JINA KUU NI TANZANIA

Na Willy Sumia, Namanyere
WATU kumi na saba wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Rukwa kwa tuhuma za kuvamia kituo cha polisi kwa lengo la kutaka kukiteketeza kituo hicho kwa moto.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa Isuto Mantage amesema Novemba 30,2010 ofisini kwake kuwa wanaoshikiliwa ni wanakijiji wa kijiji cha Wampembe wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa baada ya jaribio la kutaka kukitekeza kwa moto kituo kidogo cha polisi cha Wampembe kwa lengo la kumuua mtu mmoja waliyekuwa wanadai kuwa ni mchawi.
Amesema kuwa awali katika kijiji hicho kulitokea msiba wa kijana aliyetajwa kwa jina la Joseph Kapelo (19) baada ya kuugua muda mfupi mnamo Novemba 22, 2010 ambapo kijana huyo aligua majira ya saa mbili asubuhi nakufariki saa tano mchana kifo kilichozua mijadala kijijini hapo wakazi wengi wakidai kuwa marehemu alikuwa amefariki kutokana na imani za kishirikina.
Amefafanua kuwa baada ya kupata taarifa za kifo hicho wananchi walianza kukusanyika katika msiba na kuanza kupanga mikakati ya kummaliza baba wa marehemu aliyetajwa kwa jina la ndugu Daudi Kapelo (76) kwa madai kuwa ndiye aliyamuua mwanae huyo kwani ni miezi miwili tu tangu kijana mwingine mtoto wa huyo mzee alifariki katika mazingira ya kutatanisha kama ilivyotokea katika huo msiba.
Amesema kuwa wakati wananchi hao wakipanga mikakati hiyo taarifa zilifika kituo kidogo cha polisi Wampembe ambapo polisi wa kituo hicho waliweza kuchukua hatua ya kumuokoa Mzee huyo lakini kabla hawajafika msibani tayari Mzee huyo alikuwa ameshaanza kushambuliwa na wananchi na kuokolewa na polisi na mgambo na kasha kuchukuliwa na kwenda kuhifadhiwa kituo cha polisi kwa usalama wake.
Amesema wakati wananchi hai wakielekea kuzika walichukua jeneza la marehemu na kwenda nalo hadi kituo cha polisi ambapo waliliweka jeneza hilo hapo kituoni na kudai wanataka Mzee Daudi Kapelo atolewe humo ndani wammalize naye akazikwe na mwanae na kuanza kushambulia kituo hicho kwa mawe hali iliyopelekea askari kupiga risasi hewani lakini wananchi hao hawakuweza kuogopa na kuanza kumshambulia askari huyo na kuibua mapigano baina ya askari na wananchi wapatao 300.
Amesema kuwa wananchi hao baada ya kutawanyika walikimbia wote wakiwa tayari wameshawasha moto kituo cha polisi kikiungua ambapo askari polisi na mgambo kwa kusaidiana na viongozi wa kijiji walifanikiwa kuuzima moto huo na wananchi hao waliweza kurudi usiku wakachukua maiti ya merehemu na kwenda kuzika usiku huo huo.
Amesema mapambano hayo yaliendelea ambapo mwananchi mmoja Imelda Kayanda (46) alipigwa risasi na kufariki na Agnes Kisori(21) alijeruhiwa mguuni huku vitu vilivyoharibiwa vikiwa ni pamoja na solar panel ya kituo, vioo vya kituo vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya shilingi laki tano.
Amesema majeruhi walipelekwa kituo cha afya Wampembe na baadae hospitali ya wilaya ya Nkasi kupata matibabu ambapo hali zao zimeelezewa kuwa zinaendelea vema.
Amesema tayari jeshi la polisi limewakamata ndugu Zakaria Francis (28), Ikombe Yustini (39), Stephano Kambe (18), Benard Kabeja (16) na John Kapandila (22).
Wengine waliokamatwa amewataja kuwa ni ndugu Said Diwali (36), Vido Tuwakazi (21), Abdalah Vicent (19), Sylveter Kapala (17), Richad Bushota (19), John Mathias (58), Wilbroad Chambi (16) na Kapondo Anatoli (23) na wengine wane wote wakazi wa kijiji cha Wampembe wilaya ya Nkasi.
Kamanda wa Polisi amesema wakati watuhumiwa hao wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika na kuwa wengine waliokimbia watafuatiliwa hadi wakamatwe ili sheria ichukue mkondo wake.
Aidha kamanda Mantage ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na tabia mbaya ya kuvamia vituo vya polisi nchini hapa nchini kuwa vinalipeleka taifa kusikojulikana kutokana na ukweli kuwa hizo ni dalili za kuondoa misingi ya amani na utulivu katika jamii.
MWISHO
Na Willy Sumia, Mpanda
MWENYEKITI mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilaya ya Mpanda mkoa wa Rukwa amekihama chama chake baada ya kunyimwa fursa ya kuwa mgombea wa Udiwani katika kata mpya ya Makanyagio mjini Mpanda katika mkoa wa Katavi.
Mwenyekiti huyo Bwana Juma Mausi alihama chama chake mara baada ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa 2010 kuanza kupamba moto kufuatia kuanza kwa mikutano ya kampeni na kujikuta akitupwa nje ya timu ya wagombea wa CHADEMA katika kinyang’anyiro cha udiwani kata ya Makanyagio baada ya nafasi hiyo kupewa mjumbe wa serikali ya mtaa wa Kachoma ndugu Nziguye Juma.
Juma Mausi ambaye ndiye aliyeipokea na kuasisi chama cha CHADEMA wilaya ya Mpanda wakati wa vuguvugu la vyama vingi nchini alijikuta akikihama chama chake baada ya kubaini kile alichokieleza yeye mwenyewe kuwa CHADEMA imekamatwa na wageni na kukiita kitendo hicho kuwa ni Uvamizi wa kisiasa ndani ya CHADEMA yake.
Taarifa sahihi toka katika chanzo cha kuaminika ndani ya CHADEMA zimeeleza kuwa baada ya kuona haridhishwi na uamuzi aliofanyiwa ndani ya CHADEMA Mzee Mausi aliamua kujiunga na chama cha NCCR Mageuzi ambako alipewa nafasi ya kuwa mgombea wa chama hicho katika king’anyiro cha udiwani kata ya Makanyagio ili kupambana na wagombea wa CCM, CHADEMA na CUF.
Juma Mausi alikuwa mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mpanda hadi Agosti alipotangaza kuachana na chama hicho na kuhamia NCCR Mageuzi hali iliyopelekea CHADEMA wilaya ya Mpanda kutafuta menyekiti wa muda katika kipindi hiki cha uchaguzi ambapo chama hicho kinatetea nafasi ya ubunge jimbo la Mpanda mjini ambapo mbunge wa sasa wa jimbo hilo ni mheshimiwa Said Arfi wa CHADEMA.
mwisho