Thursday, August 15, 2013

ALIYEACHA MIHADARATI APEWE AJIRA - DC

MKUU WA WILAYA YA SINGIDA MWL QUEEN M. MLOZI AKISALIMIANA NA KIJANA YUSUFU SAIMON SHUMBI BAADA YA KUTANGAZA KUWA AMEACHANA NA MIHADARATI KATIKA ENEO LA MKESHA WA MWENGE WA UHURU 2013 KATIKA UWANJA WA KITUO CHA MABASI KIPYA CHA MJINI SINGIDA
HONGERA mwanangu kwa kuamua kuachana na madawa ya Kulevya - DC Mlozi, aliyeshika kismeo ni mganga wa Manispaa ya Singida, ilikuwa Agosti 09, 2013 kituo kipya cha mabasi mjini Singida katika wiki ya Mwenge wa Uhuru



Mganga mkuu wa Manisaa, nakuagiza umpe kazi kijana huyu kwa kuamua kuachana na madawa ya kulevya na taarifa hiyo niipate mezani kwangu kuwa umempa kazi huyu kijana - DC

Singida
MKUU wa wilaya ya Singida mkoani Singida, Mwalimu Queen Mlozi amemuagiza mganga mkuu wa Manispaa ya Singida kumuajiri kijana aliyekuwa anatumia madawa ya kulevya na kuamua kuachana nayo

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu huyo wa wilaya kufuatia ushuhuda uliotolewa na kijana Yusufu Saimoni Shumbi mbele ya wananchi katika viwanja vya stendi kuu ya mabasi Singida jana katika ukaguzi wa mabanda ya Mwenge yaliyopo eneo hilouliofanywa na Mkuu wa wilaya

Alisema maelezo ya kijana huyo yanaonesha kuwa miongoni mwa kilichosababisha Yusufu kuanza kutumia madawa ya kulevya ni kukosekana kwa kazi ya kufanya na kumpa vishawishi vya kujiunga na makundi ya madawa ya kulevya hivyo uamuzi wa kwanza wa serikali ni kumpa shughuli ya kufanya kijana

Alisema vijana wanaotumia madawa ya kuelvya wako wengi na wanahitaji kuwafuatilia kwa karibu ili kuwarejeha katika hali ya kawaida na kuokoa nguvukazi ya Taifa hivyo Manispaa ya Singida itafute mbinu za kuwaweka karibu vijana walioko katika janga la madawa ya kulevya waachane na madawa hayo

“Mganga nakupa kazi moja kubwa, kuanzia leo tafuta namna ya kumpa kazi ya kufanya kijana huyu ili asije akarejea katika madawa ya kulevya na taarifa niipate haraka sana” alisema mkuu wa wilaya

Awali akitoa ushuhuda wake Yusufu Saimoni Shumbi amesema alianza kutumia madawa ya kulevya alipokuwa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Kikatiti ambako alikuwa na rafiki zake wengine ambao walikuwa wanasoma naye na baada ya kumaliza na kufeli mtihani aligundua kuwa alijipotezea muda shuleni

Alisema kutokana na kutumia madawa hayo alibadilika afya yake akawa anaugua mara kwa mara kichwa, mwili kulegea na kukosa kumbu kumbu pamoja na kukosa uwezo wa kujimudu katika baadhi ya matendo kutokana na mwili wake kulegea mikono na mikono

Alisema hivi sasa ameamua kurudia mtihani wa kidato cha nne kwani awali alifanya mtihani huo na kufeli mwaka 2011 lakini kutokana na uwezo mdogo aliokuwa nao kutokana na kutumia madawa ya kulevya alipata daraja la nne alama 30

Kwa upande wake mama mzazi wa Yusufu, Grace Shumbi (50) amesema mwanae ni kitinda mimba katika familia yake ya watoto tisa ambapo wamekuwa wakiishi kwa kutegemea kodi ya nyumba kwani alikuwa akifanya kazi ya kuhubiri neon la Mungu katika shirika la Life Ministry na kustaafu miaka kadhaa iliyopita

Amesema mwanae licha ya kuwa na hali hiyo amekuwa mwaminifu sana nyumbani kwani hata ujenzi wa nyumba kubwa wanayokaa hivi sasa aliisimamia Yusufu wakati huo mama yake akiwa anatibiwa hospitali

Amesema hivi sasa Yusufu anamdai ada akalipe shule ili asome upya aweze kurudia mtihani wa kidato cha nne ili aweze kuendelea na masomo kwani anaelewa kuwa ana uwezo wa kuendelea kusoma shule na kufaulu hadi chuo kikuu bila shida ikiwa tu atapata ada