May 17, 2013
PAZIA LIGI KUU YA VODACOM KUFUNGWA JUMAMOSI TFF LEO
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania
Bara msimu huu (2012/2013) inafikia tamati kesho (Mei 18 mwaka huu) kwa timu
zote 14 kupambana katika viwanja saba tofauti.
Mechi zote zitachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni. Ni
jukumu la kamishna wa mechi husika kuhakikisha mchezo unaanza katika muda
uliopangwa, vinginevyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa Kanuni za
Ligi Kuu ya Vodacom toleo la 2012.
Yanga ambayo tayari imeshatwaa ubingwa itakuwa mgeni wa
Simba katika mechi namba 180 itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo
mwamuzi atakuwa Martin Saanya kutoka Morogoro na Kamishna ni Emmanuel Kavenga wa
Mbeya.
Mgambo Shooting vs African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga. Mwamuzi ni Amon Paul wa Mara wakati Kamishna ni Ally Mkomwa kutoka
Pwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam. Mwamuzi
ni Israel Mujuni wa Dar es Salaam wakati Kamishna ni Salum Kikwamba kutoka
Kilimanjaro).
Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Mwamuzi ni Ibrahim Kidiwa wa Tanga wakati Kamishna ni John Kiteve kutoka Iringa), Oljoro JKT vs Azam (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha. Mwamuzi ni Athuman Lazi wa Morogoro wakati Kamishna ni Juma Mgunda kutoka Tanga).
Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro utatumika kwa mechi
kati ya Polisi Morogoro na Coastal Union ya Tanga ambapo Mwamuzi atakuwa Said
Ndege wa Dar es Salaam wakati Kamishna ni Hakim Byemba kutoka Dodoma. Toto
Africans itacheza na Ruvu Shooting katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
ambapo mwamuzi ni Geoffrey Tumaini kutoka Dar es Salaam na Kamishna ni Josephat
Magazi wa Singida.
MECHI ZA MARUDIANO RCL WIKIENDI HII
Mechi za marudiano za raundi ya kwanza ya Ligi ya
Mabingwa wa Mikoa (RCL) zinachezwa wikiendi hii katika viwanja kumi tofauti
wakati mechi ya Flamingo ya Arusha na Machava FC ya Kilimanjaro yenyewe
itachezwa Jumatatu (Mei 20 mwaka huu).
Uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa Jumatatu ni kutokana na
Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid kutumika kwa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom
(VPL) kesho wakati Jumapili utatumika kwa shughuli nyingine za kijamii kwa
mujibu wa wamiliki wa uwanja huo (CCM Mkoa wa Arusha).
Mechi nyingine zitachezwa keshokutwa (Jumapili) ambapo
Abajalo watakuwa wenyeji wa Red Coast kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar
es Salaam. Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara utatumika kwa mechi kati ya
wenyeji Coast United na Kariakoo ya Lindi.
African Sports ya Tanga itaoneshana kazi na Techfort ya
Ifakara mkoani Morogoro katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani. Nayo
Simiyu United ya Simiyu itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja
wa Namfua, mjini Singida.
Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ndiyo utakaotumika
kuzikutanisha timu za Polisi Jamii Bunda kutoka Mara na wenyeji UDC wakati
Biharamulo FC ya Kagera na Polisi SC ya Geita zitaumana kwenye Uwanja wa Kaitaba
mjini Bukoba.
Milambo FC ya Tabora itakuwa mwenyeji wa Saigon FC ya
Kigoma kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora huku Mbinga United ya
Ruvuma ikiikaribisha Njombe Mji ya Njombe kwenye Uwanja wa Majimaji mjini
Songea.
Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa utatumika
kwa mechi kati ya wenyeji 841 KJ dhidi ya Kimondo SC kutoka Mbeya. Nazo Rukwa
United na Katavi Warriors zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini
Sumbawanga.
Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya pili zitacheza mechi
zao za kwanza kati ya Mei 25 na 26 mwaka huu wakati mechi za marudiano ni kati
ya Juni 1 na 2 mwaka huu.
UTARATIBU WA SAFARI MECHI YA TAIFA STARS v
MOROCCO
Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) litasaidia upatikanaji wa visa kwa waandishi wa habari
na Watanzania wengine wanaotaka kwenda Morocco kushuhudia mechi kati ya Taifa
Stars na Morocco itakayochezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech,
Morocco.
Kwa ambao wangependa kupata visa kupitia TFF wanatakiwa
kuwasilisha pasipoti zao, ada ya visa ambayo ni dola 50 za Marekani pamoja na
picha mbili zenye kivuli (background) ya rangi nyeupe kabla ya saa 6 kamili Mei
20 mwaka huu.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
MAMA TUNU PINDA AWAASA MAKATIBU MUHTASI WAZINGATIE MAADILI YA KAZI YAO
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amewataka Makatibu Muhtasi kuzingatia maadili ya taaluma yao ya uhazili ili kuongeza ufanisi wa
majukumu ya kazi zao.
Ametoa wito huo jana Mei 16, 2013 wakati akifungua Kongamano
la Tatu la Makatibu Muhtasi (Tanzania Personal Secretaries Association –
TAPSEA) kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa jijini Arusha (AICC).
Kongamano
hilo la siku mbili, limehudhuriwa na Makatibu Muhtasi zaidi ya 1,500
kutoka mikoa yote nchini, na baadhi ya wawezeshaji kutoka Kenya, Uganda
na Rwanda.
Mama Pinda alisema umuhimu wa taaluma ya uhazili katika tasisi ni mkubwa sana na siyo kitu cha kubeza hata kidogo
“Umuhimu
wa taaluma ya uhazili katika taasisi tunazofanyia kazi unatokana na
nafasi kubwa ya makatibu muhtasi kama wasimamizi wa ofisi na wasaidizi
wa watendaji wakuu. Nafasi yenu inawapa fursa ya kuandaa na kutunza
nyaraka mbalimbali za kiofisi zinazohusu menejimenti ya taasisi hizo.
Niwaombe makatibu muhtasi wote mzingatie maadili ya kazi ya uhazili
katika kutekeleza majukumu yenu,” alisisitiza.
Aliwataka
waongeze jitihada za kukiimarisha Chama chao ili hatimaye TAPSEA iweze
kuenea Mikoa yote na kuwa Chombo kitakachosimamia miiko na maadili ya
fani ya Uhazili kama zilivyo taaluma zingine nchini.
Alisema
majukumu ya makatibu muhtasi siyo kupiga chapa pekee na kuongeza
kwamba, kama chama cha kitaaluma, TAPSEA lazima iendeleze jitihada za
kubadili mtazamo huo ili jamii iweze kutambua umuhimu wa nafasi ya
makatibu muhtasi katika taasisi mbalimbali za umma na za sekta binafsi.
“Hata
hivyo, napenda ieleweke kwamba kazi ya kuleta mabadiliko ya kimtazamo
inaanzia kwa katibu muhtasi mwenyewe. Nawashauri wanachama wote wa
TAPSEA wawe mstari wa mbele katika kubadilika kifikra na kujiendeleza
kila wakati ili kujijengea uwezo wa kuzikabili ipasavyo changamoto za
taaluma ya uhazili katika mazingira ya sasa,” alisema.
Mama
Tunu Pinda alisema kuwekeza katika teknolojia ni jambo muhimu lakini
teknolojia pekee haiwezi kuleta mabadiliko chanya katika kuboresha
huduma na kuongeza tija hivyo teknolojia ni lazima iende sambamba na
uwekezaji katika rasilimali watu kwa watumishi kusoma zaidi na kupatiwa
fursa za mafunzo zaidi ndani na nje ya nchi
Mama
Tunu Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kuzindua kongamano hilo pia alizindua TAPSEA SACCOS na kuwataka makatibu muhtasi hao
wajiunge kwa wingi ili kutunisha mfuko wa SACCOS hiyo.
Mapema,
akimkaribisha kuzungumza na washiriki wa mkutano, Mlezi wa TAPSEA Dk.
Mary Nagu ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Uwekezaji na Uwezeshaji
aliwataka wawe waaminifu katika kuijenga TAPSEA SACCOS ili hatimaye
ifikie hatua ya kuwa benki yao maalum kama ilivyo kwa Chama cha Walimu
nchini.
Mshauri
wa Kisheria wa TAPSEA, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Angela Kairuki aliwataka washiriki wa kongamano hilo kuzingatia
maadili kwa kutunza siri za ofisi wanazozitumikia.
“Inasikitisha
kuona kila mara kunakuwa na taarifa ambazo zinavuja lakini ukifuatilia
wapi taarifa hizo zimetokea utabaini kuwa chanzo ni makatibu muhtasi…
ninawaomba sana mjitahidi kutunza siri za taasisi zenu,” alisisitiza.