WAKATI uchaguzi wa viongozi wa chama cha mapinduzi katika ngazi ya
Wilaya ukiwa ukiendelea nchini kote ,Wilayani Chunya hali imekuwa
tofauti baada ya wajumbe wa mkutano wa uchaguzi kupata ajali na
kusababisha kifo cha Katibu w uchumi na fedha Tawi Madimbwini kata ya
Mamba, Issaya Nchimbi (45) wengine  85 kujeruhiwa vibaya.
Mwandishi  Esther Macha anaripoti kuwa ajali hiyo ilitokea juzi majira ya 2:30 asubuhi katika kata ya
Matundasi, baada ya dereva wa gari aina ya Fuso lenye namba za usajili
T 420 APM kushindwa kulimudu na kupinduka mtaroni.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Chunya, Dk. Henry
Mwansasu, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa amepokea
mwili wa mtu mmoja pamoja na majeruhi 85.
Alisema kati ya majeruhi hao, 11 hali zao ni mbaya na wamelazwa
hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi, huku
majeruhi 63 ambao walipata mshtuko na majeraha madogo madogo
wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Akizungumza na gazeti hili  katika Hospitali ya wilaya ya Chunya,
mmoja wa majeruhi hao, Bw. Frank Bone (40), Mkazi wa Lupa Tingatinga,
alisema mbali na ajali hiyo kusababishwa na dereva ambaye alitaka
kupokea simu huku gari likiwa kwenye mwendo mkali, pia gari hilo
lilikuwa limajaza abiria kupita kiasi, hivyo muda mwingi wa safari yao
lilionekana kumshinda dereva.
Alisema kuwa walilianza safari  yao kutoka kijiji cha Mamba  majira ya
 saa 9:00 usiku na kuwapitia wajumbe wengine wa kata za Lupa na Upendo
,hivyo wakajikuta gari likiwa limejaa kupita kiasi na kusababisha
abiria wengine kusafiri wakiwa wamening’inia kwenye mabomba ya vyuma.
Kwa upande wake Bw.  Jamson Mwaluka, Mkazi wa kata ya Lupa, ambaye
alijeruhiwa kwenye paji la uso, alisema kabla ya ajali kutokea dereva
wa gari hilo,aliyetajwa kwa jina moja la Mchungaji, alisema chanzo cha
ajali hiyo ni simu ya mkononi.

“Dereva alipigiwa simu iliyokuwa mfukoni, wakati anahangaika kuitoa
gafla alijikuta yuko kwenye kona na alipojaribu kuliweka sawa ndipo
gari lilipoteza muelekeo na kupinduka,” alisema Bw. Mwaluka.
Kwa mujibu wa majeruhi hao, gari hiyo ilibeba zaidi ya watu 100 ambao
wote walikuwa ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa CCM wilaya ya
Chunya, kutoka kata tatu za Mamba, Lupa Tinga Tinga na Upendo katika
jimbo la Lupa.

Hata hivyo licha ya kutokea kwa ajali hiyo, mkutano wa Uchaguzi
uliendelea kama ulivyopangwa, huku baadhi ya majeruhi walioruhusiwa
kutoka hospitalini nao wakijumuika kushiriki kwenye uchaguzi na
wengine ambao wamelazwa wakiandaliwa utaratibu waz kupiga kura wakiwa
wodini.