Sunday, August 22, 2010

CHAKACHUA YA PINDA YAISUMBUA CHADEMA

Na Willy Sumia, Mpanda
WAZIRI mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda ambaye amepita bila kupingwa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Katavi mkoa wa Katavi kumeelezewa na wananchi wa jimbo lake kuwa ni uamuzi wa siku nyingi kabla hajateuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Hayo yalielezwa na baadhi ya wananchi wa jimbo hilo katika mahojiano ya hivi karibuni na waandishi wa Habari mara baada ya tume ya uchaguzi jimbo la Katavi kutangaza kuwa Pinda amepita bila kupingwa kutokana na wagombea wane wa CUF, CHADEMA, NLD na CHADEMA kujitoa katika kinyang’anyiro hicho kwa barua.
Wananchi hao wanaotoka katika vijiji vya Ilunde, Ilela, Majimoto, Kasansa na Kilida walidai kuwa tangu Pinda awe mbunge wa jimbo lao lililokuwa awali likiitwa jimbo la Mpanda Mashariki kumekuwa na maendeleo makubwa pamoja na mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi hao.
Ndugu Hussein Omari mkazi wa kijiji cha Inyonga alisema kuwa wananchi wa tarafa ya Inyonga walikuwa wakiteseka sana kutokana na kukosekana kwa barabara ya uhakika na mawasiliano ya simu lakini tangu Pinda awe mbunge wao wameweza kupata miundombinu hiyo kwa kasi ya ajabu.
Mmoja wa wagombea waliokuwa wametangaza nia ya kugombea katika jimbo hilo ndugu Sebastiani Kasinge alisema kuwa mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge jimbo la Katavi kwa Pinda alipata upinzani mkubwa sana toka kwa wananchi wa jimbo hilo, ndugu zake na hata ndani ya Chama chake cha CHADEMA.
Alisema kuwa uamuzi wake wa kuchukua fomukatika jimbo hilo ulipelekea mvutano mkubwa ndani ya CHADEMA na kupelekea mbunge wa jimbo la Mpanda kati CHADEMA Said Arfi kutangaza kujitoa katika uchaguzi iwapo chama chake kingesimamisha mgombea jimbo la Pinda ambapo mwenyekiti wa CHADEMA mwasisi aliamua kujivua uanachama wa CHADEMA na kuhamia chama kingine cha siasa katika kikao kilichokuwa kikijadili wagombea.
Chanzo cha uhakika cha habari toka katika chama cha CHADEMA kimeeleza kuwa CHADEMA ndio waliokuwa wakishinikiza Pinda apite bila kupingwa katika jimbo hilo lakini baadhi ya viongozi wa CCM walikuwa wakitaka kuwepo na mgombea ili wapate mshiko wa kampeni katika jimbo hilo na kutofautiana na katibu wa CCM wa wilaya Mohamed Omary Nyawenga aliyeonekana akifanya juhudi za kweli kuhakikisha Pinda anapita bila kupingwa akishirikiana na baadhi ya wananchi wa Inyonga.
MWISHO

No comments: