Monday, March 25, 2013

NMB YAKABIDHI DAWATI KAKESE MPANDA






















BENKI ya NMB tawi la Mpanda katika mkoa wa Katavi imekabidhi madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 9.5 katika shule ya msingi Kakese Mbugani iliyoko mjini Mpanda mkoani humo

Akizungumza katika makabidhiano hayo mkuu wa kitengo cha wajasiliamali wadogo na wa kati wa benki hiyo, Filbert Mponzi alisema benki ya NMB imekuwa ikitoa msaada wa madawati katika shule nyingi hapa nchini kutokana na uhitaji mkubwa uliopo wa madawati na baadhi ya mahitaji katika sekta ya elimu nchini

Alisema msaada huo ni sehemu ya azimio la benki hiyo kuwa karibu na jamii kwa kupitia sekta ya elimu ambapo hivi sasa imeanzisha huduma ya elimu ya fedha kwa wanafunzi mashuleni ili kuwajenga wanafunzi kukua katika mzingira yenye taaluma ya mambo ya fedha na hatimae kujenga kizazi chenye uelewa wa masuala ya fedha

Akipokea msaada huo kutoka NMB mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Mpanda, Joseph Mchina alisema shule hiyo inahitaji madawati 345 na yaliyopo shuleni hapo ni madawati 54 mapungufu ni madawati 291 hivyo baada ya NMB kukabidhi madawati 100 upungufu umebaki madawati 191.

Mkurugenzi huyo wa Mji aliishukuru benki ya NMB kwa msaada huo kwani umetolewa katika sekta inayohitaji sana msaada huo na hivyo alitoa wito kwa taasisi zingine za kibenki na zisizo za kibenki kutoa msaada wa madawati na vitu vingine katika shule zilizopo hapa nchini ili kupunguza baadhi ya mahitaji ya shule

Mchina alisema katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa madawati ofisi yake imziagiza shule kutumia asilimia ishirini ya fedha za uendeshaji kutengeneza madawati ambapo katika kipindi cha miezi sita shule ya msingi Kakese mbugani itakuwa imetengeneza madawati 100 hivyo kuwataka wazazi kupitia kamati ya shule nao kuwajibika kuchangia mchango wa madawati shuleni hapo ili kukamilisha pengo la madawati tisini na moja lililobakia

Afisa elimu wa halmashauri ya Mji wa Mpanda Vicent Kayombo alisema halmashauri yake inahitaji madawati 6313 na yaliyopo ni madawati 3213 hivyo kuwepo kwa upungufu wa madawati 3100 ili shule zote ziwe na madawati katika halmashauri yake ambapo alisema mikakati ya kuondoa kero hiyo ni kuwa kila shule itumie mgao wa uendeshaji shuleni pamoja na pesa za ukarafati asilimia ishirini kutengeneza madawati 

Kayombo alisema katika mikakati waliyoipanga katika halmashauri yake wanategemea kuondoa tatizo la uhaba wa madawati katika halmashauri yake kabla ya mwezi julai mwaka huu.