UHABA wa dawa za binadamu katika vituo vya afya na zahanati umeanza
kuchukua sura mpya baada ya baadhi ya wananchi kuiomba Serikali kuangalia upya mfumo wa
usambazaji dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini ili kunusuru
maisha ya wananchi
Wito huo ulitolewa jana na baadhi
ya wakazi wa vijiji vya Mamba na Majimoto wilaya ya Mlele mkoani Katavi
walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo
kufuatilia mpango wa huduma za chanjo kwa watoto na akinamama katika maeneo
yaliyoko mpakani mwa nchi ya Tanzania na DRC
Wananchi hao walisema licha ya
kuwa vituo vingi vya afya na zahanati vimejengwa na kuanza kutoa huduma kwa
karibu na wananchi lakini bado changamoto ya upatikanaji wa dawa za binadamu
katika vituo hivyo hairidhishi kutokana na vituo hivyo kukosa huduma hiyo kwa
muda mrefu
Walisema awali wakuwa
wakiwatuhumu baadhi ya watoa huduma katika vituo hivyo kuwa wanauza dawa hizo
lakini baadae waliweza kubaini kuwa hata wao watoa huduma wananunua dawa kutoka
maduka ya dawa pindi wanapougua kutokana na MSD kutokufikisha dawa hizo kwa
wakati katika zahanati na vituo vya afya
Walisema mtindo wa kupeleka dawa
katika vituo vya afya na zahanati kwa kipindi cha miezi mitatu ni tatizo linaloweza
kuleta dhahama katika jamii hasa ya vijijini kwani uwezekano wa dawa kukaa kwa
kipindi hicho hasa maeneo ya vijijini ni mdogo sana kutokana na mahitaji na
miundombinu ya kuhifadhia dawa kuwa bado ni duni.
Walisema mganga wa zahanati
hawezi kuzuia dawa zisitumike katika kipindi cha miezi mitatu kama wagonjwa
wapo na wanahitaji dawa hizo kwani jukumu lake ni kutibu wananchi wapate kupona
na siyo kuhifadhi dawa hadi zifikie miezi mitatu
“Huwezi kubana matumizi ya dawa
vijijini kwenye wagonjwa wengina maduka ya dawa hakuna, hapo tunadanganyana
maana hata iweje hizo dawa wanazoleta za miezi mitatu hazitoshi hata mwezi
mmoja kutokana na mahitaji kuwa makubwa” alisema Martini Pesambili mkazi wa Majimoto
Mganga mkuu msaidizi wa kituo cha
afya Matai wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Bonifasi Wambanga alisema kuwa hata wanapoagiza dawa MSD kulingana
na mahitaji dawa zinazopelekwa haziendani na mahitaji waliyopeleka na badala
yake zinapelekwa dawa zingine zisizohitajika kulingana na jiografia ya eneo
husika kutokana na kuchukua muda mrefu tangu kuagizwa dawa na kufika
Alisema kuna dawa zinahitajika
majira ya kiangazi kulingana na hali ya hewa na kipindi hicho lakini zinafika
masika ambako kuna mahitaji tofauti na dawa zinazofika kipindi hicho kutokana
na hali ya hewa ya masika