Sunday, August 22, 2010

CHAKACHUA YA PINDA YAISUMBUA CHADEMA

Na Willy Sumia, Mpanda
WAZIRI mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda ambaye amepita bila kupingwa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Katavi mkoa wa Katavi kumeelezewa na wananchi wa jimbo lake kuwa ni uamuzi wa siku nyingi kabla hajateuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Hayo yalielezwa na baadhi ya wananchi wa jimbo hilo katika mahojiano ya hivi karibuni na waandishi wa Habari mara baada ya tume ya uchaguzi jimbo la Katavi kutangaza kuwa Pinda amepita bila kupingwa kutokana na wagombea wane wa CUF, CHADEMA, NLD na CHADEMA kujitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa barua.
Wananchi hao wanaotoka katika vijiji vya Ilunde, Ilela, Majimoto, Kasansa na Kilida walidai kuwa tangu Pinda awe mbunge wa jimbo lao lililokuwa awali likiitwa jimbo la Mpanda Mashariki kumekuwa na maendeleo makubwa pamoja na mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi hao.
Ndugu Hussein Omari mkazi wa kijiji cha Inyonga alisema kuwa wananchi wa tarafa ya Inyonga walikuwa wakiteseka sana kutokana na kukosekana kwa barabara ya uhakika na mawasiliano ya simu lakini tangu Pinda awe mbunge wao wameweza kupata miundombinu hiyo kwa kasi ya ajabu.
Mmoja wa wagombea waliokuwa wametangaza nia ya kugombea katika jimbo hilo ndugu Sebastiani Kasinge alisema kuwa mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge jimbo la Katavi kwa Pinda alipata upinzani mkubwa sana toka kwa wananchi wa jimbo hilo, ndugu zake na hata ndani ya Chama chake cha CHADEMA.
Alisema kuwa uamuzi wake wa kuchukua fomukatika jimbo hilo ulipelekea mvutano mkubwa ndani ya CHADEMA na kupelekea mbunge wa jimbo la Mpanda kati CHADEMA Said Arfi kutangaza kujitoa katika uchaguzi iwapo chama chake kingesimamisha mgombea jimbo la Pinda ambapo mwenyekiti wa CHADEMA mwasisi aliamua kujivua uanachama wa CHADEMA na kuhamia chama kingine cha siasa katika kikao kilichokuwa kikijadili wagombea.
Chanzo cha uhakika cha habari toka katika chama cha CHADEMA kimeeleza kuwa CHADEMA ndio waliokuwa wakishinikiza Pinda apite bila kupingwa katika jimbo hilo lakini baadhi ya viongozi wa CCM walikuwa wakitaka kuwepo na mgombea ili wapate mshiko wa kampeni katika jimbo hilo na kutofautiana na katibu wa CCM wa wilaya Mohamed Omary Nyawenga aliyeonekana akifanya juhudi za kweli kuhakikisha Pinda anapita bila kupingwa akishirikiana na baadhi ya wananchi wa Inyonga.
MWISHO

Nguruwe kunywa dawa za Kupunguza makali ya VVU ARVs inakuwajeeeeeee

Iringa
WADAU wa asasi zisizo za kiserikali nchini wametoa onyo kwa wafugaji na wakulima wanaotumia dawa za binadamu kuwapa mifugo na kupulizia kwenye mazao na kusababisha ongezeko la madhara makubwa kwa jamii.
Hayo yalizungumzwa na washiriki wa mafunzo ya uchambuzi wa Sera yaliyoandaliwa na Mwamvuli wa asasi za kiraia mkaoni Iringa na Njombe Iringa Civil Society Organizations (ICISO) katika ukumbi wa Lutherani
mjini Makambako katika mkoa mpya wa Njombe wiki iliyopita.
Wadau hao walisema kuwa tabia iliyoibuka hivi karibuni kwa baadhi ya wafugaji na wakulima kutumia dawa zitumikazo kwa ajili ya binadamu kwa kuipa Mifugo hali inayopelekea kuibuka kwa magonjwa yasiyofahamika na kusababisha madhara kwa walaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo.
Bwana Obothe Msemakweli mmoja wa wadau kutoka asasi ya LUCAPOA ya wilayani Ludewa alisema baadhi ya wakulima wa zao la nyanya wamekuwa wakipulizia dawa ya kuua Mbu aina ya Ngao katika zao hilo kwa lengo la kuua wadudu waharibifu wa zao hilo hali inayowaletea madhara walaji.
“Unajua wakulima wanapotosha sana matumizi sahihi ya dawa ya Ngao, imefikia baadhi ya wakulima wanapulizia katika miche ya nyanya hali inayopelekea walaji kudhulika,” Alisema Msemakweli.
Walisema pia dawa za uzazi wa mpango ambazo hutumiwa na akinamama kupanga uzazi zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya wafugaji huwapa kuku kwa lengo la kuwafanya wakue haraka ili kupata bei nzuri ya mifugo hiyo kutokana na tamaa ya pesa.
Wadau hao walisema wanyama aina ya Nguruwe nao wamekuwa wakipatiwa vidonge vya ARVs ambavyo hutolewa kwa wagonjwa wa Ukimwi ili kuwaongezea siku za kuishi na mazao ya mahindi na Maharage yamekuwa yakiwekewa dawa ya Ngao ya unga kwa imani kuwa hayatabunguliwa na Fukuzi wadudu waharibifu wa mazao.
Bi Grace Sanga wa asasi ya PROMISE ya mjini Iringa alisema upotoshwaji wa matumizi hayo ya dawa yanajengwa na uzushi ambapo wafugaji na wakulima huamini kuwa baada ya kuwapa mifugo dawa za binadamu, kuku na Nguruwe hukua haraka bila kuwa na ushauri wa kitaalamu.
Bwana Renatus Mpiluka mwanachama wa asasi ya MUNGONET ya Mufindi alifafanua kuwa hali hiyo inatokana na sera nyingi kutungwa na kuishia katika vitabu na wananchi kushindwa kuzifahamu hali inayopelekea baadhi ya wananchi kufanya mambo kinyume na utaratibu wa sera husika.
“Sera ya Kilimo, yenye kauli mbiu ya Kilimo kwanza naieleweki kwa baadhi ya wakulima ambao ndiyo walengwa wakuu wa mpango huo, kuna hajaya serikali kutoa elimu sahihi ya sera ili jamii izifahamu.” Alisema
Renatusi
Naye ndugu Leonard Kalolo mujumbe wa asasi ya LIMAU ya Mgololo wilayani Mufindi alisema wakulima na wafugaji wapatiwe elimu ili kupunguza matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizo pamoja na udhibiti wa usambaaji wa dawa za binadamu.
“Mbolea na madawa zinatumiwa vibaya, unakuta mtu anaweka mbolea hata kwenye mazao ya muda mfupi kama mboga mboga, hii inasababisha kumfikia mlaji kemikali za madawa hayo zikiwa bado hazijaisha na
kusababisha maradhi ,” alisema ndugu Kalolo.
Wadau hao wa asasi zisizo za Serikali waliitaka serikali itoe elimu sahihi kwa wakulima juu ya Sera mbalimbali zitolewazo na serikali ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi katika utungaji wa Sera
kwani wao ndiyo watekelezaji wakuu wa irani hizo.
Naye muhadhiri wa chuo kikuu cha Tumaini mkoani Iringa Lucas Mwahombela aliitaka serikali kuingilia kati ukiukwaji wa matumizi hayo ikiwa ni pamoja na kuziweka wazi sera mbalimbali hasa za Kilimo ambazo
zinawalenga watu wa hali ya chini ili wazielewe na kufanikisha sera ya Kilimo kwanza na kauli mbiu ya Mapinduzi ya Kijani.

MWISHO
Na Willy Sumia, Mpanda
MWENYEKITI mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilaya ya Mpanda mkoa wa Rukwa amekihama chama chake baada ya kunyimwa fursa ya kuwa mgombea wa Udiwani katika kata mpya ya Makanyagio mjini Mpanda katika mkoa wa Katavi.
Mwenyekiti huyo Bwana Juma Mausi alihama chama chake mara baada ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa 2010 kuanza kupamba moto kufuatia kuanza kwa mikutano ya kampeni na kujikuta akitupwa nje ya timu ya wagombea wa CHADEMA katika kinyang’anyiro cha udiwani kata ya Makanyagio baada ya nafasi hiyo kupewa mjumbe wa serikali ya mtaa wa Kachoma ndugu Nziguye Juma.
Juma Mausi ambaye ndiye aliyeipokea na kuasisi chama cha CHADEMA wilaya ya Mpanda wakati wa vuguvugu la vyama vingi nchini alijikuta akikihama chama chake baada ya kubaini kile alichokieleza yeye
mwenyewe kuwa CHADEMA imekamatwa na wageni na kukiita kitendo hicho kuwa ni Uvamizi wa kisiasa ndani ya CHADEMA yake.
Taarifa sahihi toka katika chanzo cha kuaminika ndani ya CHADEMA zimeeleza kuwa baada ya kuona haridhishwi na uamuzi aliofanyiwa ndani ya CHADEMA Mzee Mausi aliamua kujiunga na chama cha NCCR Mageuzi ambako alipewa nafasi ya kuwa mgombea wa chama hicho katika king’anyiro cha udiwani kata ya Makanyagio ili kupambana na wagombea wa CCM, CHADEMA na CUF.
Juma Mausi alikuwa mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mpanda hadi Agosti alipotangaza kuachana na chama hicho na kuhamia NCCR Mageuzi hali iliyopelekea CHADEMA wilaya ya Mpanda kutafuta mwenyekiti wa muda katika kipindi hiki cha uchaguzi ambapo chama hicho kinatetea nafasi ya ubunge jimbo la Mpanda mjini ambapo mbunge wa sasa wa jimbo hilo ni mheshimiwa Said Arfi wa CHADEMA.

mwisho

Saturday, August 14, 2010

BARABARA ZA LAMI RUKWA

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amewka jiwe la Misngi katika mradi mkubwa
wa umeme wenye thamani ya shili Bilioni 12 kwa ajili ya Miji ya
Namanyere na Sumbawanga mkani Rukwa. Mradi huo uliwekewa jiwe la msingi katika eneo la Mitambo ya umeme ya shirika la umeme nchini TANESCO mjini Sumbawanga Jumamosi iliyopita unajumuisha mashine nne kubwa zenye uwezo wa kuzalisha kilowatt 5 za umeme kwa wakati mmoja zilizonunuliwa na serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 3.
Akitoa taarifa mbele ya Mheshimiwa Rais Waziri wa Nishati na Madini Wiliamu Ngeleja alisema kuwa mradi huo wa umeme unaanza Julai 2010 na kukamilika Juni 2011 ambapo waziri huyo alimueleza rais kuwa umeme utaanza kuwaka mjini Namanyere Machi 2011. Aidha Waziri Ngeleja alisema kuwa mradi huo utawawezesha wananchi waishio katika vijiji vinavyopitiwa na nguzo za umeme katika barabara ya kuelekea Namanyere mjini kupatiwa umeme kwa ajili ya matumizi ya majumbani na matumizi mengine kama ilivyo kwa wananchi wa mijini.Waziri Ngeleja alisema kuwa Serikali imeondoa gharama za nguzo kwa wananchi wa vijijini ili kupunguza gharama za kuingiza umeme katika nyumba zao na badala yake gharama za nguzo zitakzotumika kuingizia umeme kwa wananchi serikali ndiyo itakayogharamia kutokana na ukweli kuwa wananchi wa vijijini wana kipato kidogo ukilinganisha na waishio mijini.
Naye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete aliwataka wananchi wa vijiji husika kuanza kujiandaa kuupokea umeme pindi utakapofika ikiwa ni pamoja na kuachana na ujenzi wa nyumba za nyasi kwa rais alisema nyasi hazipatani na umeme “ Ndugu zangu wananchi wa Kipande na wengine walioko katika njia hii, changamkieni umeme huu ili mpate maendeleo ya haraka, acheni kujenga nyumba za nyasi kwa sababu umeme na nyasi haviendani, jengeni nyumba bora hivi sasa ili umeme ukifika kijijini kwenu muupokee na kuanza kuufaidi” alisema Mhe. Rais Rais Kikwete alisema hivi sasa wananchi wa Rukwa neema imewashukia kwani tayari umeme wanatarajia kuupata wa uhakika, barabara nazo zinajengwa kwa kiwango cha lami na pia kuna maboresho ya kilimo kupitia dhana ya KILIMO KWANZA.
Alifafanua kuwa kilimo kikizalisha mazao ya kutosha sasa wananchiwataweza kusafirisha mazao hadi kwenye soko bila matatizo na tena wakiuza mazao kwa bei nzuri katika soko wataweza kuutumia umeme
kujiletea maendeleo na hayo ndo maisha bora kwa kila Mtanzania.

MWISHO

ACHENI USHOGA NA WATENDAJI-JK

MADIWANI wametakiwa kuacha kuwa marafiki wa watendaji na wakurugenzi wa Halmashauri zao ili kuweza kudhibiti vitendo vya ufujaji wa pesa za serikali zinazoletwa katika maeneo yao kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara mjini Mpanda katika Ziara yake Mkoani Rukwa . Rais Kikwete alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na ufujaji mkubwa wa fedha za serikali hasa zinazoletwa na serikali kuu kama ruzuku ya
maendeleo katika halmashauri mbalimbali nchini lakini zimekuwa hazioneshi kuleta mabadiliko katika jamii husika. Alisema tatizo la ubadhilifu wa fedha za wananchi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi limekuwa likiongezeka siku hadi siku na hali inakuwa mbaya zaidi katika maeneo ambayo madiwani wamekuwa na urafiki na ushoga na watendaji wa halmashauri na wakurugenzi wa maendeleo. “ Hizi pesa wanaotakiwa kuzisimamia na kuhakikisha zinafanikisha malengo yaliyokusudiwa ni madiwani lakini kwa bahati mbaya madiwani katika maeneo mengine wamekuwa wakijenga urafiki na ushoga na
watendaji wa halmashauri na wakurugenzi ambao ni wezi wao, wanaishia kupewa gawio kidogo wanaridhika na kuona mambo safi kumbe wanaibiwa maana pesa za ruku ya maendeleo ni ya wananchi na wadhamini wao ni madiwani” alisema Rais Kikwete Rais Kikwete alisema madiwani wanatakiwa kuelewa kuwa wao wana dhamanaya wananchi kuwasimamia wakuu wa idara na waandamizi wao katika vikao na nje ya vikao na ikiwezekana wachukue hatua pale wanapobaini kuwepo kwa hujuma katika pesa zao bila kusita badala ya kuiachia serikali peke yake.
“Kimsingi pesa zinzoletwa na serikali kuu kama ruzuku ya maendeleo ni za wananchi na wala si za serikali ndiyo maana sisi tunawaletea huku kwenye halmashauri zenu ili zijenge barabara, madarasa, zahanati, miundombinu ya maji na Miradi mingine ya maendeleo ya wananchi ambao ninyi madiwani ni wawakilishi wao, acheni urafiki na ushoga na watendaji na wakurugenzi wa Halmashauri zenu, wasimamieni.” Alisisitiza Rais Kikwete Aidha mkuu wa mkoa wa Rukwa alimshukuru Rais Kikwete kwa serikali yake
kuhakikisha inaondoa kero kubwa kwa wananchi wa mkoa huo ya barabara zisizo pitika mwaka mzima na kuamua kujenga kwa kiwango cha lami kuwa huo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Rukwa.

MWISHO