Iringa
WADAU wa asasi zisizo za kiserikali nchini wametoa onyo kwa wafugaji na wakulima wanaotumia dawa za binadamu kuwapa mifugo na kupulizia kwenye mazao na kusababisha ongezeko la madhara makubwa kwa jamii.
Hayo yalizungumzwa na washiriki wa mafunzo ya uchambuzi wa Sera yaliyoandaliwa na Mwamvuli wa asasi za kiraia mkaoni Iringa na Njombe Iringa Civil Society Organizations (ICISO) katika ukumbi wa Lutherani
mjini Makambako katika mkoa mpya wa Njombe wiki iliyopita.
Wadau hao walisema kuwa tabia iliyoibuka hivi karibuni kwa baadhi ya wafugaji na wakulima kutumia dawa zitumikazo kwa ajili ya binadamu kwa kuipa Mifugo hali inayopelekea kuibuka kwa magonjwa yasiyofahamika na kusababisha madhara kwa walaji wa bidhaa zitokanazo na mifugo.
Bwana Obothe Msemakweli mmoja wa wadau kutoka asasi ya LUCAPOA ya wilayani Ludewa alisema baadhi ya wakulima wa zao la nyanya wamekuwa wakipulizia dawa ya kuua Mbu aina ya Ngao katika zao hilo kwa lengo la kuua wadudu waharibifu wa zao hilo hali inayowaletea madhara walaji.
“Unajua wakulima wanapotosha sana matumizi sahihi ya dawa ya Ngao, imefikia baadhi ya wakulima wanapulizia katika miche ya nyanya hali inayopelekea walaji kudhulika,” Alisema Msemakweli.
Walisema pia dawa za uzazi wa mpango ambazo hutumiwa na akinamama kupanga uzazi zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya wafugaji huwapa kuku kwa lengo la kuwafanya wakue haraka ili kupata bei nzuri ya mifugo hiyo kutokana na tamaa ya pesa.
Wadau hao walisema wanyama aina ya Nguruwe nao wamekuwa wakipatiwa vidonge vya ARVs ambavyo hutolewa kwa wagonjwa wa Ukimwi ili kuwaongezea siku za kuishi na mazao ya mahindi na Maharage yamekuwa yakiwekewa dawa ya Ngao ya unga kwa imani kuwa hayatabunguliwa na Fukuzi wadudu waharibifu wa mazao.
Bi Grace Sanga wa asasi ya PROMISE ya mjini Iringa alisema upotoshwaji wa matumizi hayo ya dawa yanajengwa na uzushi ambapo wafugaji na wakulima huamini kuwa baada ya kuwapa mifugo dawa za binadamu, kuku na Nguruwe hukua haraka bila kuwa na ushauri wa kitaalamu.
Bwana Renatus Mpiluka mwanachama wa asasi ya MUNGONET ya Mufindi alifafanua kuwa hali hiyo inatokana na sera nyingi kutungwa na kuishia katika vitabu na wananchi kushindwa kuzifahamu hali inayopelekea baadhi ya wananchi kufanya mambo kinyume na utaratibu wa sera husika.
“Sera ya Kilimo, yenye kauli mbiu ya Kilimo kwanza naieleweki kwa baadhi ya wakulima ambao ndiyo walengwa wakuu wa mpango huo, kuna hajaya serikali kutoa elimu sahihi ya sera ili jamii izifahamu.” Alisema
Renatusi
Naye ndugu Leonard Kalolo mujumbe wa asasi ya LIMAU ya Mgololo wilayani Mufindi alisema wakulima na wafugaji wapatiwe elimu ili kupunguza matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizo pamoja na udhibiti wa usambaaji wa dawa za binadamu.
“Mbolea na madawa zinatumiwa vibaya, unakuta mtu anaweka mbolea hata kwenye mazao ya muda mfupi kama mboga mboga, hii inasababisha kumfikia mlaji kemikali za madawa hayo zikiwa bado hazijaisha na
kusababisha maradhi ,” alisema ndugu Kalolo.
Wadau hao wa asasi zisizo za Serikali waliitaka serikali itoe elimu sahihi kwa wakulima juu ya Sera mbalimbali zitolewazo na serikali ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi katika utungaji wa Sera
kwani wao ndiyo watekelezaji wakuu wa irani hizo.
Naye muhadhiri wa chuo kikuu cha Tumaini mkoani Iringa Lucas Mwahombela aliitaka serikali kuingilia kati ukiukwaji wa matumizi hayo ikiwa ni pamoja na kuziweka wazi sera mbalimbali hasa za Kilimo ambazo
zinawalenga watu wa hali ya chini ili wazielewe na kufanikisha sera ya Kilimo kwanza na kauli mbiu ya Mapinduzi ya Kijani.
MWISHO
No comments:
Post a Comment