Thursday, April 19, 2012

APRIL 19 , 2012 - MAGAZETI NA HABARI

Magazeti Leo Alhamisi




Madudu Ya TBS Yanawachanganya Wabunge!

KAULI mbili zinazotofautiana zilizotolewa na mawaziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara juu ya tuhuma zinazomkabili bosi wa Shirika la Viwango (TBS), Charles Ekerege, zimewakera wabunge ambao wameitaka Serikali itoe tamko ni kauli ya waziri upi ni ya kweli.

Hatua hiyo ilijitokeza jana baada ya Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugora, kuomba Mwongozo wa Spika kutokana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu kutofautiana juu ya uchunguzi dhidi ya bosi wa TBS.

Wakati Nyalandu anajibu swali juzi alisema uchunguzi wa CAG umekamilika na ameshawasilisha ripoti serikalini, bosi wake, Dk. Chami alisema jana uchunguzi huo haujakamilika na unaendelea kufanywa na CAG.

Ekerege anatuhumiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) na ile ya Hesabu za Serikali (PAC) kuweka kampuni hewa za kukagua magari nje ya nchi na hivyo kuingizia hasara ya Sh bilioni 30 ambazo zimeainishwa katika ripoti ya CAG.

Baada ya Lugora kumaliza kuomba mwongozo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliyesema ni kweli majibu ya mawaziri hayo hayafanani na Serikali imeliona hilo, na Ofisi ya Waziri Mkuu itakusanya ushahidi wote juu ya jambo hilo na itatoa taarifa bungeni.

Lakini Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) alihoji kwa nini Serikali inashindwa kutoa majibu ya uhakika juu ya suala hilo wakati wabunge wanachotaka kufahamu ni kauli ipi yenye ukweli.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema kamati yake anayoiongoza ya Mashirika ya Umma iliunda kamati ndogo kushughulikia tuhuma zinazomkabili Ekerege na tayari wameshawasilisha taarifa kwa spika ambaye anatakiwa aipeleke Ofisi ya Waziri Mkuu ili walete taarifa ya utekelezaji bungeni.

Kwa upande wake, Naibu Spika Job Ndugai alikiri kuwa jambo hilo ni la muda mrefu umefika wakati liishie kwa kupatiwa ufumbuzi kwani linawapaka matope wabunge bila sababu za msingi. Chanzo: Habari Leo

Mkutano Wa Viongozi Wa Waislamu Na Wakristo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na baadhi ya viongozi wa dini alipowasili kwenye Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam,kwa ajili ya kufungua Kongamano la Dini la Waislam na Wakristo, lililoanza jana Aprili 18, 2012
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati akifungua rasmi Kongamano la Dini la Waislam na Wakristo lililoanza jana Aprili 18, kwenye Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
 

HALMASHAURI YA MJI MPANDA KUJENGA CHUO KIKUU CHA KILIMO 

 

HALMASHAURI ya Mji Mpanda mkoani Rukwa, ipo katika mchakato wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo (KUA) ili kuboresha huduma muhimu kwa maendeleo ya jamii na uchumi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mpanda, Nzori Kinero alisema hayo jana katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani cha kupitisha mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.

Alisema katika hatua za awali, halmashauri hiyo imeomba zaidi ya Sh bilioni tatu kutoka taasisi za kifedha ili kuanzia shughuli za uanzishwaji wa chuo hicho kinachotarajiwa kujengwa mwaka huu.

“Hata hivyo, Commercial Bank of Africa (T) Ltd wako tayari kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya uanzishwaji wa chuo hicho kwa sharti kwamba dhamana ya Serikali Kuu ipatikane kama mdhamini mkuu na Halmashauri ya Mji Mpanda ambaye ni mmiliki wa chuo hicho iwe mdhamini wa pili.

“Mchakato wa kupata udhamini wa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Fedha unaendelea vizuri na uko katika hatua za mwisho,” alisema Kinero.

Alisema halmashauri hiyo imeruhusiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa nambari nane ya mwaka 1982 na lengo ni kuiwezesha kutekeleza malengo na majukumu yake makuu.

Ili kutekeleza mradi huo, Kinero alisema halmashauri hiyo ya Mji itaongeza na kuboresha huduma za jamii na kiuchumi si kwa wakazi wa Mpanda pekee, bali Taifa kwa ujumla. Tayari halmashauri hiyo imeshapata usajili wa muda na kutambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.

No comments: