KATIKA hali isiyo ya kawaida baadhi ya wananchi katika mkoa
wa Katavi wamefurahia kitendo cha kuuwawa majangili walikiwa na vipande 73 vya meno
ya tembo katika gari waliliokuwa wakisafiria
katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma juzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Mpanda katika mkoa wa Katavi wananchi hao walisema
kuwa wamepokea kwa furaha kubwa tukio la kuuwawa majangili hao waliokuwa
wakitokea Mpanda baada ya kufanya mbinu zilizopelekea kufutwa kwa kesi
iliyokuwa ikiwakabili ya uhujumu uchumi katika mahakama ya wilaya ya Mpanda.
Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Keni alisema
kuwa watu hao walikuwa na tabia mbaya sana hapa Mpanda kwani walikuwa wanaishi
kwa biashara ya meno ya tembo wanaopatikana katika hifadhi ya wanyama ya Katavi
na Mlele na kila walipowekewa mtego walikuwa wanaukwepa na hata waliponasa
wakafikishwa mahakamani waliweza kufutiwa kesi zao kwa jinsi walivyojipanga.
Alisema walipokamatwa Nsimbo mwaka jana walikuwa na meno
mengi zaidi isipokuwa waliweza kuficha wakati wa purukushani na polisi ingawa
polisi walifanikiwa kukamata meno matatu tu licha ya kuwa yalikuwa mengi zaidi
kuliko idadi iliyokamatwa.
Alisema wakiwa mjini Mpanda majangili hao walikuwa
wanaongozwa na mwenyeji wao aliyetajwa na Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma kuwa
anatoka Kawajense mjini Mpanda ndugu Peter Mtipula ambaye ameelezewa kuwa jina
lake halisi ni Peter Matiapula na siyo Mtipula.
Keni ambaye anaishi jirani na marehemu Peter Matiapula
alisema kuwa mara kwa mara walikaa vikao vya kumuonya Peter aachane na biashara
hiyo lakini aliwajibu kuwa wasimfuate fuate maisha yao kwani kila mtu anajua
maisha anayoishi mwenyewe huku akithibitisha kuwa ipo siku atakuwa tajiri
mkubwa na kuwapa vibarua vya kufanya
Bi Elizabeth alimaarufu Mama Kulwa alisema kuwa aliposikia
jina la Peter Mtipula alihisi ni jirani yake lakini aliposikia ni mkazi wa
Kawajense akajiridhisha kuwa ni yeye mwenyewe kwani ametoweka kwa siku kadhaa
mtaani kwao
Alisema tabia ya jirani yao iliwafanya wawe na maisha ya
mashaka kwani wakati wowote mtu mwenye tabia kama hizo siku ikitokea ameishiwa
anaweza kuwaingilia hata majirani ili apate pesa za harakaharaka na hata wakati
mwingine misako ya askari wa wanyama pori na polisi inayopitishwa mtaani
kutokana na taarifa za kuwepo kwa jangili mtaani hapo
Katika gazeti moja la Kiswahili la kila siku siyo hili
iliandikwa habari kuwa wananchi wenye hasira waliweza kuwakamata na kuwaua watu
wane waliokuwa wakidhaniwa kuwa ni majangili yaliyokuwa na vipande 73 vya meno
ya tembo katika maeneo ya Mwitikila katika wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma
baada ya kuweka mtego wa polisi
Katika tukio hilo kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Kamishina
Msaidizi wa Polisi (ACP), David Misime aliwataja waliouwawa kuwa ni Joseph
Marius (59) mkazi wa Maili Mbili Manispaa ya Dodoma, Abubakari Mhina (25) na Msafiri Milawa (36) wote wakazi wa Nkuhungu
manispaa ya Dodoma na Peter Mtipula (Matiapula) (55) mkazi wa Kawajense mjini
Mpanda mkoa wa Katavi.
Alisema watu hao walikuwa wakitumia gari aina ya NOAH yenye
namba za usajiri T983BZJ ambalo baada ya kupekuliwa polisi wakuta vipande 73
vya meno ya tembo pamoja na hati ya mashitaka ya mahakama ya wilaya Mpanda ya
marehemu hao walipokuwa wameshitakiwa mahakani hapo baada ya kukamatwa Nsimbo
na gari hilo wakiwa na meno matatu ya Tembo ikionesha kesi hiyo ilifutwa
mahakani hapo Januari 30 mwaka huu.