Monday, June 21, 2010

HASIRA ZA MKIZI!!!!!!

MWALIMU AMTWANGA RISASI MKEWE
MWALIMU wa shule ya msingi Safu kata ya Katete Tarafa ya Matai wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa anasakwa na jeshi la polisi mkoani Rukwa kwa tuhuma za kumjeruhi mke wake kwa risasi kufuatia ugomvi baina yao.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa Isuto Mantage amesema mbele ya waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi Agosti 25,2010 majira ya saa kumi alfajiri katika kijiji hicho ambapo mwalimu Patrick
Edward (40) wa shule ya Msingi Safu alimjeruhi kwa risasi sehemu za tumboni na kiunoni mke wake Bi Agnes Mwingira (35) ambaye pia ni mwalimu wa shule hiyo.
Kamanda Mantege amesema kuwa mnamo Agosti 24,2010 majira ya asubuhi kuliibuka ugmvi baina ya mwalimu huyo na mkewe kutokana na mkewe kumtuhumu mumewe kuwa mwalimu huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi wao wa ndani.
Amesema wanandoa hao walisuluhishwa na majirani na kuyamaliza lakini muda wa alfajiri ya saa kumi ya agosti 25, 2010 ugomvi ulizuka tena yao hali iliyopelekea mwalimu huyo kumfyatulia risasi mkewe kiunoni na tumboni kwa kutumia bunduki aina ya short gun inayomilikiwa kihalali na mwalimu huyo.
Imeelezwa kuwa mwalimu huyo alipomaliza kufanya unyama huyo huku akidhani kuwa ameshamuua mkewe alichukua bunduki hiyo na kutokomea kusikojulikana pamoja na bunduki hiyo.
Majirani walipofika katika nyumba hiyo baada ya kusikia milio ya bunduki walimkuta mke wa Mwalimu Bi Agness Mwingira akitokwa damu nyingi tumboni na kiunoni bila msaada wowote ndipo walimchukua majeruhi na kumsafirisha hadi katika hospitali ya mkoa wa Rukwa kwa ambapo hali yake imeelezwa kuwa ni mbaya.
Kamanda wa polisi amesema kuwa jeshi la polisi linawahoji watu mbalimbali kijijini hapo ili kujua chanzo hasa cha matumizi ya risasi kwa mkewe huyo ambapo miongoni mwa wanaohojiwa ni pamoja na mwalimu
mkuu, mjomba wanayeishi naye, mtumishi wa ndani pamoja na majirani.
MWISHO.