Wednesday, December 5, 2012

MAWAZIRI NA SEMI ZAO NCHINI

WAZIRI MWAKYEMBE AWAFUKUZA KAZI VIONGOZI TPA


                                                       Dr Mwakyembe


Waziri wa Uchukuzi Dr Harrison Mwakyembe  amewaafukuza kazi  EPHRAIM MGAWE, na Naibu wake Bwana JULIUS MFUKO kufuatia ripoti iliyotolewa na tume maalum ya kuchunguza hali ya uendeshwaji wa bandari hiyo na kuonyesha kuwa watendaji hao wamekosa umakini pamoja na kufanya uzembe uliopitiliza.


Akisoma ripoti hiyo Dokta MWAKYEMBE amesema kuwa Viongozi hao wameshindwa kuonyesha umaridadi wa kuisimamia bandari hiyo, hali iliyopelekea kuisababishia Hasara kubwa Serikali sambamba na kushusha hadhi ya Bandari ya Dar es Salaam, hadi kufikia hatua ya kutajwa kama Bandari isiyoingiza faida yoyote miongoni mwa Bandari 36 za barani Afrka.

Katika Hatua nyingine Dokta MWAKYEMBE ametangaza kuwafukuza kazi Meneja Mkuu wa Bandari hiyo KASSIAN NGAMILO pamoja na Meneja wa kitengo cha Mafuta CAPTAIN TUMAINI MASSAWE, kufuatia kushindwa kusimamia ipasavyo mikataba mbalimbali ya uondoshaji wa mafuta machafu bandari hapo sambamba na uzembe uliopitiliza.

Hata hivyo Dokta MWAKYEMBE amebainisha kuwa Wizara yake haitamvumilia mtendaji yeyote kutoka idara ama taasisi iliyo chini ya Wizara hiyo ambaye utendaji wake utaonekana kulega lega, na kusabaisha Serikali kupata hasara pasipo sababu za Msingi.

Kufukuzwa kwa Viongozi hao ni miongoni mwa utekeleza wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo imeshika nafasi ya Mwisho kwa uingizaji faida katika Bandari 36 za Bara la Afrika hii ni ikiwa ni Ripoti iliyotolewa hivi karibuni.
HABARI HII NI KUTOKA MTANDAO WA www.francisgodwin.blogspot.com

NAIBU WAZIRI ALIYETIKISA RUKWA KESHO KUANZA ZIARA KATAVI KESHO




NAIBU waziri wa Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa nchini, Aggrey Mwanri baada ya kufanya ziara na kuibua mambo mazito ikiwa ni pamoja na kigugumizi ya Manispaa ya Sumbawanga kuwasha umeme katika stendi kuu ya mabasi mjini humo anatarajia kuanza ziara kama hiyo mkoani Katavi ambako atatembelea, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Taarifa zinasema kuwa waziri huyo ambaye amefanya ziara ya siku tisa mkoani Rukwa atafanya ziara mkoani kKatavi katika Halmashauri zote kuanzia Januari 16, 2013 hadi Januari 21, 2013 ambapo atafanya kazi kubwa ya kukagua miradi, kuweka mawe ya msingi katika miradi kuzindua na hatimaye atakuwa anafanya mikutano ya hadhara.

Naibu Waziri Mwanri amekuwa na tabia ya kukagua miradi kwa vitendo ambapo akiwa mjini Sumbawanga aliweza kukagua upana wa barabara kwa kutumia tepu ya kupimia na kukagua uimara wa sakafu na kuta za majengo aliyoakagua kwa kutindua na tindo kwa kutumia tindo na nyundo vitendo ambavyo vimejenga dhana ya uwajibikaji kwa watendaji wa halmashauri na manispaa

Akiwa katika mkoa wa Katavi Mhe. Mwanri atatembelea wilaya mbili za Mlele na Mpanda zinazounda halmashauri nne ambazo ni Halmashauri ya wilaya ya Mlele, halmashauri ya wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo na halmashauri ya mji Mpanda.

Katika blog hii tutajitahidi kukuletea yatakayojiri katika ziara hiyo kwa wakati ili uweze kuelewa nini kimefanyika.

WASIRA: KILIMO KWANZA KUUFIKISHA UCHUMI MIFUKONI MWA WANANCHI

 

                                                              Waziri Wasira

 NA MWANDISHI WETU
UHALISIA wa kukua kwa uchumi hadi mifukoni mwa wananchi walio wengi una matumaini ya kufikiwa kutokana na
utekelezwaji  madhubuti wa kuinua Kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza unayotekelezwa na serikali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera na Uratibu, Steven Wasira alipokuwa akizungumza kwenye
kipindi cha 'Tuongee Asubuhi' cha kituo cha televisheni cha Star Tv, leo, Januari 15, 2013.

Katika kipindi hicho, kilichokuwa na mada ya 'Uhalisia na Kukua kwa Uchumi' pamoja na Wasira wazungumzaji wengine
walikuwa, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo cha SAUTI cha Mwanza, Odas Bilame.

Wasira alisema, kwa sasa wananchi wengi hawaoni uhalisia wanapoambiwa kwamba uchumi wa nchi unakuwa, kwa
sababu, hali ya kukuwa kwa uchumi kwa sasa hakujawagusa waajiriwa katika sekta ya kilimo ambao ndio wengi kiasi
cha asilimia 80.

Alisema, katika kipindi cha kati ya mwaka juzi na mwaka jana uchumi wa Tanzania ulionyesha kuwa umekuwa kwa kati
ya asilimia 6.5 na 6.7, lakini kukua huku kuliwagusa zaidi watumishi waliopo katika sekta nyingine kama za viwanda na
watumishi wa umma.

"Katika hali hii ambayo watumishi wa sekta zote wanategemea lazima wapate chakula na mazao mengine kutoka kwa
wakulima, ambao hawajanufaika vya kutosha na mafanikio ya kukua wa uchumi huu, ni lazima, athari za kutoonekana
ukuaji uchumi katika jamii utakuwepo", alisema, Wasira.

Alisema, kutokana na kutambua kwamba ni lazima sekta ya Kilimo iboreshwe vya kutosha ndipo ukuaji wa uchumi utadhihirika kwa uhakika miongoni mwa wengi, Serikali imeelekeza nguvu zake kuhakikisha mpango wa Kilimo Kwanza unazaa matunda.

Alisema, katika jitihada za kufikia lengo hilo, Serikali imetenga sh. bilioni 300 kwa ajili ya kuwekeza kwenye utafiti katika kilimo, ambapo katika uwekezaji huo, sasa wapo wataalam wengi na maofisa ugani vijijini kwa ajili ya kuwezesha wakulima kufanya kilimo bora na cha kisasa.

Wasira alisema, pia kiwanda cha mbolea cha Minjingu kimejengwa ili kuongeza upatikanaji wa mbolea ili kuhakikisha kwamba kila mkulima anapata mbolea ya kutosha na kuongeza kuwa  pamoja na kiwanda hicho Serikali inao mpango wa kujenga vingine vya mbolea ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa pembejeo hiyo.

Alisema, wakati jitihada zimewekwa kwenye uinuaji sekta ya kilimo, ujenzi na uboreshaji miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara na reli, utafungua milango ya mazao kutoka vijijini kwenda maeneo mbalimbali nchini hata nje ya nchi kwa urahisi, hatua ambayo itachochea kukua kwa kasi zaidi kwa uchumi.

Akielezea historia ya Uchumi wa Tanzania, Wasira alisema, awali hali ya uchumi ilikuwa ikienda vizuri, lakini ilianza kuathiriwa na uhaba wa mafuta miaka uliojitokeza miaka ya 1977 lakini ukaendelea kuathiriwa zaidi na vita vya Kagera, mwaka 1978 na hadi sasa zimeendelea kuwepo changangamoto za kidunia ambapo Tanzania kama moja ya nchi zilizomo haiwezi kuzikwepa.

Kwa upande wake Profesa Lipumba, alikiri kwamba Kilimo Kwanza ni 'muarobaini' wa kukua kwa uchumi wa nchi, lakini akaonya kwamba ni lazima juhudi za makusudi zifanyike kuhakikisha kuwa uhalisia wa kukua wa uchumi ni kuigusa mifuko ya wananchi.

Pamoja na kukiri umuhimu wa mpango wa kilimo kwanza, Profesa Lipumba aliponda kwamba, licha ya mikakati mizuri  kuwepo lakini mingi ipo katika makatarasi tu, haitekelezwi kwa vitendo.

"Sasa kama dhamira ipo, umefika wakati wa watekelezaji kuacha maneno na badala yake kufanya kazi kwa vitendo zaidi", alisema Lipumba.

Kwa upande wa nafasi ya wasomi wanavyoisadifu hali ya kukua kwa uchumi Tanzania, Odax alisema, wasomi wanakubalina kwamba juhudi zikiwekezwa kwenye kilimo uchumi utakuwa.

MAHANGA ATAKA MABADILIKO YA MITAALA ELIMU YA JUU KUKAZANIA HISABATI NA SAYANSI ZAIDI



Dr Makongolo Mahanga, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Tanzania

NAIBU Waziri wa Kazi na Ajira, Dr. Makongoro Mahanga ameshauri vyuo vya elimu ya juu kurekebisha mitaala yao ili kukazania zaidi masomo ya hisibati na sayansi, na pia kuhakikisha kwamba kwenye kila fani au program katika vyuo hivyo, kunakuwepo na masomo ya ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwaandaa wahitimu kujiajiri kama hawatapata kazi za kuajiriwa. Aidha ameshauri  kwamba, kama ilivyofanywa kwa fani ya ualimu, kuwepo na program au shahada mahsusi ya ujasiriamali katika kila chuo cha elimu ya juu.

 Dr. Mahanga ametoa ushauri huo jana mjini Mtwara alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Mtwara, viongozi na wahitimu katika chuo kishiriki cha Stella Maris kilichoko Mtwara na kinachomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Alisema sababu kubwa ya baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu kukosa ajira ni pamoja na vijana hao kutotaka au kuweza kuchukua masomo ya sayansi na hisibati na pia kutotaka kuchukua fani kama ya ualimu ambazo zina fursa za uhakika za ajira. Aidha, alisema sera na mitaala ya elimu haijazingatia sawasawa mahitaji ya soko la ajira. Alisema sababu nyingine ni ukosefu wa nafasi za kujifunza elimu ya ufundi, ujasiriamali na stadi za kazi au kufanya mazoezi ya stadi za kazi ili kupata ujuzi wa aina ya ajira nzuri kwenye soko la ajira. Hivyo kuanzisha masomo au shahada ya ujasiriamali kwenye vyuo vikuu vyote ingeweza kuwa suluhisho la wahitimu wengi kukosa ajira. Alisema kwa sasa kati ya vijana zaidi ya 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka baada ya kumaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu, vijana 240,000 hawapati ajira kabisa na baadhi yao ni wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu.
> >>
> >> Dr. Mahanga, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ya kwanza ya chuo hicho ambacho ni chuo kishiriki cha Chuo Kikuu cha St. Augustine cha Mwanza, aliwataka pia wahitimu wanaokopeshwa na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi kurejesha mikopo hiyo wakishaanza kufanya kazi. Akitoa takwimu za mikopo ya wanafunzi, alisema kwa miaka 18 kuanzia mwaka 1994/95 ambapo mikopo hiyo ilianza kutolewa kwa wanafunzi hadi Juni 2012, Serikali imeshatoa mikopo ya shs. 1.184 trilioni kwa wanafunzi 593,712. Hata hivyo alisema kati ya mikopo ilioiva na kustahili iwe imesharudishwa na wahitimu waliokopa ni asilimia 49% tu imeshalipwa kwa Bodi.

HOTUBA CHINI

HOTUBA YA MHE. DKT. MILTON MAKONGORO MAHANGA (MB), NAIBU WAZIRI WA KAZI NA AJIRA KWENYE MAHAFALI YA KWANZA YA CHUO KIKUU CHA STELLA MARIS MTWARA (STEMMUCO), TANZANIA TAREHE 5 DESEMBA, 2012

    Mhashamu Baba Askofu Mkuu, Norbet Mtega – Mkuu wa Chuo,
  Mhashamu Baba Askofu Gabriel Mmole, Askofu wa Jimbo la Mtwara na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo,
    Mhashamu Baba Askofu John Ndimbo, Askofu wa Jimbo la Mbinga na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo,
    Mhashamu Baba Askofu Bruno Ngonyani, Askofu wa Jimbo la Lindi,
    Mhashamu Baba Askofu Castor Msemwa, Askofu wa Jimbo la Tunduru Masasi,
    Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,
    Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara,
    Waheshimwa Wakuu wa Vyuo na Taasisi za Elimu,
    Mabibi na Mabwana.

Tumsifu Yesu Kristu!

Ni heshima kubwa kwangu binafsi na kwa Serikali kwa ujumla kunipa mwaliko wa kuwa Mgeni Rasmi katika tukio hili la kihistoria, tukio la mahafali ya kwanza ya Chuo hiki Kishiriki cha Stella Maris hapa Mtwara.

Kwa kunialika kushiriki tukio hili, ni ishara wazi inayoonyesha ushirikiano uliopo kati ya Serikali na Taasisi hii katika suala zima la kutoa elimu kwa Watanzania – elimu inayowajengea wahitimu uwezo kiujuzi, kiuelewa, kiutaalam, kimitazamo na kimaamuzi ili waweze kushiriki kwa vitendo kuleta maendeleo halisi ya Taifa letu.

Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana,

Umuhimu wa elimu katika maendeleo ya taifa lolote haliwezi kusisitizwa zaidi.  Nchi zote ambazo zimeendelea kwa haraka duniani zimewekeza katika elimu ya watoto na vijana wake.  Tanzania vile vile imekuwa ikiwekeza kiasi kikubwa cha bajeti yake katika sekta ya elimu na kuipa kipaumbele cha kwanza kila mwaka.  Kwa mfano, katika mwaka 2010/11 Serikali ya Tanzania ilitenga shs. 2.195 trilioni kwa ajili ya sekta ya elimu, hii ikiwa ni asilimia 18.9% ya bajeti nzima ya Serikali.  Kwa mwaka 2011/12, Serikali ilitenga shs. 2.415 trilioni kwa ajili ya sekta ya elimu (asilimia 17.86%).

Kwa kushirikiana na watu binafsi na Taasisi mbalimbali likiwemo Kanisa Katoliki, Serikali inatilia maanani umuhimu wa kutoa elimu bora kwa raia. Serikali imekuwa inafuatilia kwa makini kupitia Tume na vyombo vyake vingine, utoaji wa elimu iliyo bora, elimu yenye kumkomboa mwanadamu na kumpa uwezo wa kuyatawala na kuyaboresha mazingira yake. Kwa misingi hiyo, kwa niaba ya Serikali, natoa shukrani zangu za dhati kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa ushiriki wake wa kutoa elimu bora ya ngazi zote tangu elimu ya awali hadi elimu ya juu. Ushiriki wa Kanisa katoliki na taasisi zingine za kidini na watu binafsi katika fani ya elimu umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya Taifa letu.

Wakati ambapo kufikia mwisho wa mwaka 2010/11 vyuo vya elimu ya juu vilikuwa na jumla ya wanafunzi 139,638, vyuo vya Serikali vilikuwa na wanafunzi 104,129 huku vyuo binafsi vikiwa na wanafunzi 35,509. Hata hivyo vyuo vya elimu ya juu vya Serikali vilikuwa 11 tu kulinganisha na 21 vya binafsi. Hii ina maana kwamba vyuo binafsi vilikuwa vingi (65.6%) kulinganisha na vya Serikali (34.4%) lakini viliweza kudahili wanafunzi asilimia 25.4% tu. Kwa maana hiyo kuna haja ya vyuo binafsi kupanua miundombinu ya vyuo vyake na udahili ili viweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi.

Maaskofu, Mabibi na Mabwana,
Ikijua na kujali umuhimu na mchango wa vyuo binafsi, Serikali, kupitia Tume yake ya Vyuo Vikuu (TCU), mnamo Desemba 2009, iliruhusu Taasisi hii ianze kutoa elimu ya juu kama kituo cha chuo kikuu cha SAUT. Miaka miwili baadaye, yaani Julai, 2011 Serikali iliipandisha hadhi Taasisi hii na kuifanya Chuo Kikuu Kishiriki.

Ikitambua uwezo mdogo wa kiuchumi wa Watanzania, Serikali kupitia Bodi yake ya mikopo imekuwa ikitoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu wenye vigezo vinavyotakiwa. Kwa miaka 11 toka mikopo hii ianze kutolewa mwaka 1994/95 hadi 2004/2005, jumla ya wanafunzi 113,240 waliweza kukopeshwa jumla ya shilingi 51,103,687,000.  Lakini kwa miaka saba ya awamu ya nne ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kutoka mwaka 2005/06 hadi 2011/12, Serikali, kupitia Bodi ya Mikopo iliyoundwa mwaka 2005, ilikopesha wanafunzi 480,472 jumla ya shs. 1,133,386,869,000.

Mabibi na Mabwana,

Kama ilivyoelezwa hapa leo, chuo hiki pia kilifaidika na mikopo hii ambapo asilimia 94% ya wahitimu wake wamewezeshwa kwa njia ya mikopo hiyo. Aidha kupitia Serikali za Mitaa hapa Mtwara-Mikindani, Serikali imetoa ardhi takribani ekari 140 kwa ajili ya maendeleo ya chuo hiki. Haya yote yanaonyesha jinsi Serikali yetu inavyojali watu wake katika masuala ya elimu. Kwa niaba ya Serikali nawaahidi kwamba ushirikiano huu utaendelea kudumishwa.  

Inafurahisha na kutia moyo kuwa Chuo hiki kiliona ni vema kuanza kazi yake Mkoani Mtwara kwa kuandaa walimu wa sekondari. Tunda la kwanza la chuo ni walimu walioandaliwa kutoa elimu ya Sekondari. Elimu hii itachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta maendeleo ya watanzania tukizingatia kuwa zipo shule nyingi za sekondari zenye idadi ndogo ya walimu. Tukianzia na Mikoa ya Kusini, mmejionea wenyewe uhaba wa walimu uliopo. Ninawahimiza wahitimu wa leo wawe tayari kuitumia elimu yao kuchangia kuleta maendeleo ya watanzania.

Mabibi na Mabwana,

Ukosefu wa ajira bado ni tatizo kubwa nchini, hasa kwa vijana. Kati ya vijana wapatao 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka baada ya kumaliza masomo ya msingi, sekondari na vyuo vya juu, ni asilimia kama 5 tu (au vijana 40,000) ndio wanapata ajira kwenye sekta rasmi isiyo ya kilimo.  Waliobaki wanaingia kwenye ajira kwenye sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi (asilimia 35) na sekta isiyo rasmi (aslimia 30), huku asilimia 30 waliobaki (vijana 240,000) wakikosa kazi. Kati ya vijana wanaoingia kwenye soko la ajira na kukosa kazi, wako pia wahitimu wa vyuo vikuu. 

Sababu kubwa ya baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu kukosa ajira ni pamoja na vijana hao kutotaka au kuweza kuchukua masomo ya sayansi na hisibati na pia kutotaka kuchukua fani kama ya ualimu ambazo zina fursa za uhakika za ajira. Aidha, sera na mitaala ya elimu haijazingatia sawasawa mahitaji ya soko la ajira. Na pia kuna ukosefu wa nafasi za kujifunza elimu ya ufundi, ujasiriamali na stadi za kazi au kufanya mazoezi ya stadi za kazi ili kupata ujuzi wa aina ya ajira nzuri kwenye soko la ajira.

Ningependa kutoa wito kwa vyuo vya elimu ya juu kurekebisha kasoro hizi kwa kutilia maanani masomo ya hisibati na sayansi, na pia kuhakikisha kwamba kwenye kila fani au program katika vyuo vikuu vyote, kunakuwepo na masomo ya ujasiriamali na stadi za maisha ili kuwaandaa wahitimu kujiajiri kama hawatapata kazi za kuajiriwa. Aidha ningeshauri kwamba, kama ilivyofanywa kwa fani ya ualimu, kuwepo na program au shahada mahsusi ya ujasiriamali (Bachalor of Business Administration/Management in Entreprenuership) katika kila chuo cha elimu ya juu. Nimeona kwamba ingawa leo wahitimu wa chuo hiki ni wa fani ya ualimu mlioanza nayo, lakini kwa sasa mmeshaanzisha program za shahada zingine hapa chuoni.  Angalieni pia uwezekano wa kuanzisha shahada ya ujasiriamali katika mipango yenu ya baadaye.

Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana,

Kabla sijamaliza hotuba yangu, nitoe wito kwa wenzetu 1,100 wanaohitimu leo katika chuo hiki cha Stella Maris kama ifuatavyo:-
•    Uadilifu kazini: Wahitimu mmefundishwa sio tu kuwa walimu bali walimu-walezi. Serikali inawatazamia kuwa mifano bora kazini kwa kuyaishi maadili ya kazi yenu. Epukeni upendeleo, rushwa na unyanyasaji. Fanyeni kazi kwa haki na ueledi wa hali ya juu.

•    Utayari wa kurudisha pesa ya mikopo: Mmesoma kwa pesa ya mikopo. Kumbukeni kulipa madeni ili wakopeshwe wengine. Tatizo la wahitimu wa vyuo vikuu kurudisha mikopo waliokopeshwa bado ni kubwa. Kwa mfano, kufikia Juni 2012, madeni ya wahitimu wa vyuo vya juu yaliyokuwa yameiva yalikuwa Tshs. bilioni 160.7 na kati yake, shs. 39.5 bilioni zilitakiwa ziwe zimeshakusanywa kutoka kwa waliokopa, lakini ni asilimia 49% tu kati ya hizo zilikuwa zimekusanywa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi

•    Maslahi Binafsi: Katika kazi zenu za ualimu lazima mtangulize maslahi ya wengi na wala si maslahi binafasi

•    Migomo na Vurugu: Ni muhimu mkaepuka migomo na vurugu kazini. Pale migogoro inapotokea, ni lazima mtafute suluhisho za migogoro kwa mazungumzo na pande zote zinazohusika.

•    Utayari wa kufanya kazi popote bila kubagua maeneo: Fanyeni kazi popote nchini bila kupendelea mijini au maeneo ya nyumbani kwenu. Katika risala ya chuo mmeeleza jinsi imekuwa vigumu wahitimu kufanya kazi kwenye maeneo fulani ya nchi, kwa mfano katika mikoa hii ya kusini ikiwemo Mtwara na Lindi. Kwanza sitegemei wahitimu wa chuo hiki hapa Mtwara baada ya kuzoea mazingira ya mkoa huu na ya jirani walipokuwa wakisoma, wakashindwa kufanya kazi huku baada ya kumaliza masomo yao. Lakini pia nyie wenyewe ni mashahidi kwamba Serikali imekuwa ikichukua hatua za makusudi kuboresha hali ya maisha na miundombinu ya mikoa iliyokuwa inaonekana iko nyuma kimaendeleo kama Mtwara ili wananchi wa mikoa hii na watanzania wengine wanaopangwa kufanya kazi kwenye mikoa hii wasione tofauti kubwa na mikoa mingine.

Kwa upande wa Mtwara na mikoa mingine ya kusini, ukiacha uboreshaji mkubwa wa miundombinu ya barabara, umeme na bandari, kumekuwepo vile vile uwekezaji kwenye miradi ya kiuchumi kama utafiti na uchimbaji wa gesi asilia, utafiti wa mafuta na viwanda kadhaa kama vya saruji na mbolea vinavyotarajiwa kuanza kujengwa karibuni. Yote haya yamefanya mikoa hii ianze kuwavutia hata wananchi wengine kupenda kuishi, kufanya kazi, kuwekeza na kufanya biashara katika mikoa hii.

Hapa ningependa kuwapongeza Baraza la Maaskofu Katoliki kwa kuanzisha chuo hiki hapa Mtwara na kukipa jina la Stella Maris linaloendana na maendeleo yanayoendelea kuwepo katika mkoa huu wa Mtwara. Jina hili nimeambiwa maana yake ikitafsiriwa kwa kilatini ni “Nyota ya Bahari”.  Jina hili linabeba dhana nzima ya uwepo wa chuo hiki mkoani Mtwara, kwa maana ya kuwa chimbuko la mwanga na matumaini katika misukosuko ya kimaisha, kielimu, kitaaluma na  kiuchumi. Jina hilo pia linaendana na maendeleo na uwekezaji unaoanza kuonekana hapa mkoani Mtwara kama nilivyoeleza hapo juu.
  
Waheshimiwa Maaskofu, Mabibi na Mabwana

Kwa upande wa Serikali ningependa kuahidi yafuatayo:-
   Ajira kwa walimu: Kwa kuzingatia uhitaji uliopo, Serikali inawaahidi wahitimu wa chuo hiki kupewa ajira katika fani ya ualimu, kama ambavyo imekuwa ikifanya kila mwaka kwa wahitimu wa fani hii. Kwa mfano katika mwaka 2011, Serikali ilitoa ajira 11,629 kwa walimu wa shule za sekondari kote nchini na kufanya shule hizo kuwa na walimu 52,146 mwaka 2011 kulinganisha na walimu 40,516 waliokuwepo mwaka 2010 katika shule zote za sekondari za Serikali na binafsi nchini.
  Sera nzuri kwa kazi ya ualimu: Serikali inaahidi kuendelea kuweka sera nzuri kwa kazi ya ualimu ili kuondoa kero za walimu zinazowapelekea kugoma na kuona kwamba taaluma yao haithaminiwi na Serikali.

Mwisho kabisa, niwaombe wananchi na wakazi wa Mtwara, mpokee taasisi zilizo Mtwara kama baraka na wadau wa kuleta maendeleo. Kwa misingi hiyo wapokeeni wanafunzi wasomao vyuoni Mtwara kama watoto wenu. Wapokeeni kama wapangaji kwenye nyumba zenu kwa gharama za kiungwana bila kuwadai pesa nyingi kupita uwezo wao. Wenye vyombo vya usafiri tozeni gharama za haki.

Nimalizie kwa kuwashukuru tena Baraza la Maaskofu Katoliki na uongozi wa chuo kwa kunialika kujumuika nanyi katika mahafali ya kwanza ya chuo hiki kikuu kishiriki cha Stella Maris, na niwatakie kila la heri kwenye kazi zao wahitimu wetu wa leo.


ASANTENI KWA KUNISIKILIZA