MTAA
WA FISI MJINI MPANDA KAAAZI KWELI
Na Beda Msimbe
YALIKUWA majira ya saa mbili usikui,
Ijumaa wakati nilipopita katika mtaa wa Majengo maarufu kama Kings Palice kati
kati ya mji wa Mpanda.
Nilikuwa nimechoka lakini pia
nilikuwa na hamu ya kujua usiku Mpanda ikoje na eneo ambalo niliambiwa linaweza
kunipa taswira ya Mpanda usiku ni eneo la Majengo. Mtu aliyenielekeza hakuwa na
muda wa kunipa hadhari, aliniona ni mtu wa makamo na ipo haja ya kukutanishwa
na watu wa aina yangu katika maeneo ambayo ni wenye hulka fulani tu wanakuwa na
uwezo wa kufika na kuvinjari.
Nilinyoosha miguu yangu kutoka
Kenyatta, taratibu kama vile nina muda wote duniani, nikiangalia watu na
miondoko yao hapa na pale na katika safari yangu kutoka mtaa wa Kenyatta
nasikia harufu ya bangi hapa na pale, lakini ahh nilifikiri huenda si bangi ni
majani yanachomwa moto.
Kwa siku ya leo Mpanda imeonekana
usiku wake huwa mtulivu ukiachia muziki wa hapa na pale; maduka mengi ya bidhaa
za kawaida hufungwa mapema zaidi, lakini maduka yenye bidhaa zinazofanana na
maisha ya usiku hubaki wazi mpaka saa nne usiku na mengine kuendelea.
Katika muda huu nanyoosha miguu
wamachinga wa mtaa wa Kenyatta walikuwa bado wanaendelea na shughuli zao japo
wengine walikuwa wakifunga mafurushi lakini maduka ya pombe yalikuwa bado wazi
na ya muziki pia. Katika mji ambao hadithi zake zina maingiliano makubwa na
watu kutoka nje ya Tanzania na yenye uchumi unaonekana kukua kwa sasa, maisha
haya ya usiku yasiyo na fujo yanaonekana kuwa ndio bora zaidi.
Dakika zilizidi kuyoyoma na kasi ya
mwendo ilizidi kupungua kwa jinsi ninavyokaribia mtaa wa Majengo ambao wakazi
wa hapa wameupatia jina la Uwanja wa Fisi. Nilitaka kukuficha ukweli, ukweli
kwanini niliamua kufika Mtaa wa Majengo, maarufu kama Uwanja wa Fisi.
Nilipata tetesi kuwa upo ukahaba wa
haja katika eneo hili na washiriki wake ni kutoka mikoa ya Singida, Mbeya,
Tabora na kidogo Kigoma. Nikaambiwa tena kwamba wapo wanafunzi walioacha
sekondari wakaenda katika kituo kile kikubwa kufanya ukahaba kwani unalipa.
Suala kwamba unalipa ni gumu kidogo
lakini ukifika eneo unaweza kujua unalipa kwa kiasi gani. Naam nilifika eneo
lile majira ya saa tatu na nusu kutokana na kutembea kuzembe kwangu, mambo
yalikuwa ndio kwanza yanaanza kuchangamka lakini nilichotaka sikukikiona
kirahisi vile.
Niliamua kuketi mahala kupata supu,
kwa wale tuliozoea kuandika habari laini hizi, unapokosa dira, supu au pombe
husaidia kuvuta muda kuona kuna kitu gani eneo lile. Katika supu, maneno
yalikuwa zaidi kuhusu maadili makubwa, mambo ya machimbo. Watu wanazungumzia
madini wanazungumzia utafutaji wa fedha wanazungumzia masoko na mawakala
wanaowadhulumu.
Lakini katika mazungumzo haya,
unaambulia kujua kwamba vijana wa eneo hili ambao ni mchanganyiko kutoka mikoa
na nchi mbalimbali wana fedha za kukutandikia usoni kwa kukosa nidhamu
wanayoitaka wao.
Wanachozungumza ni kuishi leo kama
vile hakuna kesho, wakati unamaliza supu, wanaokunywa pombe sasa wanaanza
kubadilika na hata wewe unaanza kuona kuna mabadiliko, mabinti ambao ulikuwa
unawaona wana ustaarabu wanaanza kuvaa nguo zinazoashiria kuwapo kwa biashara.
“Hapa pana mambo,” nilisema nikitega
njia ya maneno ili niweze kuambulia kitu. Kijana mwenye umri kati ya miaka 25
na 30 alinitazama kisha akatabasamu.”U mgeni wewe,” aliniuliza na mimi
nikamwambia, ndiyo. Hapo ndipo alipoanza kutiririka kwani alisema ni eneo zuri
hilo kwa biashara mbalimbali, wagumu wanaokaa migodini ndipo huja kuambulia
asusa za maisha baada ya kuumia.
Pana pilikapilika sana hapa na
kuwapo kwa madalali wa vyumba kuliniashiria kwamba kuna uwezekano mabinti hawa
wanaofanya biashara wanamalizia mashauri hayo ya mapatano palepale, kumbe
haikuwa hivyo.
Ukimuita binti pale, anataka muende
naye ulikopanga, lakini si kutafuta pale ambapo pana madalali wa vyumba vya
kupanga na madini, na bei yao waliwazaji hao kwa kukuangalia usoni ni nzuri lakini
kimsingi Sh 5,000 inatosha kwa uliwazaji wa fasta.
Uwanja wa Fisi ni Uwanja wa Fisi
kweli kama tabia za fisi zinavyojulikana kuna kila kitu kinachotakiwa kama
ilivyokuwa katika uwanja wa Fisi wa Dar es Salaam, tatizo ni moja tu hakuna
magodoro ya fasta eneo hilo, hakuna uwazi katika mipira japo baadhi ya gesti
zina mipira. Nilipata nafasi ya kuongea na Agness (si jina lake la kweli)
ambaye ni mwenyeji wa Mbeya.
Aliniambia kwamba amefika hapo
kutafuta fedha kwa kuwa mji umeshaanza kuwa na watu ambao wanahitaji pia
burudani. Alisema kuwepo kwa wageni wengi hasa wanaofanya mambo mbalimbali
kuanzia usakaji wa madini, biashara za madini na vyakula wakiwa vijana
wanafanya watu kama wao kuwa na sehemu ya kujipatia fedha.
Wanalipa vizuri watu hawa ambao alisema
wengi wao ni vijana wa Kisukuma na hivyo na wao wanakuwa na uwezo wa kujisaidia
na kusaidia wengine katika familia zao. Agness katika miaka yake ya 20
anapendeza kwa umbile lake lililojaa sihiri pamoja na kwamba bei yake yeye ni
nafuu ya shilingi 5,000 tu bado hakuwa na uwezo wa kutengeneza fedha nyingi
kama wenzake wengine, lakini amesema hakuna siku anayolala na njaa, wateja
wapo.
Kwa watafuta huduma ya kuliwazwa,
wanatumia fedha kwa kuwa kesho itapatikana fedha nyingine, machimbo yalikuwa
poa sana, yalikuwa yanatema na biashara ya mahindi ni nzuri pia, fedha zipo
Mpanda na mzunguko katika shughuli za aina hii upo kwa sana.
Ofisa maendeleo wa Mpanda, Grace
nilipomuuliza kuhusu vijana kesho yake na matatizo wanayokabiliana nayo,
alizungumzia mahitaji ya fedha kiurahisi kunachochea mambo mengi ambayo si
mazuri ukiwemo ukahaba.
Anasema kwamba upo ubishi wa wazi na
kutojituma miongoni mwa vijana, ingawa anajua biashara ya ukahaba inayofanyika
Mpanda washiriki wengi si wakazi wa Mpanda, bali wageni waliokuja kutafuta
fedha. Wapo wanaotafuta madini, wapo wanachimba madini na wapo waliokuja
kufuata fedha za watafuta na wachimbaji madini.
Mpaka sasa hakuna mvutano wa wazi
kati ya Polisi na makahaba hawa ambao kuanzia saa 12 jioni hutega mingo zao
uwanja wa Fisi wakitarajia biashara hadi usiku wa manane. “Unaweza kuja hata
saa nane hapa na kukuta loose, “ alisema Jovin (si jina lake) ambaye kazi yake
ni dalali wa madini ya shaba.
Kwa wanafunzi wanaofanya ukahaba,
labda ipo haja kwa taasisi za kiraia kutofumbia macho matatizo yanayoanza
kuchipuka Mpanda kwani jinsi spidi ya madini inavyozidi kuongezeka ni dhahiri
biashara ya ukahaba itashamiri na maambukizi ya magonjwa mbalimbali ya ngono
yataanza kushika kasi na serikali mwishoni italazimika kutibia watu wake kwa
fedha nyingi kutokana na ukweli kuwa mchezo wao ni mauti yetu.
KATAVI: Mkoa ulioondoa ubabaishaji
katika siasa
Na Beda Msimbe
PASI shaka ukiacha Arusha, mkoa wa
Katavi unaotokana sehemu kubwa na iliyokuwa wilaya ya Mpanda, Chadema ina nguvu
ya kutosha na miaka mwili iliyopita ilikuwa ni kama watia mafuta katika moto,
kulikuwa na ukakasi mkubwa katika siasa.
Ukakasi huo ulifanya sehemu kubwa ya
shughuli za maendeleo ama kusuasua au kudumaa kutokana na mvutano wenye lengo
la kuonesha nani mbabe katika siasa za kuendesha maeneo.
Lefi Matongo ambaye ni kiongozi wa
chama cha CHADEMA na diwani wa kata ya Kashaulili kati kati ya mji wa Mpanda
katika mazungumzo anasema hivi sasa ni shwari, Katavi kutokana na ukweli kuwa
hivi sasa siasa za ubabaishaji zinaelekea mwisho.
Nilipotaka kujua zaidi nini
kinatokea alijibu kwa utaratibu sana:” Hii ni kutokana na wananchi wengi kuwa
na uelewa kuhusu mambo mbalimbali.” Ni kweli huenda siasa zimepanuka sana na
kuwafanya watu wawe na taratibu za kuvumiliana ingawa ni dhahiri bado yapo
maeneo ambayo siasa zinatakiw akubadilishwa ili kukidhi haja ya maendeleo
katika mkoa mpya.
Eneo la Karema kandoni mwa Ziwa
Tanganyika siasa zinababatiza sana maendeleo kwani hata mtendaji wake alisema
hadhani kama watu wanafikiria vyema wanaposhindw akutafakari mahitaji yao,
nguvu zao na haja ya kutoitegea serikali katika ustawi wa jamii.
“Unauliza siasa ndugu mwandishi,
hapa siasa ina shida vyama vinazuia maendeleo, hata Diwani wa hapa ambaye ni wa
CCM naye anaendesha siasa zisizoeleweka anawataka wananchi kutochangia
maendeleo” alisema mtendaji huyo,katika mazungumzo huku tukiwa katika eneo
linapojengwa bandari mpya Karema.
Pamoja na karema kuonekana kuwa na
tatizo lakini kw aujumla vingunge wa siasa wa Katavi yaani Chadema na CCM wanakubaliana
kwamba hali kwa sasa imebadilika sana na watu wa Katavi wanashirikiana katika
kukabili changamoto zao katika sekta ya maji,kilimo na elimu.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi,
Abdalah Mselem yeye anashukuru kwa mshikamano uliopo baina ya viongozi wa siasa
mkoani kwake ambao unaonesha kukomaa kisiasa. Anasema Katavi kwa sasa
wanaupinzani usio wa vitisho wala chuki binafsi na hivyo wanachama wa vyama
tofauti vya kisiasa wote wanashirikiana katika misiba na harusi.
Katika mahojiano na Mkuu wa Mkoa wa
Katavi Dk Rajabu Rutengwe kuhusiana na hali ilivyokuwa miaka miwili iliyopita
na sasa alikiri kuwa mkoa wake umepiga hatua kubwa katika mahusiano.
“Tumefanikiwa kukuza mahusiano kati ya serikali, Chama tawala na wapinzani na
hivyo kuongeza kasi ya kusaka maendeleo miongoni mwa wananchi wetu” alisema Dk
Rutengwe kwa kujiamini.
Dk Rutengwe ambaye kabla ya kuwa
mkuu wa mkoa huo mpya alikuwa mkuu wa wilaya ya Mpanda alisema hivi karibuni
katika mahojiano na gazeti hili kuhusu hali ya kisiasa ilivyo kwa sasa mkoani
humo kuwa kwa sasa hakuna hali tete.
Alisema, ingawa miaka miwili
iliyopita hata kabla ya kuanza kwa mkoa mpya hali ya msuguano ilikuwa tete,kwa
sasa hali hiyo haipo na kwamba wananchi wanaanza kuelewa umuhimu wa kusukuma
mbele kazi za ujenzi wa taifa huku upinzani ukibaki katika hoja zaidi kuliko
hitilafu.
Kipindi cha nyuma msuguano mkubwa
ulikuwepo kati ya mashabiki wa Chadema na mamlaka mbalimbali za serikali na
chama tawala hasa katika masuala ya maendeleo. Mbunge wa Mpanda Mjini na Makamu
Mwenyekiti wa Chadema, Said Amour Arfi, anadaikuwa kuwa chachu kubwa ya
mabadiliko kutokana na jinsi anavyokabiliana na wanachama na mashabiki wenye
jazba wa chama chake katika mkoa huo.
Mwandishi mmoja wa habari ambaye
nilipata nafasi ya kuzungumza naye katika kupanuana kuhusiana na suala la siasa
katika mkoa mpya alisema kwamba kama si Arfi kutia mikono na miguu yake kila
mara na kila mahari huenda yanayotifuka huko Arusha yangelitokea na hapa.
Ukizingatia ukweli kuwa Katavi kuna
kambi ya wakimbiziambao wengi wao hawakusalimisha silaha walipoingia, kuwepo
kwa mitikisiko ya kisiasa isiyozingatia hali halisi ingelikuwa balaa kubwa kwa
mkoa huo mpya na taifa pia.
Kambi ya Katumba iliyopo Katavi
imebeba sura nyingi na inaweza kutumiwa kisiasa kama watu wasipokuwa waangalifu
na kutulia kwa hali ya kisiasa kunatokana na vinara wa usalama (Vyama husika
vya siasa) kutambua hilo na kuamua kushirikiana kuhakikisha kwamba wanakomesha
ujambazi na kutotumika kuharibu amani na maendeleo ya mkoa.
Katika mazungumzo Dk Rutengwe
alisema Kwamba serikali ya mkoa ilifanyakazi kubwa ya kuondoa na kudhibiti
mawazo hasi ya kimaendeleo ambayo yalikuwa yanakwamisha juhudi za kumkomboa
Mwanakatavi.
“Maendeleo yataletwa na wanakatavi
wenyewe;kubuni,kupanga, kutekeleza mipango yenyewe inawezekana tu kwa kuwa na
utashi usiozingatia itikadi bali hoja muhimu ya maendeleo” alisema Mkuu wa mkoa
na kuongeza kuwa wananchi wa Katavi kwa sasa wanatambua kwamba kuna umuhimu wa
kuhimizana maendeleo na si siasa za majitaka.
Mkuu wa mkoa alisisitiza kwamba mkoa
wake wenye dira ya maendeleo ya miaka 20, dira ambayo inawaelekeza wanakatavi
namna gani waende na kuweka maeneo yao katika hali tayari kuchangia uchumi
binafsi wilaya,mkoa hadi taifani haiwezi kufanikiwa kama siasa zitakuwa hovyo,
ndio maana muda mwingi ametumia kutengeneza amani ili dira hiyo itekelezwe na
wananchi wa Katavi wafaidi mali asili zao.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa mpango
huo umegawanyika kati ya muda mrefu na muda mfupi, mpango ya muda mrefu
ikilenga pamoja na mambo mengine kuiwezesha Mpanda kupata hadhi ya manispaa,
siasa za wastani zinazoonyeshwa sasa zisizokuwa na jaziba zitaifaidisha.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa alikiri
kuwapo kwa changamoto kadhaa ambazo zinaweza kabisa kusaidia watu kupingana
bila jazba bali maendeleo. Kauli yake hiyo inafanana kabisa na matamshi ya
Thomas Ngozi mzee maarufu katika mkoa wa Katavi .
Mzee huyo anasema inaonesha hivi
sasa siasa zinabaki ni za vijana kwani kumekuwa na wigo mpana sana wa kutoa
fursa kwa vijana hivyo ni mategemeo yake kwamba watatumia busara za wazee
kutengeneza amani kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wao.
Wakati wa mazungumzo alikuwa muda
wote akiwataka wakuu wa vyama kusisitiza amani na kuipa kipaumbele katika siasa
zao badala ya kuhangaika kuchovya maneno kwa lengo la kushika dola pekee na
kuacha mambo yanaharibika.
Kwa mkoa wenye kuamka na kuwa na
shughuli nyingi za madini na tarafa sita za utawala zilizotawanyika katika
mbuga kubwa na ndogo ni dhahiri utulivu wa kisiasa unaweza kabisa kutumika
kutengeneza maendeleo na kuzuia kuporwa kwa mali ya mkoa huo.
Tarafa kama za Karema, Mwese,
Kabungu, Inyonga, Nsimbo na Mpimbwe zinaotengeneza kata 33 zimetawanyika sana
katyika Hifadhi ya taifa ya Katavi huku nyingine zikiwa katika hifadhi ya
Inyonga inayozalisha asali.
Ni dhahiri utekelezaji wa dira ya
maendeleo ya miaka 20 katika mkoa ambao ndio kwanza unaanza safari ya
maendelkeo huku ikiwa na raslimali nyingi ambazo unatakiwa kufanywa kwa
mashirikiano makubwa kati ya waqzawa, wageni na wanasiasa, serikali yenyewe ni
kusimamia mipango hiyo.
Mashirikiano ya makundi ya kikabila
kama Wabende, Wakonongo, Wafipa, Warungwa na Wanyaturu ambao wanaishi Inyonga,
Karema na Mishamo kwa upande mmoja na Wapimbwe, Wanyarwanda, Wachaga, Wasukuma
na Wamasai wanaoishi Mpimbwe, Mwese, Nsimbo na Ikola kwa upande mwingine
utakuwa ni faraja kubwa.
Makundi haya ya makabila ambayo
mengi ni ya wafugaji na wawindaji utulivu wa kisiasa utawezesha pia kudhibiti
matatizo yanayotokana na ukimbizi . Katavi ina makambi mawili ya wakimbizi ya
Mishamo na Katumba yanayohifadhi watu wa kabila la Wahutu kutoka Rwanda na
Burundi kuanzia miaka 1972 japokuwa wengi wamepewa ukazi,makubaliano yao ya
ukazi bado kutekelezwa.
Siasa za Katavi pia zinasaidiwa na
kuwapo kwa machifu wa kikabila ambao wanatumika kurekebisha mambo katika jamii.
Machifu hawa pia wamemtambua mkuu wa mkoa kama Chifu wao mkuu kiasi ya kwamba
maagizo ya serikali yamekuwa yakiwafikia na kuyasimamia kwa maslahi ya umma.
SAA 37 ZA DAR HADI MPANDA
.Mama moyo wangu! yaani mashaka na hofu
barabarani,msituni
.Dereva
macho pima, abiria mapenzi, kinywaji,kuchimba dawa
.Kondakta
gari halijai si ndoo ya maji,sogea kule,ukiwa mzee balaa
Habari Na Beda Msimbe
NIMETUMIA takribani saa 37 kutoka
Dar es salaam na kufika katika makao makuu ya mkoa wa Katavi, mji unaonekana
kubadilika kwa kasi wa Mpanda.Na ninachoandika hapa si hadithi ya kubuni ni
ukweli nikichukua muda hadi muda.
Majira ni saa kumi na nusu
alfajiri,naamshwa na watoto, nisije nikachelewa kwani basi linaondoka saa moja
kasoro robo na kwa utata wa usafiri wa huku kwetu nikaapo ni lazima ujihimu
kidogo.Saa kumi na moja na dakika 15 naondoka nyumbani na dakika 25 baadaye
nafika stendi ya kunipeleka Kimara, hakuna basi , muda unaenda naamua kuchukua
pikipiki.
Saa kumi na mbili na nusu
ninafika Kimara, nasubiri basi litakalonichukua hadi Mpanda kwa kupitia Mbeya
na Sumbawanga, sikujua kwamba nitalazimika kulala Mbeya, wenyewe waliniambia
kwamba niwape 67,000 na nitafikishwa Mpanda hawakunipa hadhari kwamba ni lazima
nijitegemee kulala Mbeya na tena nikifika Sumbawanga ni lazima niingie katika
gari nyingine na hivyo kuhamisha mizigo yangu.
Moja kasoro nikawapigia simu
kwamba abiria wenu wa Kimara nawasubiri,wakaniuliza gari la saa
ngapi,nikawaambia la moja kasoro wakasema linakuja wakanitajia gari namba 616
kwamba ndilo litakalonichukua kuelekea Mpanda, mkoa mpya wa Katavi.
Wakati nashangaa kunataka
kutokea nini pale kituoni daladala akabanana na basi ninalosafiria,akalambwa
kioo nikasema ohoo ishakuwa nuksi tena, manake hapa hamjatoka Dar, dereva
kaonesha kutojua upana wa gari lake.Nikalifuata pale nikaingia, wakamalizana
tukaanza safari kuelekea Mpanda.
Mbezi tukachukua abiria mbele kidogo
tukaanza mwendo. Basi lilitakiwa kuwa lakshari, lakini haa, ndani utadhani
halikaguliwi na Sumatra manake viti hovyo, mikanda haipo na stuff carrier ilionekana
kama inataka kuachia japo ilitengenezwa kama yale ya kwenye ndege.
Mhh sikuwa pekee yangu
aliyeshangaa, mtu aliyependa Mbezi naye alishangaa, wale waliokuwapo wakasema
what kind of a car, ilikuwa kiinglish lakini matamshi yake yalifanana na watu
wanaotoka Zambia, Wanyanja wakijiuliza ni aina gani ya gari wamo,kwani
wanatazama mle ndani silo walilooneshwa jana yake wakati wakikata tiketi
linapiga madebe kwelikweli kwa ndani.
"Halafu konda hii bei ni
ya lakshari kinywaji kipo? manake basi lenyewe halielewekieleweki"
alijibiwa kiinywaji kipo lakini he Dar hadi Mbeya tulipewa kwa lazima
Cocacola ya kwenye plastiki hawakuwa na kinywaji kingine na wala maji
hawakutoa.Walitupa kinywaji hiki kabla ya kuingia Doma, mara tu baada ya
kumaliza kuchimba dawa.
Mbali baada ya kuanza kupata mwendo
tukaingia foleni ya Kibaha na mbele ya Kibaha akapanda mama analalamika
kwelikweli kaachwa na basi la kampuni hiyo,kumbe asubuhi kampenuni ile iliamua
kukodisha basi bila taarifa kwa watu wakajiendea tu,.
Njiani jamaa anaovateki magari
matatu manne na unajua barabara ya Dar-Chalinze ilivyo ikiwa na mibinuko ya
ajabu, jamaa anazipangua anaziweka, hapo roho inaanza kuwa mkononi, unashangaa
umpigie Mpinga au nani barabarani na namba walizosema wanaweka kwenye mabasi pale
haipo, unakula uchungu , mama moyo wangu! breki vuu, ghafla mnaingia kushoto.
Mashaka barabara ya lami.
Haya bora salama, Mungu
anasaidia mnaacha miti ikirejea nyuma na nyie mkisonga mbele mnaingia Morogoro,
stendi ya Msamvu unapumua,mnapakia abiria wengine, wanatoa chati kwa Sumatra na
Polisi wanaikagua wanaruhusu mnaingia barabarani tena mnaanza kuitafuta Mikumi,
Mbele kidogo kabla ya kufika Doma Kondakta anaelezea suala la kuchimba
dawa. Wazungu kama tisa hivi waliokuwa mle ndani hawakuelewa nini kinatokea.
" kuchimba dawa,
anashangaa .. "kuchimba ni to dig, dawa medicine maana yake nini
hasa" akajiuliza mtu aliyeonekan anajua kiswahili zaidi na wenzake
walitaka maelezo.Watu hawakuzungumza Kiinglish lakini walipoona, watu
wanateremka waliteremka na wakabaini kwamba ni suala la kujisaidia.
Unakumbuka maneno ya
kuwa na vyoo kwa ajili ya abiria njiani , choo kile kinauwezo wa watu watatno,
abiria sitini, wengine na wazungu kadhaa waliingia msituni huku karibu na
barabara kunagulio la nyama.
Mnamaliza kuchimba dawa
mnaingia , mnapita mbuga ya mikumi na spidi 110 wakati wenyewe wameweka matuta
na kusema spidi inayofaa ni nusu yake, unashangaa mkikutana na tembo, ama tembo
ama nyie.
Njiani sasa simulizi zinaanza
zimeanzia katika suala la kuchimba dawa. Masimulizi yanahama kushutumu serikali
na matamko yake,wakaingia hapo kuzungumzia urais na nia za akina fulani
wakiwataja kwa majina kwamba wanawania Urais huku wakiwa wagonjwa na wala
hawawezi kabisa kuongoza taifa.
Siasa za kuanzia Morogoro hadi
Comfort zilikuwa za wastani, wakichamba elimu na kusifia namna watoto
wanaojifunza Uganda walivyokuwa na akili kuliko Tanzania kwa kuwa wanajua
kupepeta Kiingereza.
"ahh kwa wale wa Uganda
labda kiingereza lakini uchambuzi na uelewa bure kabisa" niligeuka
kutazama wanaozungumza nikagundua ni vijana. Hawa walibishana kwelikweli manake
walisema kwamba mfumo wa elimu tanzania bado ni bomba mwingine akisema
kwamba si kweli elimu ya tanzania imeoza watu wanajiumajiuma katika kujieleza.
Comfort, pale Kitonga
tuliingia mapema,pamoja na ukweli kuwa enoe limechakaa, hata akili za watu
zimechakaa sana kwani wanauza bidhaa kama wapo Mogadishu, aina moja bei ghali
urafiki haupo bure kabisa.
Mnamaliza mnaondoka, mtu
na mkewe (vijana) gari limepiga mijihoni hawakusikia wala kuona na asali
zikiwamiminika (si bure wameona juzi hawa) tuko juu kelele mtindo mzima, bahati
yao tulikuwa bado kuingia barabara kuu na mzee moja akashtuka kiti kimoja
hakina abiria.
"Mmeacha mtu na
mkewe" anasema huku mtu njiani mbele anapunga bkw anguvu kuashiria
watu wanaokimbilia gari.Walipanda hawana hata sura ya hasira wakaendelea na
asali zao.
Kitonga ilipandishwa kama
tambarare, siasa zikaelekea kwenye shimo kubwa zaidi nani anafaa kuwa rais,
wote wakawa wanajadiloiana wagombea wa CCM badala ya kuangalia na vyama vingine
unasema kaazi kwelikweli.Ukimtazama dereva, haongei na mtu anabadilisha
gia,anakanyaga mafuta huku mguu upo kwenye brekiu kama anaibia vile, staili
ngumu zaidi. Kwa mwendo ule lazima awe macho pima.
Saa tatu mnaingia Mbeya,
unadhani mnaendelea:"wale abiria wa Mpanda na Sumbawanga tukiingia mjini
mfike ofisini kwa maelezo, mshuke na mizigo yenu"
Kweli tulifika maelezo ni kuwa
uripoti saa kumi na moja na nusu na basi linaondoka saa 12 kamili kuelekea
Mpanda nba wale wa Sumbawanga wakaambiwa saa mbili asubuhi. Wapi pa kulala,
mzee sio ndege uko tranziti, wewe tafuta gesti zipo nyingi la maana kesho
uawahi.
Naam linakushuka,usiku wewe
mgeni, unampa mtu buku anakutoa kidogo stendi anakufikisha gesti inaitwa sinahela.
Unalala, umechoka hata hujui itakuwaje saa kumi na moja hiyo unaomba msaada wa
kuamshwa na mlinzi. Unagusa maji ya baridi, unauliza maji vipi unaletewa maji
ya moto unaoga na fasta unalala.
Wala uhitaji kuamshwa kwani usingizi
wenyewe unao,?Anafika kukugongea anaukuta wewe unatoka kuoga angalau
uchangamke. Unasubiri kupambazuke unauliza je salama anakuambia salama.
unaondoka na kufika stendi.
Unauliza ofisini basi la
kwenda Mpanda wanakuambia mngoje mhusika. Mhusika haji unatoka nje unaenda
katika magari unauliza la Mpanda wanakuonesha unasema duhh hii kali unaingia
kukaa katika kiti cha pembeni aliyekaa kala kiti kimoja na nusu halafu
unajiangalia mwenyewe.
pembeni mwako wapo watu na asubuhi
ile wanazungumzia siasa, masuala ya sensa na jinsi wengine walivyogomea sensa.
Siasa za kuanzia Mbeya
kuelekea Mpanda zilikuwa ni ukali wa Chadema,na kutokuwa wavumilivu. he mwenzio
kama jamaa yangu na khanga yake ya CCM kafua kaianika wanakuja watu wenye
nyumba wanaanza nani kaweka balaa hili atowe mara moja, khanga ile si ilikuwa
na maji wakamlaimisha aiondoe pale.
"Jamani chadema sijui
vipi yaani washari shari".
Tukaondoka kondakta akisema
wazi hataki mtu wa kusimamisha huku dereva akilalamikia upangaji mbaya wa
mizigonutamletea taabu kwenye mizani. Tuliondoka njiani kote hakuna kupandisha
wala kuongeza tukapita mizani, tukaingia Tunduma tulipoachana na Polisi wa
Tunduma na kutokomea zaidi katika barabara ya vumbi inayojengwa, basi lilikuwa
halijai labda ndoo ya maji.
Akaingia mtu mzima akaona
haina maana akaweka begi lake, akalikalia konda akasema we wala bibi hakujibu,
mdada mmoja akasema mhh wazee hawa wana lao, jamaa anasema wala hamjibu
anayetaka kupita aende nyuma yake na apite tu, anagemesha bega lake pembeni
umruke. Inayojaa ndoo ya maji si basi.
Njiani wanapanda wawili,
mvulana na msichana inaonekana wanajuana. wanakimwaga cha nyumbani lakini
mvulana akamuona demu mmoja rangu ya chungwa amesimama, akamwambia binti
aliyeingia naye aanzishwe swaga za mapenzi, jamaa alisahau kwamba kibantu
tunasikilizana kwa asilimia 50 nikafuatilia maagizo.
Mapenzi yalinoga sana katika
gari hili la Mbeya kwenda Mpanda. Jamaa alikuwa tayari kumshusha Laela binti wa
watu na kumpandisha gari kesho yake, mtoto akamsikiliza akamtolea nje.Akasema
anajeuri ya fedha alikuwa anafika laela kununua spea ya pikipiki yake, kisha
simu hiyo inayothibitisha kwamba ni dereva wa pikipiki jamaa anatafuta usafiri
akamwambia yupon garini anaenda laela kutwaa spea ya waya wa eksereta
umekatika.
Anamaliza anaendelea
kumpelekea rapu za mapenzi msichana yule hadi anafika laela akitaka kumpa fedha
za kushika:Nikasema watu wanahatari humjui mtu katoka wapi unataka kushuka
naye.
Masikio yangu yalikuwa na utamu
mkubwa, huku mapenzi, huku uongozi ujao na katiba huku mama mmoja akisema kwamba
haoni sababu ya kupiga kura,wengine wakisema ni wajibu wake kuchagua viongozi..
wewe wanakusaidia nini au tuseme wameshakusaidia nini.
Masikio yangu yalinogeshwa na
siasa,mapenzi yanaendelea na kisha inakuja suala la barabara. Vumbi linatimka
watu wamefunga vioo kondakta akagundua wageni wengi ndani ya basi. jamani
msifunge vioo tutakufa wacheni vumbi liingie na kutoka. Basi limejaa
ndindindi. lahela sick love boy akashuka na mbele kidogo tukanasa katika maji
madogo kwenye barabara inayotengenezwa.
He tunashtukia tunaelekea
katika majumba ya watu basi limeacha njia, vile vimaji kidogo katika barabara
viliharibu kabisa eneo tunalopita. maji yale yalimwagwa katika barabara
inayojengwa. Mhh ilituchukua dakika 15 kutoka hapo, watu wengine waliamua nkutumia
muda huo kuchimba dawa.
"hawa wajanja wanataka
kumaliza barabara hii muda mfupi nkabla ya uchaguzi kujipa maileji"
anasema mtu mmoja.Ahh tunajenga na madafu yetu tunachelewa kodi hatulipi..
hapana bwana fedha hizi mbona ni za MCC. " Nakuambia kumbe watu wanajua na
uwezo wa kubishana upo, wanasema kuhusu uchelewefu halafu wanauliza rais
kwanini alimuondoa Magufuli.
Baada ya kukamata mwendo sasa
ukafika muda rasmi wa kuchimba dawa, watu waliposhushwa kulikuwa na mti wa
matunda pori, wenyeji wanajua wakaanza usijisaidie hapo( kwa lile neno halisi)
kuna matunda , watu wakenda mbali kujisaidia wakirejea wanachukua matunda hata
dereva ilituchukua muda kuondoka hapo.
Kutoka nhapo ikawa pandisha
shusha,ingia kushoto ingia kulia mpaka tukafika Sumbawanga saa 9 na
nusu.nimechakaa kwa vumbi na kutokuwa na mahali pa kuegemea. nabanwa na
mwanamama aliyejaliwa na katikati kuna mtu wa kufa mtu wamesimama.mambo hayo
nikatulia watu wakawa wanashuka. Mara mzee kama unaendelea Mpanda ni basi hilo
la pili hili hapa ndio mwisho wa safari.
Maskini mie nabadilisha basi
mara ya tatu kw atiketi moja ya Dar-Mpanda. Nikachukua vitu vyangu
nikaingia basi la pili, hapana mzee kwanza ofisini ukabadilishe tiketi.Vitu
vyangu? Hapa Sumbawanga atakayekuibia lazima awe taahira.,
Unaweka begi kubwa unaondoka
na beki lako dogo lenye vifaa vyako vya kazi.
Unabadilisha tiketi. Unaingia
msalani kumeandikwa bei 200 unatoa hela unaambiwa bei 300 zi ile iliyoandikwa.
Basi linaondoka saa kumi
hapa Polisi wanafanya kazi yao wanasema zipo namba kama dereva anajaza au
kukimbia tupigieni safarini salama. kweli basi lile lilikuwa na namba za RPC wa
Rukwa, Mbeya, katavi na Dodoma. Mnaanza safari,mazungumzo hapa
yanabadilika, watu wote wamechoka wanatazama saa, simu zinaanza kuingia.
Kila anayejibu analalamika kuchelewa
kwa gari, kumbe tulitakiwa kuwa Sumbawanga saa saba ili saa moja tuwe Mpanda.
Jirani yangu akanisimulia
jinsi ilivyo hatari kusafiri usiku na kwamba basi lile lilishawahi kufanyiwa
kitu mbaya na dereva yule yule. Watu walikusanywa simu na fedha huku mkusanyaji
akiwa ni dereva wa Fuso lililotekwa kabla yake.
Paniki zinaanza kuingia, huwa
natembea na chuo kidogo cha sala, pamoja na kumuomba raphael, malaika mkuu kuwa
nami safarini pamoja na abiria wengine na kumchunga dereva asifanye maamuzi ya
kipuuzi nilianza safari ya mateso ya Kristo, kuomba ulinzi kamili kwangu , basi
na abiria wengine kwa maana kulikuwa na wanawake wengi katika basi na watoto na
kila mmoja kwa namna fulani alionekana kugwaya.
Dereva alichapa mwendo na
wakati kiza kinaingia tulikuwa njia panda ya kwenda bandari ya Debwe, dakika 15
za ukweli zamkuchimba dawa, hakuna hata choo cha kulipia watu wakajitoma katika
vichaka vichafu unachagua tu pa kuweka uchafu wako pia.
Dakika 15 ziliisha na kisha
tukaanza mwendo tukaingia katika Mbuga kila mtu alikuwa kimya mbele kidogo
kwenye kiteremko kibaya gari likasimama, akashuka Kondakta, mara dereva akasema
Hassa mbele yako simba, watu wote wakataharuki, mama mmoja akafungua simu
akaanza kusoma duwaa,kiza kilikuwa kimetenda.
Yule mtu akaingia tukaanza
taratibu kushuka,mama mmoja jirani yangu akasema pale si pazuri hata kidogo
wakiweka mtego hatuwezi kupona, lakini jambazi anayekaa msitu wa simba naye
lazima awe kanuia kufa. Lakini ni katika hifadhi watu wanatekwa. Paniki,
nikasema damu azizi ya Kristo iliyomwagika msalabani tuondolee kiwewe. hata ile
ya Getsmane sikuikumbuka. Kila mmtu alionekana kivyake sana.
Saa mbili usiku bado tupo
katikati ya msitu, unaowaka moto na baadaye tukaupita tukakutana na magari kadhaa
na saa tatu kasoro tukaona umeme, dalili ya kumalizika kwa msitu,lakini kumbe
watekaji nayara ndio maeneo yao, kijiji cha kwanza tu kutoka mbugani.
"Naomba nishuke
..."sikusikia alisema kama kwa kilugha lakini aliyeshuka usiku ule eneo
lile lisilokuwa na umeme alikuwa na watoto sita akiwemo mchanga mgongoni, watu
wakasema jamani usiku na watoto,ulikuwa usiku lakini kile kilikuwa kijiji,
mbele watu walikuwa wakitembea.
Tulipiga mwendo, mbele zaidi
kiboko akawa ametulia katikati ya barabara.Jamaa akafunga breki akazima taa
akawasha. akazima tena. Alipowasha kiboko yule akajiondoa pale barabarani
tukapita.
Saa nne tunaingia Mpanda hoi
bin taaban, kasheshe za kutafuta mahali pa kulala.Muungwana mmoja alifika
akanipokea akanifikisha nyumba ya wageni,tukala saa tano na sita kamili
nilijitupa kitandani sikujua kinaendelea nini.
LICHA
YA KUVUNJWA UWANJA SOKA LINAENDELEA
Na Beda Msimbe, Mpanda
PAMOJA na kuvunjwa kwa uwanja pekee
wa michezo wa CCM mjini hapa,Chama Cha Soka kimesema kwamba kinakamilisha
maandalizi ya kuanza kwa ligi daraja la nne.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti
wa chama cha soka cha hapa, Seif Bakari.
Uwanja huo ambao enzi za Katavi
Rangers ulikuwa uwanja wa pili wa nje ukiachia Kaitaba kwa kuingiza mapato
ulibomolewa wiki ya jana na watu wa Tanroads, katika kuwaondoa wavamizi wa
hifadhi ya barabara.
Bakari alisema kwamba mpaka sasa
timu 7 kati ya zaidi ya 12 zimelipia ada ya ushiriki. Hakutaja timu hizo.
Alisema pamoja na kuvunjwa kwa ukuta
wa uwanja huo, wataendelea kuutumia kwa kuwa hakuna uwanja mwingine.Ukuta
wa uwanja huo unaotazamana na barabara ndio umevunjwa.
Alisema hata hivyo ligi hiyo
imechelewa kuanza kwa kuwa chama chake kimekuwa kikiratibu mashindano ya
shule za sekondari yaliyodhaminiwa na mbunge wa Mpanda Mjini, Said Amour
Arfi ambayo sasa yapo katika hatua za fainali.
Mashindano hayo yaliyoshirikisha
sekondari zote yalilenga kuibua vipaji vya watoto na kuviendeleza.
Sekondari zilizoingia katika fainali
za michuano hiyo ni Mwangaza na Misunkumilo.
SEIF BAKARI: Beki wa zamani
anayemhusudu Hussein Ngurungu 'bwana mipango'
Na Beda Msimbe,Katavi
" Utamu wa mpira ni kufunguka
bwana, wakati mwingine suala hili la kupaki basi linaudhi sana, hupati utamu
wa mpira.. mpira ufunguliwe ndio mpira unapendeza" anasema beki wa zamani
wa timu za Urambo, Coastal Sport na Ujenzi , Seif Bakari.
Beki huyo ambaye bado mwili
wake upo katika fomu na ni kiongozi wa chama cha Soka Mpanda anasema raha
ya soka ni namna inavyotandazwa na namna mshindi anavyopatikana kutokana
na ufundi wa kutandaza gozi.
Anasema ipo haja ya timu kuonesha
uwezo wake, zicheze kabumbu na mwenye uwezo atwae ushindi .
Bakari ambaye anasema kwamba soka
limemsaidia sana anasema ipo haja ya kuwapo kw ampango wa kuibua vipaji
kwa kuwa na shule maalumu na kusema TFF inahusika katika hili wanawjaibu wa
kushiriki katika kuwa na akademi za soka nchini.
Bakari ambaye alifanikiwa kumdhibiti
'bwana mipango' Hussein Ngurungu ambaye alikuwa katika timu ya taifa kwa
miaka kumi anasema analiheshimu soka kwa kuwa ndilo lililompatia kazi.Bakari
anasema hawezi kudharau soka japokuwa watoto wake hakuna hata mmoja
aliyemfuata.
Bakari ana watoto sita lakini
hakuna hata mmoja aliyetaka soka wala netiboli.
Bakari ambaye enzi zake alikuwa
anacheza nne,tatu na mbili amesema kwamba aliacha gemu kwenye miaka ya
1980 na kuanza kufundisha kutokana na maumivu ya enka wakati akiwa anacheza
Ujenzi Rukwa.
Pamoja na kuacha soka katika uwanja
aligeuka kuwa mwalimu wa soka na kuanza kufunza Ujenzi Rukwa, Katavi
Rangers na Super Star maarufu kama Kakukuku. baadaye alianza kufundisha timu
za watoto kwa kushiriki kikamilifu kunoa Mwangaza sekondari kwa miaka
minne kuanzia miaka ya 1986 hadi 1989.Kocha huyu anasema kwamba anajivunia
watu kama akina Muddy Sumri, Revocatus Kalumbe na Tabuye Mrisho ambao
walikuwa katika timu ya Katavi Rangers.
Ingawa kwa sasa yeye ni mwenyekiti
wa chama cha soka Katavi, Bakari alisema kwamba kwa sasa mchezo wa
soka kwa sasa ni gharama kubwa mkoani katavi hasa katika uendeshaji na
uwezeshaji. Kwa mkoa wa katavi ambako wadhamini ni wachache, mwalimu
unajikuta unafanyakazi zote za ukapteni, umeneja na kufanyia kazi kero
mbalimbali ambazo hazimo katika utaratibu.
Anaamini kwamba kama wakiwezeshwa
wanaweza kwenda mbali zaidi kwani soka ni mafunzo,soka ni mazoezi na soka
ni kujituma.
Akiwa amezaliwa 1954 maeneo ya
Mwanga mjini, Kigoma na kupitia shule za Mwanga Extended na Kigoma
sekondari anakumbuka watu aliotia nao ndinga kama akina Daudi salum, Abdallah
Mwinyi Mkuu na Kitulo ambaye kwa maneno yake mwenyewe alimwaminia sana
namba tisa hiyo.
Bakari ambaye kwa sasa ni fundi
sanifu mkuu umeme na elektroniki mkoani katavi anasema anakumbuka
jinsi alivyomkaba Hussein Ngurungu wakiwa Tabora pamoja na kwamba bwana
mipango huyo alikuwa anakimbiza kikwelikweli. Anasema alimkaba bwana
mipango na hakuweza kutikisa nyavu za timu yake hiyo ya Tabora.
"Lazima ujisifu kama unaweza
kumdhibiti bwana mipango, na siku ile nilimwambia hupiti na
hakupita'alisema Bakari.
Alisema nyakati hizo zilizopita
Mukebezi na Chuma pia walimfurahisha sana wakiwa uwanjani,pilikapilika
zao zilikuwa zinatisha kama Hussein Ngurungu alivyokuwa anatisha.
Analionaje soka la sasa.
Zinahitajika juhudi kubwa kufua
vipaji kwa kuanzisha shule za vipaji kwani vinasaidia sana kutambua na kutunza
vipaji, hata zamani shule kama Kazima iliwika kwa kutoa wanaojua soka kiufundi
sana,
Mwalimu wa hapa aliwachukua hata
watoto waliokuwa hawakufdanya vyema na kuwaendeleza,huu ulikuwa upenzi
wake.
Niseme kwamba upenzi ndio ulikuwa
uliifanya Kazima wakati huo kuwa na sifa ya vipaji vya wachezaji ilikuwa
inatunza vijana wanaojua nini wanakitaka katika michezo na Mwalimu wa hapa
alikuwa anazingatia hilo.
Anasema pia vilabu kama Yanga na
Simba havina budi kuimarisha timu za watoto kama nyakati za Victor
Stanslaus aliyeweza kuwatoa watu kama akina Juma Pondamali na
Matokeo."Bila kuwa na timu za watoto na kuwafunza hakuna maendeleo ya
soka, tutabaki tunanunua wachezaji magarasa ambao
thamani yake ya fedha ni duni "
alisema Kauli yake hiyo aliisema kwa mfano na kuuliza kama kweli wachezaji wa
kigeni waliopo Yanga na Simba sasa wanawazidi watoto walioiva wa hapa
nyumbani kwa thamani ya fedha wanapokuwa viwanjani."Kutegemea wachezaji wa
kununua wakati wote ni tatizo", alisema Bakari.
Pamoja na timu za watoto mikoa
inastahili kuwa na shule za vipaji maarufu kama akademi ambapo shirikisho
la soka nchini (TFF) nao wanatakiwa kutia mguu kusaidia." Hili TFF
hawawezi kulikwepa la kutengeneza wachezaji wajao" alisema Bakari na
kuongeza wanaweza kwa kushirikiana na wadau wengine.
Amesema katika kawaida ni lazima
kuandaa watoto katika kutengeneza soka lijalo vinginevyo
hakutakuwa na soka tutabaki
tukilalamika.
"Tusipowezekeza tutaendelea
kuchukua wachezaji wa kigeni wasiosaidia timu kuwa na uwezo wa kushinda na
kucheza kwa pamoja" alisema Bakari.
Dhana ya uchawi sokani
Mimi naamini kwenye mafunzo, sio
katika saikolojia ya wachawi kwani kama ni hivyo basi watu wa Katavi
na Rukwa kwa jinsi wanavyotusifia tungelikuwa tuko mbali sana katika soka
lakini sivyo.
Alisema hayo wakati mwandishi
wa habari hizi alipotaka kupata kauli ya uzoefu wakati akicheza na timu
kubwa kuhusu nguvu za kiza katika kuamua ushindi graundini.Alisema yeye haamini
katika hilo ila anajua wapo watu linawapendeza likiwa hivyo.
Alisema mara nyingi si tatizo la
kocha ni la wazee na wachezaji wenyewe kwa kutaka ushindi kwa dhana ya
kutumia nguvu za kiza. lakini mwalimu hubaki pembeni.
Alisema dhana hiyo ni potofu na hata
alishawahi kumwambia mtu mmoja kwamba wanahitaji utaalamu wa
kisayansi kushinda na sio tunguli."Mpira ni training, mkifanya vyema
katika hilo mnashinda,".
Vituko
Alisema kwamba katika maisha
yake ya soka ameshuhudia vituko vingi lakini kikubwa ni kile
kinachohusu wapiganaji wa kijeshi na
wenzao wa Polisi: Ugomvi huu wa michezo ulifanya mpaka brigedi kuingia
kati kuzima mapigano huko Tabora.
Anachopenda
kwa sasa akafikiria anapenda nini,
hakuna sinema, hakuna dansi lakini alisema kwa amani kabisa:
"Ninapenda ibada, kumtukuza
Mungu, baada ya shughuli zangu za mchana , ndiyo kusema napenda ibada"
alisema Bakari .
na Beda Msimbe
KATAVI
KUZINDUA MKOA NA MATUMAINI MAKUBWA
WAKATI serikali mkoa mpya wa Katavi
inajipanga kuzindua mkoa, mkuu wa mkoa huo Dk Rajab Rutenge amesema anaamini
kuwa miaka 15 ijayo mkoa huo utakuwa na mchango mkubwa kwa ustawi wa taifa.
Amesema kwamba kinachotakiwa sasa ni
kujipanga na kutekeleza mpango mkakati wenye sehemu tano wa kuleta
maendeleo kwa wananchi na kukaribisha wawekezaji.
kauli hiyo ameitoa katika mahojiano
maalumu na gazeti hili ofisini kwake Mpanda.
"Mpango mkakati huu
unatekelezeka na unaenda sambamba na mpango wa taifa wa maendeleo" alisema
Dk Rutenge na kuongeza kuwa mkoa huo una mpango wa miaka 20 unaotoa dira ya
maendeleo.
Alisema japokuwa mkoa huo ambao
utazinduliwa katika sherehe maalumu zitakazofanyika kuanzia 19/11 hadi 25
mwaka huu; staili ya uzinduzi umelenga kujitathmini na pia kuonesha wadau
wengine fursa mbalimbali za maendeleo na uwekezaji mkoani.
Alisema uzinduzi huo utakaombatana
na makongamano na wakazi wa mkoa huo kwa nafasi zao kuonesha nini wanafanya
katika kujikwamua kutoka umaskini, utaangalia mafanikio ya kongamano kubwala
uwekezaji lililofanyika mwaka jana.
Mkuu wa mkoa alisema wanatarajia
viongozi wakuu wa serikali kufungua na kufunga wiki hiyo ya uzinduzi.
Alisema mkoa huo wenye fursa kubwa
za uwekezaji katika kilimo cha mazao mbalimbali, na ufugaji utalii,migodi ya
madini mbalimbali yenye majina madogo na makubwa umweka kipaumbele chake
kuwapatia watu maji, bidhaa ambayo wanatumaini itafungua maeneo mengi ya
maendeleo.
Aidha alisema utalii wa ndani na wa
nje unatarajiwa kuongezeka hasa kutokana na serikali kuendelea kufungua njia na
kuwapo kwa kiwanja cha ndege cha Mpanda.
Mkoa wa Katavi umejaliwa neema ya
kuwa na wanyama wengi na wakubwa kutokana na lishe nzuri, maeneo ya matambiko
maarufu kwa wenyeji na wakazi wanaokuja kutafuta tiba,chemchem za maji
moto,mabaki ya ngome za wakoloni na ziwa lenye samaki wa aina mbalimbali.Aidha
ni eneo lenye ufugaji wa nyuki.
UWANJA
WA NDEGE MPANDA KUFUNGUA KATAVI
UWANJA wa Ndege wa Mpanda ambao kwa
sasa una njia ya kukimbilia ndege yenye uwezo wa kuchukua hata ndege aina
ya ATR 72 unajipanga kuifikisha njia hiyo kuwa kilomita 3 na kuhudumia mikoa na
nchi jirani .
Uwanja huo kwa sasa una njia ya
kukimbilia ndege ya kilomita 2.
Taarifa kutoka ofisi ya Mkuu wa MKoa
wa Katavi,dk Rajab Rutenge imesema kwamba wanataka kuufikisha uwanja huo katika
nafasi ya kuhudumia nchi za maziwa makuu na hasa baada ya kufunguliwa kwa
uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mbeya.
Uwanja huo ambao kwa sasa unatua
ndege za kukodi unafanya mazungumzo na mashirika ya mafuta ili kuweza kutoa
huduma za mafuta katika uwanja huo ambazo kwa sasa hazipo.
Hata hivyo tayari ndege za kukodi
zinatua katika uwanja huo na kampuni moja ya Mwanza imeanza kutafakari kuwa na
safari za mara moja kwa wiki, kwa kutumia ndege ndogo kutoka Mwanza.
Tayari huduma hiyo inayounganisha Mwanza,
Tabora na Sumbawanga inatangazwa kwa nguvu mkoani hapa na watu wameambiwa
wanaweza kukata tiketi kwa kutumia simu zao.
Kuanza kutumika kwa uwanja huo kwa
safari za kibiashara kutafungua zaidi biashara ya utalii katika hifadhi ya
taifa ya Katavi na maeneo mengine ya kihistoria kandoni mwa Ziwa Tanganyika.
BUSARA
ZA RC ZAONDOA MVUTANO WANAJESHI NA WAFANYABIASHARA
Mzozo kati ya wafanyabiashara wa
mahindi na wanajeshi waliopewa jukumu la kusafirisha mahindi kutoka
Sumbawanga-Mpanda hadi Shinyanga umetatuliwa na busara za mkuu wa mkoa wa Katavi
Dk Rajab Rutengwe na hivyo kuifanya kazi ya usafirishaji mahindi kwenda
inavyostahili.
Akizungumza na mwandishi wa habari
hizi kuhusu usafirishaji wa mahindi katika njia hiyo alisema kwamba kumekuwepo
na mabehewa machache mno ambayo hayawatoshi wanajeshi wala wafanyabiashara
wadogo wanaosafirisha bidhaa zao.
"Hivi karibuni ilibidi kutumia
busara ili kuleta amani" alisema Mkuu wa mkoa na kuongeza kuwa wakati
wanajeshi wanahitaji mabehewa hayo wananchi nao walianza kunung'unika kwa
kutopewa mabehewa na ndipo nilipoagiza kwamba wananchi wapewe mabehewa ili
waondoke mara moja na safari inayofuata iwe ya kampeni ya wanajeshi.
Alisema hali hiyo ilileta nafuu
kwani hata kama mabehewa 21 yaliyofika wangeligawana, wanajeshi
yasingeliwatosha na wananchi nao wasingeliwatosha na kutoridhika kuendelea na
hivyo kuleta mgongano wa kimaslahi.
Alisema ipo haja ya kuimarisha
uletaji wa mabehewa ili kampeni ya kusafirisha mahindi yote kutoka
Sumbawanga na Mpanda iweze kukamilika mapema.
kwa zaidi ya miezi miwili wanajeshi
wanahamisha mahindi kutoka sumbawanga hadi Mpanda na kuyapeleka kwenye maghala
ya Shinyanga lakini uhaba wa mabehewa unaonekana kuwapunguza kasi yao.
Jumatatu wiki hii Katibu Mkuu Ulinzi
alifika mkoani hapa katika ziara ya kukagua maendeleo ya kampeni hiyo ya kuokoa
mahindi kabla ya mvua kuanza.
Aidha naibu katibu Mkuu wizara ya
Kilimo,chakula na ushirika Mbogo Mfuta kamba naye alikuwa katika ziara ya mikoa
ya Rukwa na katavi kujionea jinsi operesheni hiyo inavyoendelea na kuweka
mikakati ya kuongeza kasi katika kilimo.
Mikoa ya Katavi na Rukwa ni miongoni
mwa mikoa inayotegemewa kama ghala la nafaka kwa Tanzania.
KARAKANA
YA WALEMAVU YAPELEA
KARAKANA ya walemavu
inayojengwa kuanzia mwaka 2008 mjini Mpanda imepelea na kufanya mradi mzima wa
kuwawezesha walemavu kujitegemea kwa kupewa elimu ya ufundi kuchelewa kuanza.
Katibu wa chama cha walemavu Mpanda,
Godfrey sadalla amesema kwamba kuchelewa kumalizika kwa jengo walilolianza
mwaka huo zinafanya juhudi za kumkomboa mlevu kukwama.
Mradi huo ambapo mpaka
utakapokamilia utakuwa ni shilingi milioni 49.8 ulipigwa jeki na TASAF
kwa shilingi milioni 9 na sasa upo katika rinta wakati SIDO walitoa baadhi ya
zana zinazotakiwa kuwepo katika karakana kama cherahani na vifaa vya
kutengenezea viatu.
Sadalla alisema kwamba ili
kukamilisha wanahitaji shilingi milioni 24 ambazo zlisema wakati wa mwenge
Mkurugenzi wa Halmashauri aliwahidi kuwachangia.
Alisema mradi huo wa karakana ambao
ulitarajiwa kutoa mafunzo ya ushonaji,ufundi wa kuunga vyuma,ufundi wa viatu na
ufundi seremala unamilikiwa na kikundi cha walemavu chenye wanachama 49.
Alisema walemavu ni watu wa kawiada
ambao wakipata elimu na utaalamu wa kutosha wataondokana na kuwa mzigo kwa
familia na hata kwa taifa.
"hatutaki kuomba, mradi huu
unataka kusaidia walemavu wote kupata ujuzi na kujiajiri we nyewe au katika
vikundi" alisema Sadalla ambaye kitaaluma ni fundi viatu.
Alisema ufundi huo alijifunzia chuo
cha walemavu Yombo.
pamoja na kuelezea mradi huo mkubwa
alisema kwamba wangelipenda kuwa na watu wa kujitolea wa kuweza kuwafunza ili
wawe na utaratibu wa maisha kama wenzao wa mikoa ya kaskazini ambako watu wa
kujitolea wamefanya kazi kubwa ya kufundisha na kuwaaminisha walemavu.
Hata hivyo alisema kama taasisi
mbalimbali zitawakumbuka na kukamilisha jengo lao wanahakika kampeni yao ya
kutaka wazazi wenye watoto walemavu wasifungie watoto wao majumbani
itafanikiwa.
KATAVI SIASA KUTOKWAMISHA MAENDELEO-RC
Na Beda Msimbe
MKOA wa Katavi umefanikiwa kukuza
mahusiano kati ya serikali,Chama tawala na wapinzani na hivyo kuongeza kasi ya
kusaka maendeleo miongoni mwa wananchi wake.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa
wa Katavi Dk Rajabu Rutengwe katika mahojiano na gazeti hili kuhusu hali ya
kisiasa ilivyo kwa sasa mkoani humo.
Alisema ingawa miaka miwili
iliyopita hata kabla ya kuanza kwa mkoa mpya hali ya msuguano ilikuwa tete,kwa
sasa hali hiyo haipo na kwamba wananchi wanaanza kuelewa umuhimu wa kusukuma
mbele kazi za ujenzi wa taifa.
Msuguano mkubwa ulikuwa kati ya
mashabiki wa Chadema na mamlaka mbalimbali za serikali na chama tawala
hasa katika masuala ya maendeleo.Katavi unaweza kusema kwamba ni ngome ya
Chadema.
Dk Rutengwe alisema Kwamba serikali
ya mkoa ilifanyakazi kubwa ya kuondoa na kudhibiti mawazo hasi ya kimaendeleo
ambayo yalikuwa yanakwamisha.
"Maendeleo yataletwa na
wanakatavi wenyewe;kubuni,kupanga, kutekeleza mipango yenyewe inawezekana tu
kwa kuwa na utashi usiozingatia itikadi bali hoja muhimu ya maendeleo" alisema
Mkuu wa mkoa na kuongeza kuwa wananchi wa Katavi kwa sasa wanatambua kwamba
kuna umuhimu wa kuhimizana maendeleo.
Mkuu wa mkoa alisisitiza kwamba mkoa
wake una dira tayari ya maendeleo ya miaka 20, dira ambayo inawaelekeza
wanakatavi namna gani waende na kuweka maeneo yao katika hali tayari kuchangia uchumi
binafsi wilaya,mkoa hadi taifani.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa mpango
huo umegawanyika kati ya muda mrefu na muda mfupi.Mipango ya muda mrefu pamoja
na mambo mengine imelenga kuiwezesha Mpanda kupata hadhi ya manispaa
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa amesema
kwamba bado zipo changamoto kadhaa ambazo zinaweza kabisa kusaidia watu
kupingana bila jazba bali kwa hoja kwa ajili ya maendeleo.
MATAMBIKO KUREJESHA UHAI NA USALAMA WA KATAVI
KUREJESHWA kwa shughuli za
matambiko katika hifadhi ya taifa ya Katavi kumeelezwa kufanikisha malengo ya
ruhusa hiyo, ya kuweka salama hifadhi na kuipa uendelevu.
Hayo yalielezwa na Mhifadhi wa
katavi Davis Mushi wakati akielezea sababu za kurejeshwa kwa matambiko katika
hifadhi ya Katavi kiasi cha miaka miwili iliyopita.
Alisema hoja ya kurejesha ruksa hiyo
inaonesha matunda kwani kumekuwepo na ushiriki wa moja kwa moja wa kulinda
maeneo ya Matambiko yaliyoko hifadhini na hivyo kuilinda hifadhi dhidi ya mioto
na uwindaji haramu.
"Ndugu mwandishi wazee
hawa wanapofanya matambiko katika maeneo yao, wakirejea nyumbani wanaelezea
umuhimu wa mizimu inayotambikiwa kuishi kwa amani na kutoharibiwa kwa mazingira
yake na hilo ndilo Hifadhi ya Katavi inalitamani." alisema Mushi na
kuongeza kuwa sauti ya wazee husikika zaidi na hivyo kupitia kwao hifadhi
itaendelea kuwepo
Katika mbuga ya Katavi kuna maeneo
takribani manne yanayofanyiwa matambiko likiwemo eneo la mzimu wa Katabi mwenye
kuleta asili ya katavi.Mzimu huo unaelezwa kuwa ni mali ya Wadembe na wapimbwe.
Mzimu huo unaowakilishwa na
miti mikubwa miwili upo kandoni mwa ziwa Katav na inasemekana hufanya maajabu
mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mushi tayari we nye
matambiko katika hifadhi wameshafanya matambiko hayo huku wao wakitoa askari
kwa ajili ya usalama wao ili wasivamiwe na wanyama wakali.
VIJANA WATAKA HUDUMA KARIBU NAO
VIJANA wa Usevya wilayani
Mlele mkoani Katavi wameitaka serikali kusogeza huduma za elimu na ufundi kwa
vijana walioko maeneo ya pembezoni ili kuwezesha vijana hao kupata maarifa
mapya kukabiliana na changamoto za ajira.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi hivi karibuni vijana hao wamesema kwamba kjuhudi hizo zisipofanyika
vijana wanakuwa na mawazo mgando kuhusu ajira na hivyo kuwa bomu la kitaifa.
"Tuna matatizo mengi sana
lakini moja linalokera ni ukosefu wa ajira. Kilimo kipo lakini hakuna msukumo
na vijana wanajibweteka tu " alisema Antony Mhanda ambaye hata hivyo
alimshukuru Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kuwapatia trekta kubwa kubadili namna
ya kuendesha kilimo katika eneo hilo.
Walisema vijana hawana elimu ya
kutosha katika mambo mengi kuanzia siasa,elimu ya demokrasia,afya ya uzazi
kutokana na kuwa katika ukanda ambao hauna vyombo vya mawasiliano redio wala
magazeti.
"Kutokana na ukosefu wa elimu
kuna tatizo la mimba za utotoni japo zimepungua. Kondomu zipo lakini elimu ya
afya ya uzazi ni kidogo" alisema Sebastian Beshumsi katika mazungumzo
hayo.
Vijana hao wamesema wanapokuwa
hawakuchaguliwa kuendelea na elimu ya msingi hawana mahali pengine pa
kujiendeleza hasa ukizingatia umbali uliopo na maeneo yenye kuendesha elimu
hiyo mkoani Katavi.
Alisema kukosekana kwa elimu
hata masuala ya ujasiriamali hayajadiliwi, kwani hata hawajui fursa zilizopo
katika kujiendeleza na kama ni suala la mikopo nini kifanyike. Usevya ipo
kiasi cha kilomita nane kutoka eneo la Kibaoni ambako ndiko nyumbani kwa
waziri Mkuu Pinda.Aidha wapo takariani kilomita 150 kutoka Mpanda mjini.
"waliofika mjini wanazungumzia
usafiri wa pikipiki, tunauhitaji san ahuku kutokana na umbali wa maeneo yetu,
lakini unajifunza wapi kuendesha pikipiki, unapata wapi fedha za kununulia
pikipiki?" alisema Mhanda na kuomba serikali kuwasogezea elimu.
MVUA KUSITISHA UJENZI WA KIGAWA MAJI KAREMA
UJENZI wa Kigawa maji
katika bonde la Nkuswe, Karema kwenye skimu ya umwagiliaji ya Karema
utasitishwa mara tu masika itakapoanza.
Kusitishwa kwa ujenzi huo
kunamaananisha kwamba mradi huo huenda ukakamilika Juni mwakani.
Awali kigawa maji hicho
kilitarajiwa kumalizika Desemba mwaka huu.
"Mvua zikianza hapa bonde
lote hili hufurika, hatuwezi kuendelea na kazi" alisema mtunza ghala
aliyekuwa eneo la ujenzi Jerome Paul.
Alisema japokuwa mto huo si
endelevu, wakati wa masika hleta kizaazaa kikubwa na kw amujibu wa takwimu
walizonazo hawawezi kuendelea na ujenzi huo katika kipindi hicho.
Alisema katika mauzngumzo
klwamba kwa sasa wanajenga gkala ndogo na ofisi kwa ajili ya kuhjifadhi taarifa
zao na zana zao wakati utakapofika.
Kwa kawaida masika katika mkoa
wa Katavi huanza mwishoni mwa mwezi wa Kumi au mwanzoni mwa mwezi Novemba na
mvua zake huwa nyingi kutokana na mkoa kuwa bado na misitu mingi.
Kigawa maji hicho kinategemewa
kukuza kilimo katika skimu ya Karema yenye wakulima wadogo wadogo.
WAKONONGO WATAMBIKIA AMANI
WATU wa kabila la wakonongo
wanaopatikana katika mkoa wa Katavi, wilaya ya Mlele hufanya matambiko makubwa
mara mbili kwa mwaka na ya dharura kila mwezi kwa lengo la kuombea amani na uchumi.
Chifu Kayamba ll akizungumza kutoka katika
makazi yake yaliyopo Iyonga, alisema amani ikipotea masahihisho yake ni magumu
ndio maana wao kila mwezi wanafanya tambiko la kuombea amani kwenye taifa.
Alisema kiongozi mwenye busara ni
yuile ambaye atawezesha amani kwani kupitia maani shughuli nyingine za
kujiletea kipato na maendeleo kinawezekana.
Aidha alisisitiza kwamba hakuna kitu
kisichokuwa na mila; mwanzo wa jambo lolote ni mila na kusikitika namna
wananchi wanavyoacha mila zao na kuzikumbatia za kigeni ambazo nyingi ni
kasumba kwa ajili ya kuwezesha kutawaliwa kwa wananchi na kutawala kwa upande
wa wakoloni.
Alisema sehemu kubwa ya matatizo
yaliyopo nchini yanaweza kuondolewa kwa kuzingatia mila ambazo zinatoa mamlaka
kwa wasimamizi kuhakikisha kuna maendeleo, amani na upendo.
"Pamoja na kwamba kuna asilimia
80 ya watu vijijini bado wakuu wa kimila hawaheshimiwi na matokeo yake
kububujika kwa maadili na kuvurugika kwa tabia nchi.
Alisema suala la demokrasia
limelemaza watu na tafsiri potofu waliyonayo, inawafanya watu kukurupikia hata
mambo ambayo hayana thamani kwao huku yakiwagombanisha na wazee wao waliokufa
(MIZIMU) ambao wanataka kuwasaidia katika shida mbalimbali.
Chifu Kayamba ll alisema mila
ni mpango wa Mungu na kila anayefuata mila hufanikiwa na ndio mmaana ili sisi
(wananchi) tusifanikiwe wakoloni walipiga vita imani za wenyeji.