NKASI - WAMPEMBE - 17 MBARONI KWA KUVAMIA KITUO CHA POLISI
WATU kumi na saba wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Rukwa kwa tuhuma za kuvamia kituo cha polisi kwa lengo la kutaka kukiteketeza kituo hicho kwa moto.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa Isuto Mantage amesema Novemba 30,2010 ofisini kwake kuwa wanaoshikiliwa ni wanakijiji wa kijiji cha Wampembe wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa baada ya jaribio la kutaka kukitekeza kwa moto kituo kidogo cha polisi cha Wampembe kwa lengo la kumuua mtu mmoja waliyekuwa wanadai kuwa ni mchawi.
Amesema kuwa awali katika kijiji hicho kulitokea msiba wa kijana aliyetajwa kwa jina la Joseph Kapelo (19) baada ya kuugua muda mfupi mnamo Novemba 22, 2010 ambapo kijana huyo aligua majira ya saa mbili asubuhi nakufariki saa tano mchana kifo kilichozua mijadala kijijini hapo wakazi wengi wakidai kuwa marehemu alikuwa amefariki kutokana na imani za kishirikina.
Amefafanua kuwa baada ya kupata taarifa za kifo hicho wananchi walianza kukusanyika katika msiba na kuanza kupanga mikakati ya kummaliza baba wa marehemu aliyetajwa kwa jina la ndugu Daudi Kapelo (76) kwa madai kuwa ndiye aliyamuua mwanae huyo kwani ni miezi miwili tu tangu kijana mwingine mtoto wa huyo mzee alifariki katika mazingira ya kutatanisha kama ilivyotokea katika huo msiba.
Amesema kuwa wakati wananchi hao wakipanga mikakati hiyo taarifa zilifika kituo kidogo cha polisi Wampembe ambapo polisi wa kituo hicho waliweza kuchukua hatua ya kumuokoa Mzee huyo lakini kabla hawajafika msibani tayari Mzee huyo alikuwa ameshaanza kushambuliwa na wananchi na kuokolewa na polisi na mgambo na kasha kuchukuliwa na kwenda kuhifadhiwa kituo cha polisi kwa usalama wake.
Amesema wakati wananchi hai wakielekea kuzika walichukua jeneza la marehemu na kwenda nalo hadi kituo cha polisi ambapo waliliweka jeneza hilo hapo kituoni na kudai wanataka Mzee Daudi Kapelo atolewe humo ndani wammalize naye akazikwe na mwanae na kuanza kushambulia kituo hicho kwa mawe hali iliyopelekea askari kupiga risasi hewani lakini wananchi hao hawakuweza kuogopa na kuanza kumshambulia askari huyo na kuibua mapigano baina ya askari na wananchi wapatao 300.
Amesema kuwa wananchi hao baada ya kutawanyika walikimbia wote wakiwa tayari wameshawasha moto kituo cha polisi kikiungua ambapo askari polisi na mgambo kwa kusaidiana na viongozi wa kijiji walifanikiwa kuuzima moto huo na wananchi hao waliweza kurudi usiku wakachukua maiti ya merehemu na kwenda kuzika usiku huo huo.
Amesema mapambano hayo yaliendelea ambapo mwananchi mmoja Imelda Kayanda (46) alipigwa risasi na kufariki na Agnes Kisori(21) alijeruhiwa mguuni huku vitu vilivyoharibiwa vikiwa ni pamoja na solar panel ya kituo, vioo vya kituo vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya shilingi laki tano.
Amesema majeruhi walipelekwa kituo cha afya Wampembe na baadae hospitali ya wilaya ya Nkasi kupata matibabu ambapo hali zao zimeelezewa kuwa zinaendelea vema.
Amesema tayari jeshi la polisi limewakamata ndugu Zakaria Francis (28), Ikombe Yustini (39), Stephano Kambe (18), Benard Kabeja (16) na John Kapandila (22).
Wengine waliokamatwa amewataja kuwa ni ndugu Said Diwali (36), Vido Tuwakazi (21), Abdalah Vicent (19), Sylveter Kapala (17), Richad Bushota (19), John Mathias (58), Wilbroad Chambi (16) na Kapondo Anatoli (23) na wengine wane wote wakazi wa kijiji cha Wampembe wilaya ya Nkasi.
Kamanda wa Polisi amesema wakati watuhumiwa hao wote watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika na kuwa wengine waliokimbia watafuatiliwa hadi wakamatwe ili sheria ichukue mkondo wake.
Aidha kamanda Mantage ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na tabia mbaya ya kuvamia vituo vya polisi nchini hapa nchini kuwa vinalipeleka taifa kusikojulikana kutokana na ukweli kuwa hizo ni dalili za kuondoa misingi ya amani na utulivu katika jamii.
MWISHO
MBUNGE mmoja wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Mpanda amelalamikiwa kuwafanyia kitu mbaya vijana watatu akiwemo mlemavu asiyekuwa na uwezo wa kutembea.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa mbunge huyo mwenye sifa ya kuitwa Mbuyu mdogo amewadhulumu vijana watatu waliokuwa watumishi wa ofisi yake ya bunge katika jimbo lake ofisi zilizoko mjini Mpanda baada ya kuwatumikisha bila kuwalipa mishahara yao halali.
Wakiongea kwa uchungu vijana hao pamoja na binti mmoja mlemavu wa miguu aisyeweza kutembea kwa miguu ya kawaida walidai kuwa mbunge huyo amewadhulumu zaidi ya shilingi miliono moja na laki nane zikiwa ni mishahara na posho za kazi zaidi ya shilingi milioni moja na laki mbili.
Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Peter Pulwila Panta aliyekuwa ameajiriwa kwa kazi ya udereva na kupewa kitambulisho chenye nambari 001 alisema wamekuwa wakimdai mbunge huyo mishahara yao lakini cha kusikitisha amekuwa akidai kuwa hizo pesa hajaletewa kutoka ofisi ya bunge kitu ambacho si kweli kutokana na maelezo yaliyoko katika barua yenye kumb namba FA.155/2006/01/70.
Alisema licha ya kuwa barua inaagiza kuwalipa mshahara wa kiasi cha shilingi 150,000 kwa mwezi lakini yeye aliwaeleza kuwa watakuwa wanalipwa shilingi laki moja kila mwezi na kuwa alikuwa anakidai kuwa anawalipa kutokana na mshahara wake wa ubunge ihali barua inaonesha kuwa fedha hizo zinatumwa kila mwezi katika akaunti ya mbunge huyo kwa ajili ya mishahara na posho.
Naye binti mwenye ulemavu aliyekuwa akifanya kazi kama mhudumu wa ofisi ya mbunge huyo alisema kuwa tangu mwaka 2005 alikuwa akifanya kazi na kupewa hela ya soda tu shilingi 20,000/= tu kila anapodai mshara wake na kuwa ukosefu wa mshahara kumepelekea mwanaye anayesoma katika shule ya sekondari Mwese kuzuia kuendelea masomo kutokana na madeni ya ada.
Alipofuatwa na mwandishi wa habari ofisini kwake kujua kulikoni anadaiwa na watumishi wake akiwemo mlemavu wa miguu lakini mbunge huyo hakuweza kupatikana badala yake alikuwepo mtu aliyejieleza kuwa ni katibu wa mbunge huyo ingawa alikataa ktaja jina lake aliyeeleza kuwa mbunge wake yuko katika kikao CCM
Juhudi za kumtafuta kwa simu mbunge huyo zilifanikiwa ambapo mbunge huyo alijibu katika simu kuwa anahitaji kuonana na mwandishi wa habari.
Cha kushangaza ni kuwa alikwenda mwandishi ofisini kwake kuzungumzia suala la madeni na kuzomewa alikozomewa wakati wa mkutano wa hadhara katika kijiji kimoja mbunge huyo alimsihi mwandishi huyo asiandike taarifa yoyote mbaya kumhusu na kumpatia kiasi cha shilingi elfu ishirini kwa ajili ya kumziba mdomo pesa ambazo mwandishi alizikataa na kuondoka
Uchunguzi umebaini kuwa madai hayo na mengine mengi yalishawahi kufikishwa katika ofisi za CCM wilaya ya Mpanda na kukosa suluhu ambapo mbunge huyo amekuwa akijinadi kuwa ni mtaalamu wa propaganda, mbuyu mdogo anataka kugombea mwakani kutetea kiti cha ubunge hivyo wasimjadili kuhusu madeni yake.
Mbunge huyo alijikuta akitemwa katika kura ya maoni ndani ya chama chake katika uchaguzi mkuu wa 2010 nchini Tanzania
MWISHO
MILIONI KUMI HIZI ZIMETUMIKA KWELI NAMNA HII
ZAIDI ya shilingi milini 10.1 zimetumika kwa ajili ya kuwanunulia sare za shule na kuwalipia ada na chakula watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu wilaya ya Mpanda mkoani Rukwa
Mratibu wa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya SHDEPHA + tawi la Mpanda Mwalimu Euzebius Ngulusha alisema hayo jana (Novemba 3, 2009) wakati wa hafla fupi ya kuwakabidhi sare, chakula na mahitaji ya shuleni watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi wapatao 54 iliyofanyika katika ukumbi wa SHDEPHA + mjini Mpanda.
Alisema katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu zaidi ya shilingi milini 10.1 zimetumika kuwahudumia watoto 204 wanaoishi katika mazingira hatarishi, yatima na watoto wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wilayani Mpanda fedha ambazo zimetoka kwa wafadhili mbalimbali ikiwa ni pamoja na shirika la Kimarekani la WALTER REED la nchini Marekani.
Alisema shirika lake limelipia ada za sekondari na kuwanunulia sare za shule watoto wanaosoma katika shule za sekondari wapatao 150 kwa gharama ya shilingi 8,304,300/= na watoto wanaosoma shule za Msingi wapatao 35 na wachache wanaotoka katika mazingira hatarishi.
Alisema kiasi cha shilingi 1,800,000 zimetumika kuwanunulia mahitaji ya shuleni kama vile daftari, kalamu, vihifadhio, mifuko ya shule na vifaa vya kuchorea vya wanafunzi hao ili nao wajisikie kama sehemu ya jamii.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mji wa Mpanda afisaelimu wa sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda Said Mwapongo aliwashukuru viongozi wa asasi hiyo ya SHDEPHA + kwa kufanya kazi ya kuwasaidia wanaohitaji katika jamii na kuvishinda vishawishi wanavyokumbana navyo vishawishi ambavyo amesema vinawapelekea kushikwa na tamaa ya kutumia fedha hizo bila kujali ni za nani.
Alisema moyo wa kuwafikishia walengwa ambao hawakujua kama wanaletewa nini ni moyo wa kipekee na wa kiungwana ambapo amewasihi kutokukata tamaa na kuwa Mungu peke yake ndiye atakayewalipa kwa kazi njema hiyo.
Mwapongo aliwasihi wanafunzi hao kuitumia misaada waliyoipata na wanayoendelea kuipata kwa kusoma kwa bidii, kuwa na heshima katika jamii ili kuwawezesha kufikia malengo yao ambayo ni kuwaondoa katika lindi la maisha ya masikitiko na umasikini uliopindukia.
MWISHO
WANANCHI HAWA WAMECHUKIA DILI ZA POLISI AU NI HASIRA KWELI?
WANANCHI wenye hasira wamefanikiwa kuliua jambazi lililokuwa likitafutwa na jeshi la polisi mkoani Rukwa baada ya kumkuta akiiba magunia ya mpunga
Akiyeuwawa ametajwa kwa jina la Revocatus Benedicto Katunga mwenye umri wa miaka 33 mkazi wa Nsemulwa mjini mpanda ambaye aliuwawa na wananchi Septemba 23,2009 saa kumi na mbili asubuhi mara baada ya kukutwa akiiba magunia ya mpunga katika mashine ya kusaga ya mfanyabiashara anayejulikana kwa jina la Kasimu lyanga maarufu kwa jina la Usayi.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa Isuto Mantage aliwaeleza waandishi wa habari kuwa siku ya tukio marehemu anayesadikiwa kuwa ni jambazi sugu aliyekuwa anatafutwa na jeshi hilo alikutwa na wananchi akiwa katika harakati za kuiba magunia ya mpunga ambapo alikuwa ameshaiba magunia manne ya kuyatoa nje ya jingo hilo .
Alisema baada ya kumkuta marehemu huyo wananchi hao walianza kumhoji lakini akawa anawajibu maneno ya jeuri kwa sauti kubwa iliyowaamusha majirani wengine waliofika hapo na kumkuta jambazi huyo aliyekuwa akitafutwa na jeshi la polisi mkoani Rukwa kwa tuhuma za kushiriki katika matukio kadhaa ya uhalifu walianza kumpa kipigo hadi akapoteza fahamu ndipo wakawaita polisi kituo cha Mpanda.
Alisema kamanda Mantage kuwa polisi walipofika eneo la tukio walimchukua marehemu na kumwahisha hospitali ambako kabla ya kupewa huduma yoyote alifariki akiwa eneo la hospitali.
Kamanda alisema hakuna aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo ambapo alieleza kuwa marehemu alikuwa akitafutwa kwa kosa la kuvunja na kuiba vitabu katika shule ya msingi Katavi iliyoko mjini Mpanda na pia alikuwa na kesi mahakani ya kuiba kwa kutumia silaha
Kwa upande wao wananchi wa eneo la Mpanda Hoteli mjini Mpanda walionesha kusikitishwa kwao na mwenendo wa utendaji kazi wa jeshi la polisi wilayani Mpanda kwani jambazi huyo alikuwa ameshikana kukamatwa na jeshi hilo hadi walipomkamata wananchi wenyewe na kumpa hukumu ya kifo licha ya kuwa alikuwa na matukio mengi ya kutafutwa.
the end