Na Willy Sumia, Mpanda
MWENYEKITI mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilaya ya Mpanda mkoa wa Rukwa amekihama chama chake baada ya kunyimwa fursa ya kuwa mgombea wa Udiwani katika kata mpya ya Makanyagio mjini Mpanda katika mkoa wa Katavi.
Mwenyekiti huyo Bwana Juma Mausi alihama chama chake mara baada ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu wa 2010 kuanza kupamba moto kufuatia kuanza kwa mikutano ya kampeni na kujikuta akitupwa nje ya timu ya wagombea wa CHADEMA katika kinyang’anyiro cha udiwani kata ya Makanyagio baada ya nafasi hiyo kupewa mjumbe wa serikali ya mtaa wa Kachoma ndugu Nziguye Juma.
Juma Mausi ambaye ndiye aliyeipokea na kuasisi chama cha CHADEMA wilaya ya Mpanda wakati wa vuguvugu la vyama vingi nchini alijikuta akikihama chama chake baada ya kubaini kile alichokieleza yeye
mwenyewe kuwa CHADEMA imekamatwa na wageni na kukiita kitendo hicho kuwa ni Uvamizi wa kisiasa ndani ya CHADEMA yake.
Taarifa sahihi toka katika chanzo cha kuaminika ndani ya CHADEMA zimeeleza kuwa baada ya kuona haridhishwi na uamuzi aliofanyiwa ndani ya CHADEMA Mzee Mausi aliamua kujiunga na chama cha NCCR Mageuzi ambako alipewa nafasi ya kuwa mgombea wa chama hicho katika king’anyiro cha udiwani kata ya Makanyagio ili kupambana na wagombea wa CCM, CHADEMA na CUF.
Juma Mausi alikuwa mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mpanda hadi Agosti alipotangaza kuachana na chama hicho na kuhamia NCCR Mageuzi hali iliyopelekea CHADEMA wilaya ya Mpanda kutafuta mwenyekiti wa muda katika kipindi hiki cha uchaguzi ambapo chama hicho kinatetea nafasi ya ubunge jimbo la Mpanda mjini ambapo mbunge wa sasa wa jimbo hilo ni mheshimiwa Said Arfi wa CHADEMA.
mwisho
No comments:
Post a Comment