Wednesday, August 14, 2013

REFA ALAMBWA KIPIGO AVULIWA NGUO UWANJANI



Na Ernest Simya, Sumbawanga
Mwamuzi na wachezaji watatu wa timu ya Serengeti SC ya wilayani Sumbawanga mkoani  Rukwa wamelazwa kwenye kituo cha Afya cha Laela baada kushambuliwa na kwa kupigwa sehemu mbalimbali za miili yao katika mchezo wa Ligi ya ujirani mwema.



Katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa shule ya msingi Kisalala kata ya Laela Mwamuzi wa mchezo huo Eliaza Simsokwe ilipofika dk ya 75 alishambuliwa  na kundi la mashabiki na kumvua nguo zake wakiendelea kumpa kipigo

Kipigo hicho kilisababisha mwamuzi huyo kujisaidia haja kubwa kipigo kinachodaiwa kutolewa na wapenzi wa timu ya Serengeti FC wakipinga bao lililofungwa na mchezaji wa timu pinzani ya Muchiza FC, Siyaye Mgonde wakidai alikuwa ameotea kabla ya kufunga.

Meneja wa Timu ya Serengeti FC ya Kisalala , Andrew William alisema kuwa baada ya mwamuzi huyo kuvuliwa nguo na kupata kipigo hicho ilibidi baadhi ya wananchi kuingilia kati na kumwokoa hatimaye mwanamke mmoja alimsaidia kwa kumfunga khanga  ya kumsitili kabla ya  kukimbizwa kituo cha Afya cha Laela kwa ajili ya matibabu.

 Katika vurugu hizo pia wachezaji wawili na kocha watimu ya Serengeti walijeruhiwa na kulazwa kwenye kituo hicho cha Afya pamoja na uharibifu mkubwa wa pikipiki na baiskeli 10 zilizokuwapo uwanjani hapo

Aidha ugomvi huo uliibuka tena majira ya usiku nje ya uwanja ambako watu wanaodaiwa kuwa ni wakazi wa kijiji cha Kisalala walivamia tena wachezaji wa timu ya Serengeti FC na kumjeruhi Peter Willy alijeruhiwa kwa kupigwa panga kichwani na kusababishiwa jeraha kubwa.

Kufuatia hali hiyo uongozi wa Chama cha soka wilayani Sumbawanga (SURUFA) kupitia kwa katibu wake, Kanyiki Nsokolo kimewatahadharisha washabiki wa mchezo huo kuachana na vitendo vya vurugu kwenye michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashambulia waamuzi wa mchezo kwa kuwapiga pale wanapochezesha michezo mbalimbali.

Alisema kufanyika kwa vitendo hivyo ni matokeo ya kuendesha masuala ya soka kienyeji pasipo kufuata taratibu ikiwa ni pamoja mashindano hayo kufanywa pasipo kukishirikisha chama cha soka cha wilaya sanjari na kutokuwapo kwa makocha  na waamuzi wenye sifa kwa ajili ya kuchezesha michezo mbalimbali ya soka.