TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mei 19, 2013 Chama Cha Mapinduzi kilifanya kikao
cha siku moja na wabunge wanaotokana na CCM, kikao hicho kilifanyika mjini Dodoma ambapo pamoja na
viongozi wengine wa juu wa CCM kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa
CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la wabunge wa
CCM na viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambaye pia ni
Rais na mtekelezaji mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kubadilishana uzoefu wa
namna ilani ilivyotekelezwa hasa kwenye majimbo kwa kipindi cha nusu ya muhula
wa miaka mitano. Baada ya kubadilishana mawazo uliwekwa mwelekeo wa namna bora
ya kutekeleza ilani na ahadi mbalimbali kwa kipindi kilichobaki.
Kwahiyo kwa kifupi lengo la kikao hicho
ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa ilani majimboni na kuangalia namna bora
ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi kwa kipindi kilichobaki cha utekelezaji
wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa 2010/2015, lengo likiwa kuhakikisha ilani na
ahadi za CCM na wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
Hata hivyo baada ya semina hiyo baadhi ya
vyombo vya habari vimenukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya
Kikwete kuwa ameruhusu wanaokusudia kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa 2015
kufanya kampeni.
CCM imesikitishwa na nukuu hiyo ya kupotosha
ukweli wa kilichojadiliwa na hivyo tumelazimika kutoa ukweli wa kilichojiri na
kujadiliwa. Ni kweli kuwa mjadala juu ya watu mbalimbali wanaotajwa au
wanaojitaja kuwa na nia ya kugombea nafasi mbalimbali hasa udiwani, ubunge na
Urais ulikuwepo na ulikuwa mkali.
Hata hivyo hitimisho la kikao na majumuisho
ya Mwenyekiti wa CCM Taifa lilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirika hizo na
uvunjifu huu wa makusudi wa kanuni za Chama chetu ambazo kimsingi pirika hizi
zinakigawa Chama na kuvuruga mshikamano na umoja ndani ya Chama.
Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi ya vyombo
vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea kuna kikundi cha watu
wanamgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka anapungukiwa na sifa, hivyo
wanajaribu kumuongezea sifa kwa kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwaapa baadhi ya
waandishi, uhuni huo haukubaliki.
CCM ina kanuni na taratibu zake
zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya shughuli zake mbalimbali zikiwemo za
mchakato wa kuwapata wagombea wake katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi
taifa.
Kanuni hizo ni pamoja na kanuni za Uteuzi wa
wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na
Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012.
Katika Kanuni za Uchaguzi wa CCM Toleo la
2012 kanuni za jumla Ibara ya 33 inazungumzia Miiko ya kuzingatiwa wakati wa
shughuli za uteuzi na uchaguzi. nanukuu“ Maadili na nidhamu ya chama katika
kusimamia na kutekeleza shughuli za uchaguzi wa chama lazima kuzingatiwa na
wale wote wanaohusika. Hivyo yawapasa kuelewa na kutambua kuwa;-
(1). “….wanachama
wenye nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote kabla ya
majina yao kuteuliwa
na kikao kinachohusika”.
(4). “Ni mwiko kwa
kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya
chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini chini kinyume na ratiba
ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa”.
Ibara hiyo ya 33 kifungu kidogo cha 1 na 4
vinaweka wazi msimamo wa kikanuni wa Chama. Hivyo basi kwa mujibu wa kanuni za
Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari,
2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012 na kwa mujibu wa maagizo
yaliyotolewa na kupokelewa kwenye kikao cha Mwenyekiti wa CCM Taifa na wabunge
wa CCM mjini Dodoma tarehe 19/05/2013;
Ni marufuku kwa mwanachama yeyote wa CCM
anayetaka kuomba CCM impe nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa dola kujipitishapitisha
na kuita wapiga kura na kukutana nao kinyume na kanuni za Chama. Hatua kali
zitachukuliwa kwa mwana CCM yeyote atakaye kiuka agizo hili.
Lakini pia ni marufuku kwa viongozi na
watendaji wa Chama kujihusisha na kuwakusanyia wapiga kura watu hao wenye nia
ya kugombea kupitia CCM kwenye uchaguzi wa dola. Hatua kali zitachukuliwa dhidi
ya viongozi na watendaji wote watakao kiuka agizo hili la Chama.
Tunawataka wote wenye nia, viongozi na
watendaji wa CCM kuzingatia agizo hili, ili tusije laumiana mbele ya safari.
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
Kimesema
sheria kanuni na taratibu zinazokiongoza Chama katika kupata wagombea
wake ziko palepale na kwamba hakitamvumilia yeyote atakayebainika
kuzikiuka.
Onyo hilo lilitolewa jana Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, wakati akiongea na
waandishi wa habari kuhususu mkutano kati ya CCM na wabunge wake
uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.
"Viko vyombo vya
habari ambavyo kwa makusudi vimepotosha ukweli kuhusu tulichoafikiana
katika kikao kati ya CCM na wabunge wake. Si Mwenyekiti wa taifa wala
Chama kilichoruhusu wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali
kujipitishapitisha kwa wananchi.
"Nasisitiza nukuu hiyo ya
baadhi ya vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli.
Inaelekea kuna kikundi cha watu wenye mgombea wao wa kuchonga ambaye
bila shaka anapungukiwa sifa, hivyo wanajaribu kumuongezea sifa kwa
kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwapa baadhi ya waandishi wa habari.
Uhuni huo haukubaliki," alisema Nape.
Kwa mujibu wa Nape,
licha ya ajenda kuhusu wana-CCM wenye nia ya kuwania nafasi mbalimbali
ikiwemo udiwani, ubunge na urais kujadiliwa kwa kina katika kikao hicho,
hitimisho na majumuisho ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ilikuwa
ni kukemea kwa nguvu zote pirikapirika hizo ambazo ni uvunjifu wa
makusudi wa kanuni za Chama.Alisema kimsingi pirikapirika zinazofanywa
na baadhi ya makada zinaweza kukigawa Chama na kuvuruga mshikamano na
umoja uliopo ndani ya CCM.
Nape alisema CCM ina kanuni na
taratibu zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya shughuli zake
mbalimbali zikiwemo za mchakato wa kuwapata wagombea wake katika ngazi
mbalimbali kuanzia shina hadi taifa. Kanuni hizo ni pamoja na za uteuzi
wa wagombea wa Chama kuingia kwenye vyombo vya dola toleo la Februari,
mwaka 2010 na kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la mwaka 2012.
“Ni
mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo
rasmi ndani ya chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini
chini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa”
alisema.Katibu huyo alisema iwapo mwanachama yeyote atakiuka kwa
makusudi na kuvunja taratibu hizo, Chama kitamwajibisha bila ya kumuonea
haya na kwamba itakapofikia hapo asilaumiwe yeyote kwa kuwa ndivyo
taratibu zinavyoagiza.
Akizungumzia malengo ya kikao hicho,
alisema kililenga kutathimini utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM
majimboni na kuangalia namna bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi
kwa sehemu iliyobaki ya utekelezaji wake katika kipindi cha mwaka
2010/2015, ili kuhakikisha ahadi za Chama na wagombea wake zinatekelezwa
kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya magazeti (Uhuru halimo) katika
matoleo yao ya juzi, yalimnukuu Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete, akiwaruhusu wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao
mwaka 2015 kuendelea na mchakato.
Magazeti hayo yalidai kuwa Rais aliruhusu hilo kutendeka huku
akiwatahadharisha
watakaokuwa tayari kufanya hivyo kuendesha kampeni zao kwa ustaarabu
bila kuibua chuki na kujenga makundi kwa kuwa ni hatari kwa uhai wa
Chama.