Miaka 51 yawatoa jela wafungwa 3,814,sherehe uwanja wa taifa nazo zanoga
Baraza la mawaziri na wawakilishi wa mataifa ya nje nchini |
Wale wanaokumbukaSharo milionea katika mkasa wa kukabidhiwa mikoba aliona mkia wakerewe hawa walifanya mambo |
Warembo kutoka nchi jirani ya Rwanda walifika kuwakilisha uzuri katikia maonesho ya miaka 51 ya Uhuru |
Hata kama uko jukwaani na jana uliwaona lazima uwasalimie:Jk akisalimiana na baadhi ya wakuu na wageni wengine waliofika kutupa tafu miaka 51 |
RAIS Jakaya Kikwete na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
na Usalama nchini, ametoa msamaha kwa wafungwa 3,814 wakiwemo wenye magonjwa
yasiopona na wanawake wajawazito.
Hata hivyo msamaha huo uliotolewa kuadhimisha Miaka 51 ya Uhuru
wa Tanzania, hauwahusu wafungwa wenye makosa ya ubakaji, ulawiti, kuwapa
wanafunzi mimba, waliotumia madaraka vibaya na wala rushwa.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi imeeleza kuwa, Rais Kikwete
ametekeleza hilo kwa kutumia madaraka aliyonayo chini ya Ibara ya 45 (1) (d) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wafungwa waliohusika na msamaha
huo ni waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu (TB) na saratani
ambao wako katika hali mbaya, wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea.
“Wamo waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kuwepo gerezani kwa
ridhaa ya Rais wa Tanzania chini ya kifungu cha 26 cha Kanuni ya Adhabu, ambao
hadi Desemba 9, mwaka huu wamekaa gerezani si chini ya miaka mitano na wamekuwa
na tabia njema,” alisema Dk Nchimbi.
Wengine ni wafungwa wanawake walioingia na mimba au na watoto
wadogo gerezani, wenye ulemavu wa mwili na akili, wanaotumikia kifungo
kisichozidi miaka mitano na ambao walishatumikia robo ya kifungo chao.
Dk Nchimbi alisema kuwa, kutokana na madaraka hayo, Rais
Kikwete ametoa msamaha huo kwa wafungwa 3,814 na kwamba wafungwa wenye matatizo
maalum kati ya waliosamehewa, wamethibitishwa na jopo la madaktari chini ya
Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya husika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, msamaha huo hauwahusu wafungwa
waliohukumiwa kunyongwa, kifungo cha maisha, waliofungwa kwa kujihusisha na
dawa za kulevya, waliotoa au kupokea rushwa na wenye makosa ya unyang’anyi wa
kutumia silaha na wizi wa magari kwa silaha.
Pia hauwahusu waliopatikana na makosa ya kunajisi, kubaka na
kulawiti, waliowapa wanafunzi mimba, walioharibu miundombinu kama kuiba nyaya
za simu, umeme au mafuta ya transformer na waliokutwa na silaha au risasi.
Dk Nchimbi alisema wengine wasiohusika ni wafungwa wazoefu
wanaotumikia kifungo cha pili na kuendelea, waliowahi kupewa msamaha lakini
wanatumikia sehemu ya kifungo kilichobaki, waliowahi au kujaribu kutoroka na
waliotumia madaraka vibaya.
Wengine ni waliohukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kusoma na
wale wanaotumikia kifungo chini ya Sheria namba 25 ya mwaka 1994 ya Bodi ya
Parole na Sheria ya Huduma kwa Jamii
namba 6 ya mwaka 2002.
Katika maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa
Tanzania mwaka jana, Rais Kikwete alitoa msamaha kwa wafungwa 3,803 na mwaka 2010
katika shehere kama hizi alisamehe wafungwa 3563.
Mwisho.