Dr Mwakyembe
Waziri wa Uchukuzi Dr Harrison Mwakyembe
amewaafukuza kazi EPHRAIM MGAWE, na Naibu wake Bwana JULIUS MFUKO
kufuatia ripoti iliyotolewa na tume maalum ya kuchunguza hali ya
uendeshwaji wa bandari hiyo na kuonyesha kuwa watendaji hao wamekosa
umakini pamoja na kufanya uzembe uliopitiliza.
Akisoma
ripoti hiyo Dokta MWAKYEMBE amesema kuwa Viongozi hao wameshindwa
kuonyesha umaridadi wa kuisimamia bandari hiyo, hali iliyopelekea
kuisababishia Hasara kubwa Serikali sambamba na kushusha hadhi ya
Bandari ya Dar es Salaam, hadi kufikia hatua ya kutajwa kama Bandari
isiyoingiza faida yoyote miongoni mwa Bandari 36 za barani Afrka.
Katika
Hatua nyingine Dokta MWAKYEMBE ametangaza kuwafukuza kazi Meneja Mkuu
wa Bandari hiyo KASSIAN NGAMILO pamoja na Meneja wa kitengo cha Mafuta
CAPTAIN TUMAINI MASSAWE, kufuatia kushindwa kusimamia ipasavyo mikataba
mbalimbali ya uondoshaji wa mafuta machafu bandari hapo sambamba na
uzembe uliopitiliza.
Hata hivyo
Dokta MWAKYEMBE amebainisha kuwa Wizara yake haitamvumilia mtendaji
yeyote kutoka idara ama taasisi iliyo chini ya Wizara hiyo ambaye
utendaji wake utaonekana kulega lega, na kusabaisha Serikali kupata
hasara pasipo sababu za Msingi.
Kufukuzwa
kwa Viongozi hao ni miongoni mwa utekeleza wa uboreshaji wa Bandari ya
Dar es Salaam ambayo imeshika nafasi ya Mwisho kwa uingizaji faida
katika Bandari 36 za Bara la Afrika hii ni ikiwa ni Ripoti iliyotolewa
hivi karibuni.
HABARI HII NI KUTOKA MTANDAO WA www.francisgodwin.blogspot.com
NAIBU waziri wa
Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa nchini, Aggrey Mwanri baada ya kufanya
ziara na kuibua mambo mazito ikiwa ni pamoja na kigugumizi ya Manispaa ya
Sumbawanga kuwasha umeme katika stendi kuu ya mabasi mjini humo anatarajia
kuanza ziara kama hiyo mkoani Katavi ambako atatembelea, kukagua na kuweka mawe
ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Taarifa zinasema kuwa
waziri huyo ambaye amefanya ziara ya siku tisa mkoani Rukwa atafanya ziara
mkoani kKatavi katika Halmashauri zote kuanzia Januari 16, 2013 hadi Januari
21, 2013 ambapo atafanya kazi kubwa ya kukagua miradi, kuweka mawe ya msingi
katika miradi kuzindua na hatimaye atakuwa anafanya mikutano ya hadhara.
Naibu Waziri Mwanri
amekuwa na tabia ya kukagua miradi kwa vitendo ambapo akiwa mjini Sumbawanga
aliweza kukagua upana wa barabara kwa kutumia tepu ya kupimia na kukagua uimara
wa sakafu na kuta za majengo aliyoakagua kwa kutindua na tindo kwa kutumia
tindo na nyundo vitendo ambavyo vimejenga dhana ya uwajibikaji kwa watendaji wa
halmashauri na manispaa
Akiwa katika mkoa wa
Katavi Mhe. Mwanri atatembelea wilaya mbili za Mlele na Mpanda zinazounda
halmashauri nne ambazo ni Halmashauri ya wilaya ya Mlele, halmashauri ya wilaya
ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo na halmashauri ya mji Mpanda.
Katika blog hii tutajitahidi kukuletea yatakayojiri katika ziara hiyo kwa wakati ili uweze kuelewa nini kimefanyika.
Waziri Wasira
NA MWANDISHI WETU
UHALISIA wa kukua kwa uchumi hadi mifukoni mwa wananchi walio wengi una matumaini ya kufikiwa kutokana na
utekelezwaji madhubuti wa kuinua Kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza unayotekelezwa na serikali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera na Uratibu, Steven Wasira alipokuwa akizungumza kwenye
kipindi cha 'Tuongee Asubuhi' cha kituo cha televisheni cha Star Tv, leo, Januari 15, 2013.
Katika kipindi hicho, kilichokuwa na mada ya 'Uhalisia na Kukua kwa Uchumi' pamoja na Wasira wazungumzaji wengine
walikuwa, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo cha SAUTI cha Mwanza, Odas Bilame.
Wasira alisema, kwa sasa wananchi wengi hawaoni uhalisia wanapoambiwa kwamba uchumi wa nchi unakuwa, kwa
sababu, hali ya kukuwa kwa uchumi kwa sasa hakujawagusa waajiriwa katika sekta ya kilimo ambao ndio wengi kiasi
cha asilimia 80.
Alisema, katika kipindi cha kati ya mwaka juzi na mwaka jana uchumi wa Tanzania ulionyesha kuwa umekuwa kwa kati
ya asilimia 6.5 na 6.7, lakini kukua huku kuliwagusa zaidi watumishi waliopo katika sekta nyingine kama za viwanda na
watumishi wa umma.
"Katika hali hii ambayo watumishi wa sekta zote wanategemea lazima wapate chakula na mazao mengine kutoka kwa
wakulima, ambao hawajanufaika vya kutosha na mafanikio ya kukua wa uchumi huu, ni lazima, athari za kutoonekana
ukuaji uchumi katika jamii utakuwepo", alisema, Wasira.
Alisema,
kutokana na kutambua kwamba ni lazima sekta ya Kilimo iboreshwe vya
kutosha ndipo ukuaji wa uchumi utadhihirika kwa uhakika miongoni mwa
wengi, Serikali imeelekeza nguvu zake kuhakikisha mpango wa Kilimo
Kwanza unazaa matunda.
Alisema, katika jitihada za kufikia lengo hilo, Serikali imetenga
sh. bilioni 300 kwa ajili ya kuwekeza kwenye utafiti katika kilimo,
ambapo katika uwekezaji huo, sasa wapo wataalam wengi na maofisa ugani
vijijini kwa ajili ya kuwezesha wakulima kufanya kilimo bora na cha
kisasa.
Wasira alisema, pia kiwanda cha mbolea cha Minjingu kimejengwa ili
kuongeza upatikanaji wa mbolea ili kuhakikisha kwamba kila mkulima
anapata mbolea ya kutosha na kuongeza kuwa pamoja na kiwanda hicho
Serikali inao mpango wa kujenga vingine vya mbolea ili kuongeza wigo wa
upatikanaji wa pembejeo hiyo.
Alisema, wakati jitihada zimewekwa kwenye uinuaji sekta ya kilimo,
ujenzi na uboreshaji miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara na reli,
utafungua milango ya mazao kutoka vijijini kwenda maeneo mbalimbali
nchini hata nje ya nchi kwa urahisi, hatua ambayo itachochea kukua kwa
kasi zaidi kwa uchumi.
Akielezea historia ya Uchumi wa Tanzania, Wasira alisema, awali hali
ya uchumi ilikuwa ikienda vizuri, lakini ilianza kuathiriwa na uhaba wa
mafuta miaka uliojitokeza miaka ya 1977 lakini ukaendelea kuathiriwa
zaidi na vita vya Kagera, mwaka 1978 na hadi sasa zimeendelea kuwepo
changangamoto za kidunia ambapo Tanzania kama moja ya nchi zilizomo
haiwezi kuzikwepa.
Kwa upande wake Profesa Lipumba, alikiri kwamba Kilimo Kwanza ni
'muarobaini' wa kukua kwa uchumi wa nchi, lakini akaonya kwamba ni
lazima juhudi za makusudi zifanyike kuhakikisha kuwa uhalisia wa kukua
wa uchumi ni kuigusa mifuko ya wananchi.
Pamoja na kukiri umuhimu wa mpango wa kilimo kwanza, Profesa Lipumba
aliponda kwamba, licha ya mikakati mizuri kuwepo lakini mingi ipo
katika makatarasi tu, haitekelezwi kwa vitendo.
"Sasa kama
dhamira ipo, umefika wakati wa watekelezaji kuacha maneno na badala yake
kufanya kazi kwa vitendo zaidi", alisema Lipumba.
Kwa upande wa nafasi ya wasomi wanavyoisadifu hali ya kukua kwa
uchumi Tanzania, Odax alisema, wasomi wanakubalina kwamba juhudi
zikiwekezwa kwenye kilimo uchumi utakuwa. |
|
Dr Makongolo Mahanga, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Tanzania |
NAIBU Waziri wa Kazi na Ajira, Dr. Makongoro Mahanga ameshauri vyuo vya elimu
ya juu kurekebisha mitaala yao ili kukazania zaidi masomo ya hisibati na
sayansi, na pia kuhakikisha kwamba kwenye kila fani au program katika vyuo
hivyo, kunakuwepo na masomo ya ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwaandaa
wahitimu kujiajiri kama hawatapata kazi za kuajiriwa. Aidha ameshauri
kwamba, kama ilivyofanywa kwa fani ya ualimu, kuwepo na program au shahada
mahsusi ya ujasiriamali katika kila chuo cha elimu ya juu.
Dr. Mahanga ametoa ushauri huo jana mjini Mtwara alipokuwa akiwahutubia
wananchi wa Mtwara, viongozi na wahitimu katika chuo kishiriki cha Stella Maris
kilichoko Mtwara na kinachomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
Alisema sababu kubwa ya baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu kukosa ajira ni pamoja
na vijana hao kutotaka au kuweza kuchukua masomo ya sayansi na hisibati na pia
kutotaka kuchukua fani kama ya ualimu ambazo zina fursa za uhakika za ajira.
Aidha, alisema sera na mitaala ya elimu haijazingatia sawasawa mahitaji ya soko
la ajira. Alisema sababu nyingine ni ukosefu wa nafasi za kujifunza elimu ya
ufundi, ujasiriamali na stadi za kazi au kufanya mazoezi ya stadi za kazi ili
kupata ujuzi wa aina ya ajira nzuri kwenye soko la ajira. Hivyo kuanzisha
masomo au shahada ya ujasiriamali kwenye vyuo vikuu vyote ingeweza kuwa
suluhisho la wahitimu wengi kukosa ajira. Alisema kwa sasa kati ya vijana zaidi
ya 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka baada ya kumaliza elimu
ya msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu, vijana 240,000 hawapati ajira
kabisa na baadhi yao ni wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu.
> >>
> >> Dr. Mahanga, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ya kwanza
ya chuo hicho ambacho ni chuo kishiriki cha Chuo Kikuu cha St. Augustine cha
Mwanza, aliwataka pia wahitimu wanaokopeshwa na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi
kurejesha mikopo hiyo wakishaanza kufanya kazi. Akitoa takwimu za mikopo ya
wanafunzi, alisema kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1994/95 ambapo mikopo hiyo
ilianza kutolewa kwa wanafunzi hadi Juni 2012, Serikali imeshatoa mikopo ya
shs. 1.184 trilioni kwa wanafunzi 593,712. Hata hivyo alisema kati ya mikopo
ilioiva na kustahili iwe imesharudishwa na wahitimu waliokopa ni asilimia 49%
tu imeshalipwa kwa Bodi.
HOTUBA CHINI
HOTUBA YA MHE. DKT. MILTON MAKONGORO MAHANGA (MB), NAIBU WAZIRI WA KAZI NA
AJIRA KWENYE MAHAFALI YA KWANZA YA CHUO KIKUU CHA STELLA MARIS MTWARA
(STEMMUCO), TANZANIA TAREHE 5 DESEMBA, 2012
Mhashamu Baba Askofu Mkuu, Norbet Mtega – Mkuu wa Chuo,
Mhashamu Baba Askofu Gabriel Mmole, Askofu wa Jimbo la
Mtwara na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo,
Mhashamu Baba Askofu John Ndimbo, Askofu wa Jimbo la Mbinga
na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo,
Mhashamu Baba Askofu Bruno Ngonyani, Askofu wa Jimbo la
Lindi,
Mhashamu Baba Askofu Castor Msemwa, Askofu wa Jimbo la
Tunduru Masasi,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara,
Waheshimwa Wakuu wa Vyuo na Taasisi za Elimu,
Mabibi na Mabwana.
Tumsifu Yesu Kristu!
Ni heshima kubwa kwangu binafsi na kwa Serikali kwa ujumla kunipa mwaliko wa
kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hili la kihistoria, tukio la mahafali ya kwanza
ya Chuo hiki Kishiriki cha Stella Maris hapa Mtwara.
Kwa kunialika kushiriki tukio hili, ni ishara wazi inayoonyesha ushirikiano
uliopo kati ya Serikali na Taasisi hii katika suala zima la kutoa elimu kwa
Watanzania – elimu inayowajengea wahitimu uwezo kiujuzi, kiuelewa, kiutaalam,
kimitazamo na kimaamuzi ili waweze kushiriki kwa vitendo kuleta maendeleo
halisi ya Taifa letu.
Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana,
Umuhimu wa elimu katika maendeleo ya taifa lolote haliwezi kusisitizwa
zaidi. Nchi zote ambazo zimeendelea kwa haraka duniani zimewekeza katika
elimu ya watoto na vijana wake. Tanzania vile vile imekuwa ikiwekeza
kiasi kikubwa cha bajeti yake katika sekta ya elimu na kuipa kipaumbele cha
kwanza kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka 2010/11 Serikali ya Tanzania
ilitenga shs. 2.195 trilioni kwa ajili ya sekta ya elimu, hii ikiwa ni asilimia
18.9% ya bajeti nzima ya Serikali. Kwa mwaka 2011/12, Serikali ilitenga
shs. 2.415 trilioni kwa ajili ya sekta ya elimu (asilimia 17.86%).
Kwa kushirikiana na watu binafsi na Taasisi mbalimbali likiwemo Kanisa
Katoliki, Serikali inatilia maanani umuhimu wa kutoa elimu bora kwa raia.
Serikali imekuwa inafuatilia kwa makini kupitia Tume na vyombo vyake vingine,
utoaji wa elimu iliyo bora, elimu yenye kumkomboa mwanadamu na kumpa uwezo wa
kuyatawala na kuyaboresha mazingira yake. Kwa misingi hiyo, kwa niaba ya
Serikali, natoa shukrani zangu za dhati kwa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania kwa ushiriki wake wa kutoa elimu bora ya ngazi zote tangu elimu ya
awali hadi elimu ya juu. Ushiriki wa Kanisa katoliki na taasisi zingine za
kidini na watu binafsi katika fani ya elimu umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta
maendeleo ya Taifa letu.
Wakati ambapo kufikia mwisho wa mwaka 2010/11 vyuo vya elimu ya juu vilikuwa na
jumla ya wanafunzi 139,638, vyuo vya Serikali vilikuwa na wanafunzi 104,129
huku vyuo binafsi vikiwa na wanafunzi 35,509. Hata hivyo vyuo vya elimu ya juu
vya Serikali vilikuwa 11 tu kulinganisha na 21 vya binafsi. Hii ina maana
kwamba vyuo binafsi vilikuwa vingi (65.6%) kulinganisha na vya Serikali (34.4%)
lakini viliweza kudahili wanafunzi asilimia 25.4% tu. Kwa maana hiyo kuna haja
ya vyuo binafsi kupanua miundombinu ya vyuo vyake na udahili ili viweze
kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Maaskofu, Mabibi na Mabwana,
Ikijua na kujali umuhimu na mchango wa vyuo binafsi, Serikali, kupitia Tume
yake ya Vyuo Vikuu (TCU), mnamo Desemba 2009, iliruhusu Taasisi hii ianze kutoa
elimu ya juu kama kituo cha chuo kikuu cha SAUT. Miaka miwili baadaye, yaani
Julai, 2011 Serikali iliipandisha hadhi Taasisi hii na kuifanya Chuo Kikuu
Kishiriki.
Ikitambua uwezo mdogo wa kiuchumi wa Watanzania, Serikali kupitia Bodi yake ya
mikopo imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wenye
vigezo vinavyotakiwa. Kwa miaka 11 toka mikopo hii ianze kutolewa mwaka 1994/95
hadi 2004/2005, jumla ya wanafunzi 113,240 waliweza kukopeshwa jumla ya
shilingi 51,103,687,000. Lakini kwa miaka saba ya awamu ya nne ya
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kutoka mwaka 2005/06 hadi 2011/12, Serikali,
kupitia Bodi ya Mikopo iliyoundwa mwaka 2005, ilikopesha wanafunzi 480,472 jumla
ya shs. 1,133,386,869,000.
Mabibi na Mabwana,
Kama ilivyoelezwa hapa leo, chuo hiki pia kilifaidika na mikopo hii ambapo
asilimia 94% ya wahitimu wake wamewezeshwa kwa njia ya mikopo hiyo. Aidha
kupitia Serikali za Mitaa hapa Mtwara-Mikindani, Serikali imetoa ardhi
takribani ekari 140 kwa ajili ya maendeleo ya chuo hiki. Haya yote yanaonyesha
jinsi Serikali yetu inavyojali watu wake katika masuala ya elimu. Kwa niaba ya
Serikali nawaahidi kwamba ushirikiano huu utaendelea kudumishwa.
Inafurahisha na kutia moyo kuwa Chuo hiki kiliona ni vema kuanza kazi yake
Mkoani Mtwara kwa kuandaa walimu wa sekondari. Tunda la kwanza la chuo ni
walimu walioandaliwa kutoa elimu ya Sekondari. Elimu hii itachangia kwa kiasi
kikubwa katika kuleta maendeleo ya watanzania tukizingatia kuwa zipo shule
nyingi za sekondari zenye idadi ndogo ya walimu. Tukianzia na Mikoa ya Kusini,
mmejionea wenyewe uhaba wa walimu uliopo. Ninawahimiza wahitimu wa leo wawe
tayari kuitumia elimu yao kuchangia kuleta maendeleo ya watanzania.
Mabibi na Mabwana,
Ukosefu wa ajira bado ni tatizo kubwa nchini, hasa kwa vijana. Kati ya vijana
wapatao 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka baada ya kumaliza
masomo ya msingi, sekondari na vyuo vya juu, ni asilimia kama 5 tu (au vijana
40,000) ndio wanapata ajira kwenye sekta rasmi isiyo ya kilimo. Waliobaki
wanaingia kwenye ajira kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi (asilimia 35)
na sekta isiyo rasmi (aslimia 30), huku asilimia 30 waliobaki (vijana 240,000)
wakikosa kazi. Kati ya vijana wanaoingia kwenye soko la ajira na kukosa kazi,
wako pia wahitimu wa vyuo vikuu.
Sababu kubwa ya baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu kukosa ajira ni pamoja na
vijana hao kutotaka au kuweza kuchukua masomo ya sayansi na hisibati na pia
kutotaka kuchukua fani kama ya ualimu ambazo zina fursa za uhakika za ajira.
Aidha, sera na mitaala ya elimu haijazingatia sawasawa mahitaji ya soko la
ajira. Na pia kuna ukosefu wa nafasi za kujifunza elimu ya ufundi, ujasiriamali
na stadi za kazi au kufanya mazoezi ya stadi za kazi ili kupata ujuzi wa aina
ya ajira nzuri kwenye soko la ajira.
Ningependa kutoa wito kwa vyuo vya elimu ya juu kurekebisha kasoro hizi kwa
kutilia maanani masomo ya hisibati na sayansi, na pia kuhakikisha kwamba kwenye
kila fani au program katika vyuo vikuu vyote, kunakuwepo na masomo ya
ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwaandaa wahitimu kujiajiri kama
hawatapata kazi za kuajiriwa. Aidha ningeshauri kwamba, kama ilivyofanywa kwa
fani ya ualimu, kuwepo na program au shahada mahsusi ya ujasiriamali (Bachalor
of Business Administration/Management in Entreprenuership) katika kila chuo cha
elimu ya juu. Nimeona kwamba ingawa leo wahitimu wa chuo hiki ni wa fani ya
ualimu mlioanza nayo, lakini kwa sasa mmeshaanzisha program za shahada zingine
hapa chuoni. Angalieni pia uwezekano wa kuanzisha shahada ya ujasiriamali
katika mipango yenu ya baadaye.
Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana,
Kabla sijamaliza hotuba yangu, nitoe wito kwa wenzetu 1,100 wanaohitimu leo
katika chuo hiki cha Stella Maris kama ifuatavyo:-
• Uadilifu kazini: Wahitimu mmefundishwa sio tu kuwa walimu
bali walimu-walezi. Serikali inawatazamia kuwa mifano bora kazini kwa kuyaishi
maadili ya kazi yenu. Epukeni upendeleo, rushwa na unyanyasaji. Fanyeni kazi
kwa haki na ueledi wa hali ya juu.
• Utayari wa kurudisha pesa ya mikopo: Mmesoma kwa pesa ya
mikopo. Kumbukeni kulipa madeni ili wakopeshwe wengine. Tatizo la wahitimu wa
vyuo vikuu kurudisha mikopo waliokopeshwa bado ni kubwa. Kwa mfano, kufikia
Juni 2012, madeni ya wahitimu wa vyuo vya juu yaliyokuwa yameiva yalikuwa Tshs.
bilioni 160.7 na kati yake, shs. 39.5 bilioni zilitakiwa ziwe zimeshakusanywa
kutoka kwa waliokopa, lakini ni asilimia 49% tu kati ya hizo zilikuwa
zimekusanywa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
• Maslahi Binafsi: Katika kazi zenu za ualimu lazima
mtangulize maslahi ya wengi na wala si maslahi binafasi
• Migomo na Vurugu: Ni muhimu mkaepuka migomo na vurugu
kazini. Pale migogoro inapotokea, ni lazima mtafute suluhisho za migogoro kwa
mazungumzo na pande zote zinazohusika.
• Utayari wa kufanya kazi popote bila kubagua maeneo: Fanyeni
kazi popote nchini bila kupendelea mijini au maeneo ya nyumbani kwenu. Katika
risala ya chuo mmeeleza jinsi imekuwa vigumu wahitimu kufanya kazi kwenye
maeneo fulani ya nchi, kwa mfano katika mikoa hii ya kusini ikiwemo Mtwara na
Lindi. Kwanza sitegemei wahitimu wa chuo hiki hapa Mtwara baada ya kuzoea
mazingira ya mkoa huu na ya jirani walipokuwa wakisoma, wakashindwa kufanya
kazi huku baada ya kumaliza masomo yao. Lakini pia nyie wenyewe ni mashahidi
kwamba Serikali imekuwa ikichukua hatua za makusudi kuboresha hali ya maisha na
miundombinu ya mikoa iliyokuwa inaonekana iko nyuma kimaendeleo kama Mtwara ili
wananchi wa mikoa hii na watanzania wengine wanaopangwa kufanya kazi kwenye
mikoa hii wasione tofauti kubwa na mikoa mingine.
Kwa upande wa Mtwara na mikoa mingine ya kusini, ukiacha uboreshaji mkubwa wa
miundombinu ya barabara, umeme na bandari, kumekuwepo vile vile uwekezaji
kwenye miradi ya kiuchumi kama utafiti na uchimbaji wa gesi asilia, utafiti wa
mafuta na viwanda kadhaa kama vya saruji na mbolea vinavyotarajiwa kuanza
kujengwa karibuni. Yote haya yamefanya mikoa hii ianze kuwavutia hata wananchi
wengine kupenda kuishi, kufanya kazi, kuwekeza na kufanya biashara katika mikoa
hii.
Hapa ningependa kuwapongeza Baraza la Maaskofu Katoliki kwa kuanzisha chuo hiki
hapa Mtwara na kukipa jina la Stella Maris linaloendana na maendeleo
yanayoendelea kuwepo katika mkoa huu wa Mtwara. Jina hili nimeambiwa maana yake
ikitafsiriwa kwa kilatini ni “Nyota ya Bahari”. Jina hili linabeba dhana
nzima ya uwepo wa chuo hiki mkoani Mtwara, kwa maana ya kuwa chimbuko la mwanga
na matumaini katika misukosuko ya kimaisha, kielimu, kitaaluma na
kiuchumi. Jina hilo pia linaendana na maendeleo na uwekezaji unaoanza kuonekana
hapa mkoani Mtwara kama nilivyoeleza hapo juu.
Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana
Kwa upande wa Serikali ningependa kuahidi yafuatayo:-
Ajira kwa walimu: Kwa kuzingatia uhitaji uliopo, Serikali
inawaahidi wahitimu wa chuo hiki kupewa ajira katika fani ya ualimu, kama
ambavyo imekuwa ikifanya kila mwaka kwa wahitimu wa fani hii. Kwa mfano katika
mwaka 2011, Serikali ilitoa ajira 11,629 kwa walimu wa shule za sekondari kote
nchini na kufanya shule hizo kuwa na walimu 52,146 mwaka 2011 kulinganisha na
walimu 40,516 waliokuwepo mwaka 2010 katika shule zote za sekondari za Serikali
na binafsi nchini.
Sera nzuri kwa kazi ya ualimu: Serikali inaahidi kuendelea
kuweka sera nzuri kwa kazi ya ualimu ili kuondoa kero za walimu zinazowapelekea
kugoma na kuona kwamba taaluma yao haithaminiwi na Serikali.
Mwisho kabisa, niwaombe wananchi na wakazi wa Mtwara, mpokee taasisi zilizo
Mtwara kama baraka na wadau wa kuleta maendeleo. Kwa misingi hiyo wapokeeni
wanafunzi wasomao vyuoni Mtwara kama watoto wenu. Wapokeeni kama wapangaji
kwenye nyumba zenu kwa gharama za kiungwana bila kuwadai pesa nyingi kupita
uwezo wao. Wenye vyombo vya usafiri tozeni gharama za haki.
Nimalizie kwa kuwashukuru tena Baraza la Maaskofu Katoliki na uongozi wa chuo
kwa kunialika kujumuika nanyi katika mahafali ya kwanza ya chuo hiki kikuu
kishiriki cha Stella Maris, na niwatakie kila la heri kwenye kazi zao wahitimu
wetu wa leo.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA