Sunday, March 24, 2013

NMB YAKABIDHI DAWATI MIA SHULENI KAKESE



HALMASHAURI ya mji wa Mpanda imeishukuru benki ya NMB Tawi la Mpanda kwa kukabidhi madawati mia moja katika shule ya Msingi Kakese Mbugani yenye thamani ya shilingi milioni tisa na nusu na kupunguza kero ya uhaba wa madawati shuleni hapo

Akizungumza mara baada ya kupokea madawati hayo kutoka kwa benki hiyo Mkurugenzi wa mji wa Mpanda Joseph Mchina alisema mchango wa madawati mia kwa ajili ya shule ya Msingi Kakese mbugani kunasaidia juhudi za serikali za kuondoa kero ya uhaba wa madawati hapa nchini

Alisema katika halmashauri yake kuna uhitaji wa madawati 6313 wakati yaliyopo ni madawati 3213 na hivyo kuwa na upungufu wa madawati 3100 na kutokana na msaada wa benki wa madawati mia upungufu unabaki dawati 3000

Alitoa wito kwa taasisi zingine kurejesha sehemu fa faida yake kwa kusaidia jamii katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya wanawake na watoto

Akizungumza katika hafla hiyo mkuu wa kitengo cha wajasiliamali wadogo na wa kati wa NMB, Filbert Mponzi alisema hivi sasa benki yake imeanzisha utaratibu wa kutoa huduma ya elimu ya fedha mashuleni ili kuwajenga wanafunzi kukua katika elimu ya fedha

“Tunataka kuhakikisha tunajenga kizazi chenye uelewa na taaluma ya fedha kutoka shuleni hadi katik jamii’’
alisema afisa huyo wa benki