Friday, May 17, 2013

WAIOMBA HALMASHAURI KUGAWA KATA




WAKAZI wa kata za Nsemulwa na Kakese wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wameiomba Halmashauri ya mji wa Mpanda kuzigawa kata hizo ili kuboresha upatikanaji wa huduma na kurahisisha utendaji kwa watumishi ngazi ya kata 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kata za Nsemulwa na Kakese zilizoko katika Halmashauri ya Mji Mpanda baadhi ya wakazi hao walisema kata zao zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya ukubwa wa eneo na idadi kubwa ya watu.







Katika kata ya Kakese wakazi wa kata hiyo walidai kuwa kata hiyo ina eneo kubwa lenye idadi kubwa ya watu kuliko kata zote kwenye Halmashauri ya mji wa Mpanda na kulalamikia jiografia ya kata hiyo kuwa ni ngumu kwani kuna baadhi ya vijiji havijaunganishwa kwa barabara na makao makuu ya kata hiyo

Walisema kijiji cha Mwamkulu kiko umbali wa kilometa kumi kutoka makao makuu ya kata hiyo ingawa kijiji hicho kimo katika kata ya Kakese lakini unapotaka kufika katika kijiji hicho kwa gari kutoka Mbugani ilipo ofisi ya kata unatakiwa kutembea zaidi ya kilomita arobaini kwa kuzunguka Mpanda mjini

Uwepo wa mbuga inayotumika kwa kilimo cha mpunga inayotenganisha kijiji cha Mbugani na Mwamkulu kunachangia ukosefu wa barabara ya kupita kwa magari kutokana na tope lililopo mbugani na hivyo kulazimika kutumiwa kwa mitambo mikubwa ya kulima barabara ya kuunganisha makao makuu ya kata ya kakese katika kijiji cha Mbugani na kijiji cha Mwamkulu

Baadhi ya Wakazi wa kata ya Nsemulwa walisema kuwa msongamano wa makazi unachangiwa na wingi mkubwa wa watu ambapo kata hiyo ina jiografia pana zaidi kuliko kata zingine za mjini Mpanda

Walisema inawawia vigumu kupata huduma katika ofisi ya kata kutokana na afisa mtendaji aliyepo kuzidiwa na mahitaji ya huduma yake kwani matatizo ni mengi kutokana na wingi wa watu uliopo katika kata yao

Akizungumza ofisini kwake, mchumi wa Halmashauri ya mji Mpanda, Fredinand Filimbi alisema ni kweli kata hizo zina idadi kubwa ya wakazi kuliko kata zingine ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa eneo kubwa kijiografia linalochangia uwepo wa changamoto za maeneo hayo

Alisema katika halmashauri yake juhudi za makusudi zimeanza kuchukuliwa katika kuhakikisha wakazi wa kata za Kakese na Nsemulwa changamoto zinazowakabili zinashughulikiwa kwa uzito mkubwa na kutoa huduma bora kwa wakazi wake 

Alisema mgawanyo wa huduma za kijamii umekuwa ukitolewa kwa kuzingatia idadi ya watu ingawa changamoto bado ni kubwa kwa kata ya Nsemulwa na kakese ambako pia ndiyo maeneo yenye changamoto nyingi zaidi kutokana na ukuaji wa kasi wa maeneo yao na kudai ongezeko la mahitaji ya huduma za kijamii kama vile shule, zahanati, maji na pembejeo

Alisema kata ya Kakese mara baada ya sensa ya watu na makazi ya 2012 imebainika kuwepo kwa watu 21,360 na kata ya Nsemulwa ina wakazi 17,166 ambapo halmashauri ya Mji Mpanda ina jumla ya wakazi 102,900 wanaume 50,437 na wanawake 52,463.

Alisema kuhusu kuzigawa kata hizo na kuunda kata zingine inawezekana isipokuwa taratibu zinaanzia katika ngazi ya mitaa, kata na wilaya na kuwa mchakato wa mgawanyo huo unaweza kufanyika wakati wa  kipindi cha uchaguzi mkuu wa 2015




WANNE MBARONI KWA MAUAJI YA MCHUNGAJI 

KIJANA  mmoja ameuwawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na watu
wasiojulikana alipokuwa akichunga ng’ombe wa baba yake saa saba mchana
katika kijiji cha Mtakumbuka kata ya Kapalala wilaya ya Mlele mkoani
Katavi.

Marehemu alitajwa kwa jina la Mahela Nkonya Dotto (15) aliyekuwa
akichunga ng’ombe wa mzazi wake Mei 6, 2013 aliondoka nyumbani kwao
majira ya saa nne kwenda kuchunga  ng’ombe wa mzazi wake aliyetajwa
kwa jina la Nkonya Dotto Maduka (40) ambapo alivamiwa na watu
wasiojulikana na kumpiga kichwani kwa kutumia kitu kizito na kufariki
dunia papo hapo

Ilielezwa kuwa marehemu hakuweza kurejea nyumbani siku hiyo hadi kesho
yake Mei 7, 2013 ndipo mwili wake ulikutwa kichakani ukiwa na jeraha
kubwa kichwani

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Katavi Dhahiri Kidavashari
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa kufuatia tukio
hilo watu wanne walikamatwa na wanahojiwa na polisi kwa upelelezi ili
kuweza kubaini wauaji wa kijana huyo

Licha ya kuwashukuru wananchi walioweza kutoa taarifa sahihi na kwa
wakti zilizofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa aliwataja waliokamatwa
kwa tuhuma za mauaji kuwa ni ndugu Mashaka Benedicto (21) mkazi wa
kijiji cha Mtakumbuka, Benedicto Sanane (55) mkazi wa kijiji cha
Mtakumbuka, Richard Benedicto (22) mkazi wa kijiji cha Mtakumbuka na
Rogati Kasala (32) mkazi wa Nsemulwa mjini Mpanda

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi alisema watuhumiwa wote wanaendekea
kuhojiwa na askari wa upelelezi ambapo watuhumiwa watafikishwa
mahakamani mara upelelezi utakapokamilika