TAARIFA MBALI MBALI KUTOKA TFF LEO
Release No. 061
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 20, 2012
KOCHA NGORONGORO HEROES AAHIDI USHINDI
Kocha
Kim Poulsen anayeinoa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 cha
Tanzania (Ngorongoro Heroes) ameahidi kikosi chake kufanya vizuri kwenye
mechi dhidi ya Sudan.
Akizungumza
jana (Aprili 20 mwaka huu) kwenye mkutano na Waandishi wa Habari,
Poulsen amesema timu yake imejiandaa vizuri kwa mechi hiyo na kiu yao ni
kushinda.
Kwa
upande wake Kocha wa Sudan, Azhari Osman El Tahir amesema ingawa
haifahamu vizuri timu ya Tanzania, lakini wamejiandaa kushinda kwani kwa
muda mrefu walikuwa hawajashiriki mashindano ya vijana ya kimataifa.
Mechi
hiyo ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri huo itachezwa kesho
(Aprili 21 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10
kamili jioni kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh.
15,000.
Sudan
iliwasili nchini jana (Aprili 19 mwaka huu) ikiwa na kikosi cha
wachezaji 20, viongozi kumi na mwandishi wa habari mmoja kwa ajili ya
mechi hiyo ya kwanza kabla ya timu hizo kurudiana jijini Khartoum kati
ya Mei 4, 5 na 6 mwaka huu.
Mechi
hiyo itachezeshwa na mwamuzi Brian Miiro atakayesaidiwa na Mark Ssonko,
Lee Patabali na Denis Batte wote kutoka Uganda. Ejigu Ashenafi wa
Ethiopia ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 15.
Fainali
za Afrika kwa michuano hiyo zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria
wakati za Dunia zitafanyika nchini Uturuki kuanzia Juni hadi Julai
mwakani. Katika fainali za Dunia, Afrika itawakilishwa na timu nne za
kwanza kwenye fainali za Algeria.
MALINZI MGENI RASMI MKUTANO MKUU TFF
Mwenyekiti
wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi anatarajia kuwa
mgeni rasmi kwenye ufunguzi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika kwa siku mbili (Aprili 21 na 22
mwaka huu) kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam.
Wajumbe
wa mkutano huo watawasili jijini kesho (Aprili 20 mwaka huu) na
watafikia kwenye hoteli ya Royal Valentino. Wajumbe wanatoka katika
vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu
ya Vodacom.
Mkutano
huo utakaoanza saa 3 asubuhi utakuwa na ajenda kumi na moja. Baadhi ya
ajenda hizo ni hotuba ya Rais wa TFF, taarifa ya utendaji ya mwaka 2011,
bajeti ya mwaka 2012 na taarifa ya ukaguzi wa hesabu (audited
accounts).
MECHI ZA VPL WIKIENDI HII, MAREKEBISHO
Ligi
Kuu ya Vodacom inaingia raundi ya 24 wikiendi hii kwa mechi mbili
zitakazochezwa Aprili 22 jijini Dar es Salaam. Villa Squad itaumana na
African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi wakati Yanga itakuwa mwenyeji wa
Polisi Dodoma katika Uwanja wa Taifa.
Azam
na Mtibwa Sugar zilizokuwa zicheze Aprili 21 mwaka huu sasa zitacheza
Aprili 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati siku
hiyo hiyo jioni kutakuwa na mechi kati ya Simba na Moro United. Mechi
zote zitaanza saa 10.30 jioni.
Aprili
25 mwaka huu Oljoro JKT itaikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati JKT Ruvu itakuwa
mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Raundi
ya 25 itakamilika kwa mechi nne; Aprili 28 mwaka huu Coastal Union
itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga
huku Mtibwa Sugar ikiwa mgeni wa African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi.
Azam na Toto African zitacheza Chamazi, Aprili 30 mwaka huu wakati Mei 1
mwaka huu Villa Squad itaumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Chamazi.
Ligi
hiyo itafunga msimu wa 2011/2012, Mei 5 mwaka huu ambapo timu zote 14
zitakuwa uwanjani. Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs
Polisi Dodoma (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Ruvu Shooting vs Villa
Squad (Mabatini, Mlandizi), Coastal Union vs Toto African (Mkwakwani,
Tanga), African Lyon vs JKT Ruvu (Manungu, Morogoro), Azam vs Kagera
Sugar (Chamazi, Dar es Salaam) na Moro United vs Mtibwa Sugar (Jamhuri,
Morogoro).
WASWAZI KUCHEZESHA SIMBA, AL AHLY SHANDY
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Swaziland
kuchezesha mechi ya kwanza ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho kati ya
Simba na Al Ahly Shandy ya Sudan itakayochezwa Aprili 29 mwaka huu
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi
hao wa mechi hiyo namba 71 ni Nhleko Simanga Pritchard atakayepuliza
filimbi wakati wasaidizi wake ni Mbingo Petros Mzikayifani na Sibandze
Thulani. Mwamuzi wa mezani atakuwa Fakudze Mbongiseni Elliot.
CAF pia imemteua Kayijuga Gaspard wa Rwanda kuwa Kamishna wa mechi hiyo.
KAMPUNI NNE ZAPITA TENDA YA TIKETI
Kampuni
nne kati ya sita zimepita hatua ya kwanza ya mchakato wa kupata moja
itakayofanya kazi ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya
mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na nyingine zinazosimamiwa na Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Shughuli
ya ufunguzi wa maombi ya hatua ya awali ya kuonesha nia (Expression of
Interest) kwa ajili ya tenda hiyo ilifanywa jana (Aprili 19 mwaka huu)
na Kamati ya Mipango na Fedha ya TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya
shirikisho.
Kampuni
ambazo zimepita hatua hiyo ya kwanza sasa zinatakiwa kuwasilisha rasmi
tenda zao kwa ajili ya shughuli hiyo ndani ya kipindi cha wiki tatu
tangu ulipofanyika ufunguzi wa hatua ya kwanza.
Baadaye
Bodi ya Tenda itakutana tena kupitia tenda zitakazokuwa zimewasilishwa
na kufanya uteuzi wa kampuni moja itakayofanya kazi hiyo.
Kampuni
ambazo zimefanikiwa kuingia katika hatua hiyo ya pili ni CRDB Bank PLC,
SKIDATA People Access Inc., Prime Time Promotions na Punchlines (T)
Limited.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)