Wednesday, October 9, 2013

MANISPAA YAMKABA KOO MKANDARASI SUMBAWANGA









MANISPAA ya Sumbawanga mkoani Rukwa imemuagiza mkandarasi wa barabara anayefanya matengenezo ya muda katika barabara za mjini humo kurudia kazi hiyo kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yake

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na ofisi ya Mhandisi wa Manispaa ya Sumbawanga na kuthibitishwa na mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini, mkandarasi anayefanya matengenezo ya barabara sita ndani ya Manispaa hiyo kusimamisha kazi hiyo mara moja na badala yake kurudia tena kazi yake kutokana na mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi uliofanyika Septemba 5, 2013

Katika barua hiyo iliyosainiwa na mkaguzi wa Barabara wa Manispaa hiyo, Kashinde Malilo imeelezwa kuwa katika ukaguzi huo ilibainika kuwa kifusi kinachotumika katika barabara hizo hakifai kutokana na kuwa na vumbi jingi tofauti na maelekezo yaliyoko katika mkataba

Barua hiyo iliyoandikwa kwenda kwa kampuni ya NOVIDS LTD ya jijini Mwanza ambayo imepewa zabuni ya kufanya matengenezo hayo imezitaja barabara zinazotakiwa kurudiwa na kampuni hiyo kuwa ni barabara ya Mtaa wa Jangwani, Mtaa wa Majengo, Posta hadi NMC,  Kasulu hadi Kanisa la Neema, Msakila hadi Kasulu na Mtaa wa Katusa.

Akizungumza na wanahabari katika ofisi za CCM mkoa wa Rukwa, mbunge wa jimbo la Sumbawanga mjini, Mhe. Aeshi hilal alisema kuwa katika kikao walichofanya hivi karibuni katika ofisi za Manispaa walikubaliana kusimamia kwa karibu suala la uchakachuaji wa makandarasi mbali mbali katika manispaa hiyo ili kuzuia makosa yaliyofanywa na uongozi uliopita yasirudiwe tena

Aliyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ujenzi chini ya kiwango wa stendi ya basi Sokomatola, ujenzi wa barabara ya lami mjini sumbawanga, ujenzi wa jingo la shule ya sekondari ya Mazwi na mitaro katika baadhi ya barabara mjini Sumbawanga

Katika hatua ya kushangaza  mmiliki wa kampuni ya NOVIDS LTD ya Mwanza ambayo ndiyo iliyosimamishwa isiendelee na kazi mjini Sumbawanga, Leonard Lukasi alikataa kupokea barua hiyo na kudai kuwa huenda amekabidhiwa mwakilishi wake aliyemtaja kwa jina moja la Willy ambaye hakuweza kupatikana kuzungumzia sakata hilo.
mwisho