Thursday, June 6, 2013

SERIKALI YAJUTIA UHARIBIFU WA MAZINGIRA



NAMANYERE



KATIKA hali isiyo ya kawaida Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Mohammed Ghalib Bilal ameelezea kujutia namna uharibifu wa mazingira ulivyo hivi sasa nchini
Dr Bilal alionesha kujutia kwake na hali ilivyo sasa ya uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo mbali mbali nchini na kuelezea madhara yanayojitokeza kutokana na uharibifu huo kwa Watanzania nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha vifo
Akihutubiwa Watanzania katika kilele cha siku ya mazingira duniani katika uwanja wa sabasaba katika mji wa Namanyere wilaya ya Nkasi mkoa wa Rukwa Makamu wa Rais alisema ni ukweli ulio wazi kwamba pamoja na umuhimu wa mazingira bado tunaendelea kufanya uharibifu wa mazingira
“Ni ukweli ulio wazi kwamba, pamoja na umuhimu wa mazingira bado, tunaendelea kufanya uharibifu wa mazingira na hivi sasa tumeshaona na kujutia athari za uharibifu wa mazingira tulioufanya” alisema Dkt bilal
Aidha alifafanya kuwa baadhi ya athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira duniani ni pamoja na kupungua kwa mvua, majira kubadilika na kuongezeka kwa vipindi vya ukame, kupungua kwa kasi ya theluji katika ncha ya kaskazini nay a kusini na kwenye vilele vya milima kote dunia ambapo hata mlima Kilimanjaro nao unaathirika pia
Athari zingine alizitaja kuwa ni kupungua kwa kina cha maji katika maziwa mbali mbali na katika nchi yetu maziwa yanayoathirika ni Ziwa Tanganyika, Victoria na Ziwa Rukwa, kuongezeka kwa kina cha bahari na kuathiri maeneo ya nchi kavu ambapo maeneo mengi yamezama na mengine yako hatarini kuzama ambapo hapa Tanzania kisiwa cha Maziwe katika Bahari ya Hindi kimezama ambapo pia visima vya  maji katika ukanda wa Pwani vimeanza kuwa na maji chumvi
Alisema madhara mengine aliyataja kuwa ni kuenea kwa magonjwa kama malaria kwenye maeneo ambayo hayakuwa na mbu lakini siku hizi mbu wapo huko kutokana na ongezeko la joto kwa mfano maeneo yenye miinuko na baridi hususani Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini hapa nchini
Madhara mengine alisema ni kupungua kwa kiwango cha maji duniani kwenye chemic hemi, mito, vijito, maziwa na mabwawa kukauka, kuendelea kupungua kwa kasi kwa misitu na jangwa kuzidi kuongezeka kwenye maeneo ambayo hayakuwa na jangwa hapo awali pamoja na kuathirika kwa ubora wa ardhi na kupunguza malisho ya mifugo na wanyama wengine ambapo pia imebainika kuwa maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na viwandani yamepungua sana.
Kufuatia hali hiyo Makamu wa Rais alisisitiza kuwa hali siyo nzuri hata kidogo hivyo inabidi hatua za makusudi zichukuliwe kukabiliana na tatizo lililopo
“kwa ujumla hali siyo nzuri hata kidogo na kwamba hatuna budi kuchukua hatua za dhati za kurekebisha hali hii, lazima tuchukue hatua za makusudi kupunguza kasi na kurekebisha uharibifu wa mazingira na tuendelee na juhudi za kuejnga upya tulipoharibi na kulinda palipo salama” alisema Dr Bilal
Alifafanua kuwa  mwakani kutakuwa na tuzo ya Rais ya Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Kupanda miti na Kutunza itakayotolewa mwaka ujao wa 2014 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na kuzitaka tasisi, kaya, shule, makampuni, vyuo, wilaya, mikoa, mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali kushiriki.
Awali Naibu Waziri, wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Seif Selemani Rashid alitangaza halmashauri zilizoshinda shindano la usafi wa mazingira lililoendeshwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii 2013 ambapo katika halmashauri za Majiji jiji la Nyamagana Mwanza ambalo lilipewa kombe, cheti maalumu na pikipiki
Katika kundi la halmashauri za Manispaa Dk Seif aliitangaza manispaa ya Moshi kuwa ya kwanza kwa kushinda shindano hilo la usafi wa Mazingira nchini na kukabidhiwa Kombe, cheti maalumu na Pikipiki aina ya Yamaha cc125 ambapo manispaa ya Iringa walipata ushindi wa pili na kukabidhiwa cheti maalumu na pikipiki aina ya Yamaha cc 110 na Manispaa ya tau ilitangazwa kuwa ni Manispaa ya Morogoro ambayo ilipewa cheti maalumu cha ushindi na pikipiki aina ya Yamaha 110
Naibu Waziri wa Afya Dkt Seif aliitangaza Halmashauri ya Mji wa Mpanda kuwa bingwa wa mashindano ya usafi wa Mazingira yaliyoendeshwa na wizara yake ambapo halmashauri hiyo ilikabidhiwa na Makamu wa Rais Cheti maalum, Kombe na Pikipiki aina ya Yamaha cc 125, mshindi wa pili ni halmashauri ya mji wa Njombe ambayo ilipewa cheti maalum na pikipiki aina ya Yamaha 110
Katika halmashauri za wilaya Dkt Seif aliitanga Halmashauri ya wilaya ya Njombe kuwa mshindi wa kwanza wa mashindano hayo ambayo ilikabidhiwa cheti maalumu, kombe na pikipiki aina ya Yamaha cc 125 na ya pili kuwa ni halmashauri ya wilaya ya Rungwe iliyokabidhiwa cheti maalum na pikipiki aina ya Yamaha cc 110 na ya tatu ilitangazwa halmashauri ya wilaya ya Meru ambayo ilikabidhiwa cheti maalumu na pikipiki aina ya Yamaha cc110
Aidha Dkt Seif alifafanua kuwa mwaka huu wizara yake iliendesha mashindano ya kampeni ya vyoo bora na usafi wa mazingira kwa halmashauri ambapo halmashauri ya wilaya ya Kondoa ilifanya vizuri ambayo ilikabidhiwa cheti na pikipiki aina ya Yamaha cc 125
Alisema vitongoji nchini vilishindanishwa katika matumizi bora ya vyoo bora ambapo kitongoji cha Mserakati kata ya Kwamtoro halmashauri ya wilaya ya Kondoa iliweza kushinda ambapo ilikabidhiwa Baiskeli tatu aina ya Phoenix, cha pili ni kitotongoji cha Ndemanilwa, kata ya Kibaoni wilaya ya Mlele ambacho kilikabidhiwa baiskeli mbili aina ya Phoenix na kitongoji cha tatu ni cha Kasanda kilichopo katika kata ya Busagara halmashauri ya wilaya ya Kibondo ambacho kilikabidhiwa zawadi ya baiskeli mbili aina ya Phoenix
mwisho