbani kwake

Kufuatia kukosekana kwa marehemu chumbani kwake ndugu na majirani walianza kumtafuta aliko ndipo baadae walimkuta akiwa amejinyonga kwa kutumia kanga yake aliyokuwa akiivaa umbali wa mita sabini hivi kutoka nyumbani kwake

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoani Katavi, Emanuely Nley alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa uchunguzi wa awali wa jeshi la polisi umebaini kuwa chanzo cha tukio kinatokana na maradhi ya akili yaliyokuwa yakimsumbua marehemu tangu akiwa na ujauzito wa mtoto wake wa mwisho na umauti umemkuta akiendelea na matibabu katika hospitali ya wilaya ya Mpanda na matibabu ya kijadi.

Katika tukio linguine Mwinamila Dohole (50) mkazi wa kijiji cha Mnyamasi wilaya ya Mlele aliuwawa kwa kukatwa katwa na mapanga sehemu za kichwani na kisogoni baada ya kukutwa akiongea na mke wa ndugu Julius Lutema (38) mkazi wa kijiji hicho

Kwa mujibu wa Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Katavi Emanuely Nnley marehemu alifikwa na mauti hayo alipokuwa amesimama na mke wa Julius Lutema barabarani baada ya mke wa Julius kutoka kushitaji ugomvi wa kindoa katika Serikali ya kijiji uliokuwa ukiendelea baina yao

Nnley alisema siku ya tukio mke wa marehemu anayeitwa Diu Uswelu (35) alikuwa na ugomvi na mumewe akaamua kwenda kushitaki katika serikali ya kijiji alipokuwa akirudi alisimama na ndugu Julius Lutema ndipo walianza kushambuliana kwa mapanga na kupelekea kifo cha marehemu na kumjeruhi mke wa marehemu ambaye alikimbizwa hospitali ya wilaya kunusuru uhai  wake.

Alisema jeshi la polisi linamtafuta mtuhumiwa Julius Lutema ambaye alitoweka baada ya tukio ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria

Akifafanua kuhusu tukio lingine Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Katavi, Nnley alisema mnamo Oktoba 17, 2013 katika mtaa wa Nsemulwa – airtel mjini Mpanda, Isack Enock Kalinga (27) mkazi wa Kasimba alikutwa ameuwawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya kichwani, shingoni na kwenye mkono wa kushoto na watu wasiojulikana.

Alisema kabla ya kuuwawa marehemu alikuwa akiishi peke yake katika nyumba yao baada ya mama yake mzazi kumkimbia kutokana na vitisho alivyokuwa akimtishia mama yake kuwa angemuua baada ya kushindwa kumpatia mtaji wa shilingi milioni moja.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa na tabia ya ukorofi na alikuwa ametoka kifungoni kutoka na vitendo vya ukorofi alivyokuwa akivifanya kila na kufungwa jela kwa kipindi cha miezi minne kwa mara mbili tofauti ambapo bado upelelezi unaendelea ili kuwabaini waliofanya mauaji hayo.

Tuesday, October 15, 2013

LEO MPANDA MJI KAMA KULEEEEE


KATIKA MAZINGIRA YA KUMSHUKURU MWENYEZI MUNGU SIKUU YA EID EL HAJI IMESHEREHEKEWA KWA AMANI BILA MATUKIO MAKUBWA YA AJALI HASA ZA BODA BODA KATIKA MJI WA MPANDA TOFAUTI NA HALI ILIVYOKUWA KATIKA SIKUKUU ZILIZOPITA.

leo hali ya mpanda mji ni kama vile YERUSALEMU MPYAAAAAAAAAAAA

TUNAWATAKIA SIKUKUU NJEMA YA EID EL HAJI - Blogger

MAJENGO YA SHULE YANAUZWA KAHAMA MJINI

TITTLE No. 37755 Registered Mwanza
LAND plot No. 122 
BLOCK 'P' low Density
Mbulu Kahama Urban Area
GURANTEE ; 33 yrs
MMILIKI; BERTHA MABULA KINUNGU
SIMU: +255756 01 83 36











KAMA UNAHITAJI WASILIANA NA MMILIKI WA SHULE: Bertha Mabula Kinungu wa S. L. P 34 Kahama; simu No. +255756 01 83 36
Email: willysumia@gmail.com
BEI NI NAFUU SANA

Thursday, October 10, 2013

KATAVI KUWAZADIA WALIMU WATAKAOFAULISHA






Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dr Rajabu Rutengwe akizungumza na wanahabari ofisini kwake, kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emanuely Kalobelo

MKOA wa Katavi unajiandaa kuanza kutoa zawadi kwa walimu watakaowezesha shule zao kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya Taifa ili kuinua kiwango cha taaluma katika shule za Sekondari na Msingi mkoani humo.

Hayo yalibainishwa na Katibu Tawala wa mkoa huo, Mhandisi Emanueli Kalobelo alipokuwa akizindua semina ya wahojaji kutoka wilaya za mkoa huo watakaoendesha utafiti wa kiwango cha uelewa wa stadi za kusoma na kuhesabu katika jamii iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la UWEZO TANZANIA. 

Alisema hali ya taaluma katika shule za Msingi na Sekondari katika mkoa wa Katavi siyo nzuri na hivyo kulazimisha uongozi wa mkoa kuanza mikakati imara ya kuanza kukabiliana na hali hiyo ili kukiokoa kizazi cha leo na kijacho katika mkoa huo.

Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutoa zawadi kwa walimu watakaowezesha shule zao kufanya vema katika mitihani ya Taifa ya sekondari na Msingi pamoja na kuwapa mafunzo ya mara kwa mara walimu waliopo kazini kwa lengo la kuwapa ujuzi wa kutosha walimu hao.

Alisema Mkoa wa Katavi  unajumla ya wanafunzi 5,855 wasiojua kusoma wala kuhesabu wanaosoma darasa la pili katika shule za Msingi licha ya kuwa wamekuwa wakihudhuria masomo darasani

Alifafanua kuwa  lengo la  Mkoa wa Katavi ni kuhakikisha kwamba wanafunzi wanajua  kusoma  na kuandika  wakiwa Darasa la pili kabla ya kuingia darasa la tatu ili waweze kuanza kupokea maarifa mapya kutoka kwa walimu na kwenye vitabu.

Aidha Katibu tawala wa mkoa alisema  mkoa wa Katavi umelenga  kuboresha taaluma ili kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kumaliza elimu ya  msingi  kufikia asilimia sitini mwaka huu  ukilinganisha na asilimia 26 za ufaulu wa mwaka jana katika matokeo ya darasa la saba.

Akizungumzia kiwango cha ufaulu kwa shule za Sekondari mkoani mwake Kalobelo alisema wamepanga kuinua kiwango cha ufaulu  wa mtihani wa kidato cha nne  kufikia  asilimia sitini mwaka 2013 kutoka asilimia arobaini na mbili  za mwaka jana na asilimia sabini  mwaka 2014 ili mwaka 2015 ufaulu uweze kufikia asilimia themanini

Alisema Mkoa umeanzisha utaratibu wa kuzipanga shule kuwa  katika madaraja katika matokeo na kutangaza matokeo ya mitihani ya kila shule  kwenye  vyombo vya habari  na mbao za matangazo sambamba na kutoa tuzo kwa shule bora zinazofanya vizuri kwa mwaka huo katika mitihani ya Taifa

Wednesday, October 9, 2013

MANISPAA YAMKABA KOO MKANDARASI SUMBAWANGA









MANISPAA ya Sumbawanga mkoani Rukwa imemuagiza mkandarasi wa barabara anayefanya matengenezo ya muda katika barabara za mjini humo kurudia kazi hiyo kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yake

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na ofisi ya Mhandisi wa Manispaa ya Sumbawanga na kuthibitishwa na mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini, mkandarasi anayefanya matengenezo ya barabara sita ndani ya Manispaa hiyo kusimamisha kazi hiyo mara moja na badala yake kurudia tena kazi yake kutokana na mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi uliofanyika Septemba 5, 2013

Katika barua hiyo iliyosainiwa na mkaguzi wa Barabara wa Manispaa hiyo, Kashinde Malilo imeelezwa kuwa katika ukaguzi huo ilibainika kuwa kifusi kinachotumika katika barabara hizo hakifai kutokana na kuwa na vumbi jingi tofauti na maelekezo yaliyoko katika mkataba

Barua hiyo iliyoandikwa kwenda kwa kampuni ya NOVIDS LTD ya jijini Mwanza ambayo imepewa zabuni ya kufanya matengenezo hayo imezitaja barabara zinazotakiwa kurudiwa na kampuni hiyo kuwa ni barabara ya Mtaa wa Jangwani, Mtaa wa Majengo, Posta hadi NMC,  Kasulu hadi Kanisa la Neema, Msakila hadi Kasulu na Mtaa wa Katusa.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi za CCM mkoa wa Rukwa, mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini, Mhe. Aeshi hilal alisema kuwa katika kikao walichofanya hivi karibuni katika ofisi za Manispaa walikubaliana kusimamia kwa karibu suala la uchakachuaji wa makandarasi mbali mbali katika manispaa hiyo ili kuzuia makosa yaliyofanywa na uongozi uliopita yasirudiwe tena

Aliyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ujenzi chini ya kiwango wa stendi ya basi Sokomatola, ujenzi wa barabara ya lami mjini sumbawanga, ujenzi wa jingo la shule ya sekondari ya Mazwi na mitaro katika baadhi ya barabara mjini Sumbawanga

Katika hatua ya kushangaza  mmiliki wa kampuni ya NOVIDS LTD ya Mwanza ambayo ndiyo iliyosimamishwa isiendelee na kazi mjini Sumbawanga, Leonard Lukasi alikataa kupokea barua hiyo na kudai kuwa huenda amekabidhiwa mwakilishi wake aliyemtaja kwa jina moja la Willy ambaye hakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo.
mwisho

MSD WAJIPANGE UPYA - WANAKIJIJI




UHABA wa dawa za binadamu katika vituo vya afya na zahanati umeanza kuchukua sura mpya baada ya baadhi ya wananchi kuiomba Serikali kuangalia upya mfumo wa usambazaji dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kunusuru maisha ya wananchi

Wito huo ulitolewa jana na baadhi ya wakazi wa vijiji vya Mamba na Majimoto wilaya ya Mlele mkoani Katavi walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo kufuatilia mpango wa huduma za chanjo kwa watoto na akinamama katika maeneo yaliyoko mpakani mwa nchi ya Tanzania na DRC

Wananchi hao walisema licha ya kuwa vituo vingi vya afya na zahanati vimejengwa na kuanza kutoa huduma kwa karibu na wananchi lakini bado changamoto ya upatikanaji wa dawa za binadamu katika vituo hivyo hairidhishi kutokana na vituo hivyo kukosa huduma hiyo kwa muda mrefu

Walisema awali wakuwa wakiwatuhumu baadhi ya watoa huduma katika vituo hivyo kuwa wanauza dawa hizo lakini baadae waliweza kubaini kuwa hata wao watoa huduma wananunua dawa kutoka maduka ya dawa pindi wanapougua kutokana na MSD kutokufikisha dawa hizo kwa wakati katika zahanati na vituo vya afya

Walisema mtindo wa kupeleka dawa katika vituo vya afya na zahanati kwa kipindi cha miezi mitatu ni tatizo linaloweza kuleta dhahama katika jamii hasa ya vijijini kwani uwezekano wa dawa kukaa kwa kipindi hicho hasa maeneo ya vijijini ni mdogo sana kutokana na mahitaji na miundombinu ya kuhifadhia dawa kuwa bado ni duni.

Walisema mganga wa zahanati hawezi kuzuia dawa zisitumike katika kipindi cha miezi mitatu kama wagonjwa wapo na wanahitaji dawa hizo kwani jukumu lake ni kutibu wananchi wapate kupona na siyo kuhifadhi dawa hadi zifikie miezi mitatu

“Huwezi kubana matumizi ya dawa vijijini kwenye wagonjwa wengina maduka ya dawa hakuna, hapo tunadanganyana maana hata iweje hizo dawa wanazoleta za miezi mitatu hazitoshi hata mwezi mmoja kutokana na mahitaji kuwa makubwa” alisema Martini Pesambili mkazi wa Majimoto

Mganga mkuu msaidizi wa kituo cha afya Matai wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Bonifasi Wambanga alisema kuwa hata wanapoagiza dawa MSD kulingana na mahitaji dawa zinazopelekwa haziendani na mahitaji waliyopeleka na badala yake zinapelekwa dawa zingine zisizohitajika kulingana na jiografia ya eneo husika kutokana na kuchukua muda mrefu tangu kuagizwa dawa na kufika

Alisema kuna dawa zinahitajika majira ya kiangazi kulingana na hali ya hewa na kipindi hicho lakini zinafika masika ambako kuna mahitaji tofauti na dawa zinazofika kipindi hicho kutokana na hali ya hewa ya masika