May 17, 2013
PAZIA LIGI KUU YA VODACOM KUFUNGWA JUMAMOSI TFF LEO
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania
Bara msimu huu (2012/2013) inafikia tamati kesho (Mei 18 mwaka huu) kwa timu
zote 14 kupambana katika viwanja saba tofauti.
Mechi zote zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Ni
jukumu la kamishna wa mechi husika kuhakikisha mchezo unaanza katika muda
uliopangwa, vinginevyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za
Ligi Kuu ya Vodacom toleo la 2012.
Yanga ambayo tayari imeshatwaa ubingwa itakuwa mgeni wa
Simba katika mechi namba 180 itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo
mwamuzi atakuwa Martin Saanya kutoka Morogoro na Kamishna ni Emmanuel Kavenga wa
Mbeya.
Mgambo Shooting vs African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga. Mwamuzi ni Amon Paul wa Mara wakati Kamishna ni Ally Mkomwa kutoka
Pwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam. Mwamuzi
ni Israel Mujuni wa Dar es Salaam wakati Kamishna ni Salum Kikwamba kutoka
Kilimanjaro).
Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Mwamuzi ni Ibrahim Kidiwa wa Tanga wakati Kamishna ni John Kiteve kutoka Iringa), Oljoro JKT vs Azam (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha. Mwamuzi ni Athuman Lazi wa Morogoro wakati Kamishna ni Juma Mgunda kutoka Tanga).
Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro utatumika kwa mechi
kati ya Polisi Morogoro na Coastal Union ya Tanga ambapo Mwamuzi atakuwa Said
Ndege wa Dar es Salaam wakati Kamishna ni Hakim Byemba kutoka Dodoma. Toto
Africans itacheza na Ruvu Shooting katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
ambapo mwamuzi ni Geoffrey Tumaini kutoka Dar es Salaam na Kamishna ni Josephat
Magazi wa Singida.
MECHI ZA MARUDIANO RCL WIKIENDI HII
Mechi za marudiano za raundi ya kwanza ya Ligi ya
Mabingwa wa Mikoa (RCL) zinachezwa wikiendi hii katika viwanja kumi tofauti
wakati mechi ya Flamingo ya Arusha na Machava FC ya Kilimanjaro yenyewe
itachezwa Jumatatu (Mei 20 mwaka huu).
Uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa Jumatatu ni kutokana na
Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid kutumika kwa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) kesho wakati Jumapili utatumika kwa shughuli nyingine za kijamii kwa
mujibu wa wamiliki wa uwanja huo (CCM Mkoa wa Arusha).
Mechi nyingine zitachezwa keshokutwa (Jumapili) ambapo
Abajalo watakuwa wenyeji wa Red Coast kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar
es Salaam. Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara utatumika kwa mechi kati ya
wenyeji Coast United na Kariakoo ya Lindi.
African Sports ya Tanga itaoneshana kazi na Techfort ya
Ifakara mkoani Morogoro katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani. Nayo
Simiyu United ya Simiyu itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja
wa Namfua, mjini Singida.
Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ndiyo utakaotumika
kuzikutanisha timu za Polisi Jamii Bunda kutoka Mara na wenyeji UDC wakati
Biharamulo FC ya Kagera na Polisi SC ya Geita zitaumana kwenye Uwanja wa Kaitaba
mjini Bukoba.
Milambo FC ya Tabora itakuwa mwenyeji wa Saigon FC ya
Kigoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora huku Mbinga United ya
Ruvuma ikiikaribisha Njombe Mji ya Njombe kwenye Uwanja wa Majimaji mjini
Songea.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa utatumika
kwa mechi kati ya wenyeji 841 KJ dhidi ya Kimondo SC kutoka Mbeya. Nazo Rukwa
United na Katavi Warriors zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini
Sumbawanga.
Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya pili zitacheza mechi
zao za kwanza kati ya Mei 25 na 26 mwaka huu wakati mechi za marudiano ni kati
ya Juni 1 na 2 mwaka huu.
UTARATIBU WA SAFARI MECHI YA TAIFA STARS v
MOROCCO
Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) litasaidia upatikanaji wa visa kwa waandishi wa habari
na Watanzania wengine wanaotaka kwenda Morocco kushuhudia mechi kati ya Taifa
Stars na Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech,
Morocco.
Kwa ambao wangependa kupata visa kupitia TFF wanatakiwa
kuwasilisha pasipoti zao, ada ya visa ambayo ni dola 50 za Marekani pamoja na
picha mbili zenye kivuli (background) ya rangi nyeupe kabla ya saa 6 kamili Mei
20 mwaka huu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)