Thursday, February 28, 2013

KATAVI FEBRUARI


Matumizi ya vyandarua yanazidi kupanuka, hapa vijana wamekutwa na kamera yetu wakiwa wamefunga vyandarua katika magori kama nyavu za magori ya mpira wa miguu katika eneo la Uwanja wa ndege mjini Mpanda mtaa wa Kashaulili.





Uwanja wa ndege wa Mpanda


Mmiliki wa blog hii akiwa uwanja wa ndege wa Mpanda hivi karibuni







Na Willy Sumia, Mpanda
MKE wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete amewataka Watanzania kudumisha umoja, mshikamano na upendo baina yao ili kupata fursa ya kufanya kazi zitakazowaletea maendeleo ya haraka
Mama Salma Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa taasisi ya WAMA alisema hayo Februari 27, 2013 alipokuwa akisalimiana na wananchi waliojitokeza uwanja wa ndege wa Mpanda mkoa wa Katavi kumlaki alipokuwa akibadilisha usafiri wa ndege alipokuwa akitoka Sumbawanga kuelekea DSM
Kutokana na kilichoonekana ni kuvutiwa na umati wa wananchi waliofurika uwanjani hapo alipokuwa akiwasili kutoka Sumbawanga Mama Salma Kikwete alilazimika kuzungumza walau kwa dakika kumi mara baada ya mkuu wa wilaya ya Mpanda Paza Mwamlima kumueleza kuwa wananchi hao walipopata taarifa kuwa atapita katika uwanja wao waliamua kufika uwanjani ili walau wasalimiane naye.
Kabla ya kuzungumza chochote mke wa Rais Kikwete, Mama Salma Kikwete alionekana kuguswa na umati wa watu uliojitokeza ndipo alipoanza kwa kusema anawapenda sana wananchi hao
“Katavi Oyeee!!! Nawapenda sana ndugu zangu, mmekuja huku uwanjani kunipokea kwa furaha namna hii, asanteni sana.” Alisema mama Kikwete
Alisema kuwa licha ya kutambua kuwa wananchi wa mkoa wa Katavi ni wakulima hodari anawakumbusha kuendelea kulima kwa kufuata kanuni na maelekezo ya kitaalamu ili kuzalisha chakula cha kutosha na ziada ya kuuza ili kujipatia pesa za kufanyia mambo mengine ya maendeleo
Alisema pamoja na kuwa hivi sasa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi unaendelea vizuri lakini anawasihi wananchi wa Tanzania kuendelea kushikamana, kupendana na kudumisha umoja baina ya jamii nzima ili kuepuka vurugu na kupata muda wa kufanya kazi za maendeleo
“Nawasihi ndugu wananchi kuendelea kushikamana kwa umoja wetu, kupendana na kuhakikisha tunashirikiana katika nchi yetu ili tuweze kuepuka vurugu na pia itatusaidia kuwa badala ya kuvutana tuwe na muda wa kufanya kazi na hivyo amani ya nchi yetu itaendelea” alisema
Aliwataka watoto kusoma kwa bidii mashuleni pamoja na kuwaasa akinamama kuchukua jukumu la kuwaangalia watoto wanapokwenda shuleni na wanapotoka shuleni.
mwisho











Mkuu wa wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima akihutubia wakazi wa kata ya Nsemulwa mjini Mpanda Februari 27, 2013 alipokuwa akizindua maadhimisho ya mazingira ya afya Afrika kimkoa katika mkoa wa Katavi


MSIGOMBANIE KUCHINJA WATANZANIA ... DC


MIGOGORO ya kidini inayoibuka hivi sasa nchini inasababishwa na mataifa maadui wa Tanzania wanaotaka kupandikiza vita na mapigano ili yaweze kufanya biashara ya madini na silaha wakati wa vita hivyo.

Hayo yalibainishwa na mkuu wa wilaya ya Mpanda, Paza Tusamale Mwamlima Februari 27, 2013 katika mkutano wa hadhara wakati wa hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya mazingira ya afya Afrika katika kata ya Nsemulwa mjini Mpanda katika mkoa wa Katavi.

Mkuu huyo wa wilaya aliposimama ili kuzindua maadhimisho hayo alisema kabla ya kuanza shughuli yoyote uwanjani hapo kwanza aseme mambo ya msingi sana kwa mustakabali wa Watanzania na Tanzania yenyewe kuhusu hali ya vurugu iliyoanza kuibuka karibu siku hadi siku.

“Ndugu zangu kuna mataifa ya nje yanayotamani madini ya Tanzania, pia kuna mataifa yanatafuta kwa kuuzia silaha zao, ili wafanikishe malengo yao hayo wamekuwa wakiwarubuni Watanzania kuhusu mambo ya imani ambapo wapo wanaowapa maelekezo na wakati mwingi ufadhiri baadhi ya Wakristo kuwa Muisilamu akichinja hakuna kula nyama hiyo, na watu hao bila kutafakari wanayabeba kama yalivyo na kuyafanyia kazi eti hakuna Muisilamu kuchinja nyama ya kula wakristo.” Alisema mkuu wa wilaya

Alisema hivi sasa Tanzania imefikia umri wa miaka hamsini tangu kupata Uhuru na waislamu wamekuwa wakichinja kitoweo na wala hakuna aliyewahi kudhurika awe ni Muisalamu au Mkristo sasa iweje leo sisi kizazi cha leo ndo tuanze kuvitana sana kuliko hata waliopigania uhuru wa nchi hii kuona kuwa lazima na wakristo nao wachinje nyama zao, ni upotofu mkubwa na wala hakuna mantiki ya kulisimamia hilo bali ni kuharibu umoja na mshikamano wa Taifa

Aliwasihi Wakristo kupuuza misimamo ya uchinjaji kuwa ni kutetea imani ya ukristo kwani hakuna matokeo mazuri kuendelea na marumbano ya nani achinje na nani asichinje bali wakristo wanapotaka kuchinja wawape Waislamu wawachinjie tu kwani kitoweo ni kile kile na zaidi sana kitadumisha umoja baina ya wananchi bila kujali utofauti wa kiimani kwani wananchi watapata fursa ya kuendelea kushirikiana katika misiba, sherehe na hata katika chakula.

Alisema licha ya kuwa wananchi watasimama kutetea imani zao kwa misingi ya uchinjaji lakini bado hakutakuwa na suluhisho litakaloiweka Tanzania pamoja kama ilivyokuwa miaka hamsini iliyopita na hivyo kuwaomba Watanzania wote kuanza ukurasa wa kusameheana, kuvumiliana, kuheshimiana, kujaliana na kujiona wote ni wamoja katika msingi wa Utanzania wao. 

Alisema katika mikoa yote hapa Tanzania, kanda za mahubiri ya kidini yanayokashifu imani za dini zingine zimepigwa marufuku hata kama ni nyumbani kwako ambapo alisema kumetolewa maelekezo kuwa yeyote mwenye kanda za mahubiri yanayokashifu imani ya dini nyingine afungulie kwa sauti inayomtosheleza yeye mwenyewe ndani asiruhusu sauti kutoka nje kiasi cha kuwasikilizisha majirani kinachohubiriwa.

“kutokana na kuibuka kwa mahubiri ya kukashifiana baina ya dini moja na nyinge serikali imeagiza kuwa hakuna ruhusa kwa mtu yeyote awe mtu binafsi nyumbani kwake, dukani, kwenye maduka ya kanda au mahala popote kufungulia kanda hizo kwa sauti ya kuwasikilizisha na majirani, kufanya hivyo ni kosa na utachukuliwa hatua” alisema Mwamlima

Mkuu wa wilaya ya Mpanda alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Katavi, Dr Rajabu Rutengwe ambaye alikuwasafarini kama mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya mazingira ya afya Afrika yaliyofanyika kimkoa katika kata ya Nsemulwa mjini Mpanda ambayo kilele chake yatafanyikia katika kijiji cha Majalila wilaya ya Mpanda.










TUNAANDIKA MAAGIZO YA MKUU.