Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dr Rajabu Rutengwe akizungumza na wanahabari ofisini kwake, kushoto kwake ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emanuely Kalobelo |
MKOA wa Katavi unajiandaa kuanza kutoa zawadi kwa walimu
watakaowezesha shule zao kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya Taifa ili
kuinua kiwango cha taaluma katika shule za Sekondari na Msingi mkoani humo.
Hayo yalibainishwa na Katibu Tawala wa mkoa huo,
Mhandisi Emanueli Kalobelo alipokuwa akizindua semina ya wahojaji kutoka wilaya
za mkoa huo watakaoendesha utafiti wa kiwango cha uelewa wa stadi za kusoma na
kuhesabu katika jamii iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la UWEZO
TANZANIA.
Alisema hali ya taaluma katika shule za Msingi na
Sekondari katika mkoa wa Katavi siyo nzuri na hivyo kulazimisha uongozi wa mkoa
kuanza mikakati imara ya kuanza kukabiliana na hali hiyo ili kukiokoa kizazi
cha leo na kijacho katika mkoa huo.
Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kutoa
zawadi kwa walimu watakaowezesha shule zao kufanya vema katika mitihani ya
Taifa ya sekondari na Msingi pamoja na kuwapa mafunzo ya mara kwa mara walimu
waliopo kazini kwa lengo la kuwapa ujuzi wa kutosha walimu hao.
Alisema Mkoa wa Katavi
unajumla ya wanafunzi 5,855 wasiojua kusoma wala kuhesabu wanaosoma darasa
la pili katika shule za Msingi licha ya kuwa wamekuwa wakihudhuria masomo
darasani
Alifafanua kuwa lengo
la Mkoa wa Katavi ni kuhakikisha kwamba
wanafunzi wanajua kusoma na kuandika
wakiwa Darasa la pili kabla ya kuingia darasa la tatu ili waweze kuanza
kupokea maarifa mapya kutoka kwa walimu na kwenye vitabu.
Aidha Katibu tawala wa mkoa alisema mkoa wa Katavi umelenga kuboresha taaluma ili kuinua kiwango cha
ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi
kufikia asilimia sitini mwaka huu
ukilinganisha na asilimia 26 za ufaulu wa mwaka jana katika matokeo ya
darasa la saba.
Akizungumzia kiwango cha ufaulu kwa shule za Sekondari mkoani
mwake Kalobelo alisema wamepanga kuinua kiwango cha ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne kufikia asilimia sitini mwaka 2013 kutoka asilimia
arobaini na mbili za mwaka jana na
asilimia sabini mwaka 2014 ili mwaka
2015 ufaulu uweze kufikia asilimia themanini
Alisema Mkoa umeanzisha
utaratibu wa kuzipanga shule kuwa katika
madaraja katika matokeo na kutangaza matokeo ya mitihani ya kila shule kwenye
vyombo vya habari na mbao za
matangazo sambamba na kutoa tuzo kwa shule bora zinazofanya vizuri kwa mwaka
huo katika mitihani ya Taifa