MTUHUMIWA WA MAUWAJI YA MWANGOSI AKWAMA MAHABUSU TENA
Huyu ndie mtuhumiwa wa mauwaji ya Daudi Mwangosi |
MTUHUMIWA wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi aliyetakiwa kufikishwa mahakamani kwa mara nyingine kutokana na sababu ya magari ya kubebea mahabusu kukosa mafuta.
Mwandishi wa mtandao huu kutoka Iringa Gustav Chahe anaripoti kuwa ,Askari wa kikosi cha kuzuia ghasia wengine waliokuwa na silaha mbalimbali huku wengine wakivaa kiraia waliweka ulinzi mkali kuhakikisha waandishi wa habari hawapati mwanya wa kupiga picha.
Mwendesha mashtaka wa serikali Adolf Maganda aliambia mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Dyness Lyimo kuwa mtuhumiwa hakufikishwa mahakamani kutokana na magari ya kuwabeba mahabusu yamekosa mafuta.
Hata hivyo Maganda alisema upelelezi haujakamilika na kesi imeahilishwa hadi 19 Desemba mwaka huu.
Pasificus Cleophace Simon (23) alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa tuhuma ya kumuua kwa makusudi mwandishi huyo katika ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa uliofanyika Septemba 2 mwaka huu.
Siku ya kwanza mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa gari la kifahari lenye namba za kiraia T 320 ARC linalosadikiwa kuwa ni la RCO huku kwa mara ya pili akifikishwa kwa miguu na kuondolewa mahakamani hapo kwa gari namba DFP 2175 pick up akiwa katika ulinzi mkali huku waandishi wa habari wakidhibitiwa na polisi na mmoja wao kunusurika kupigwa jambo lililozusha hisia tofauti miongoni mwa wananchi wengi mkoani hapa.
Hii ni mara ya pili kwa mtuhumiwa huyo kutokufikishwa mahakamani kutokana na sababu ya magari kukosa mafuta japo kuwa kwa wakati huu hakuna tatizo la mafuta kama kipindi cha mwanzo.
Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2 mwaka huu katika kijiji cha Nyololo yo alipokuwa akiwajibika kwa kazi za kihabari wakati wa ufunguzi wa matawi hayo.