Thursday, August 8, 2013

KITONGOJI CHAVAMIWA


JESHI la polisi mkoani Katavi limewatahadharisha wananchi kujihadhari na wageni wasioeleweka shughuli zao na mahali wanakotoka kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu vinavyodaiwa kufanywa na wageni kwa kushirikiana na baadhi ya wakazi wa mkoa huo
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa polisi jamii kwenye makazi ya wakimbizi ya Katumba wilaya ya Mlele, Kamanda wa polisi mkoa wa Katavi Dhahir Kidavashari alisema kuwa katika kipindi cha kiangazi kumekuwa na wimbi la wahalifu kuongezeka katika mkoa wake kunakotokana na mwingiliano mkubwa wa wananchi na wafanyabiashara wa ndani ya mkoa huo na wageni
Alisema katika matukio ya hivi karibuni kumekuwa na vitendo vya uhalifu vilivyofanywa na baadhi ya wageni kwa kushirikiana na baadhi ya wakazi wa mkoa huo wasio waaminifu ambapo licha ya polisi kufanikiwa kuwakamata wahalifu lakini vitendo vya uporaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na hata mauaji yamekuwa yakiendelea kutokea
Alisema katika tukio la hivi karibuni baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Ilebula B’ kata ya Katuma wilaya ya Mpanda walivamiwa na majambazi waliokuwa na silaha aina ya SMG na kupora fedha  na simu zao majira ya saa sita usiku katika tukio la Agosti 2, 2013
Aliwataja walioporwa katika tukio hilo ambalo awali majambazi walifyatua risasi mbili hewani ni ndugu Juma Kubu (38) aliporwa fedha taslimu shilingi 132,000/= na simu aina ya Techno yenye thamani ya shilingi 40,000/=, ndugu Moshi Masanilo (23) aliporwa baiskeli moja aina ya Phoenix yenye thamani ya shilingi 150,000/=, Thelethini Msoke (45) aliporwa bia sita na soda nne vyote vikiwa na thamani ya shilingi 16,000/=
Wengine walioporwa aliwataja kuwa ni Alphonce Charles (23) aliporwa fedha taslimu shilingi 130,000.= na simu aina ya Yxtel yenye thamani ya shilingi 65,000/=, Jumanne Kashindye (28) aliporwa simu aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 40,000/=, Christina John (42) aliporwa fedha taslimu shilingi 120,000/= na simu aina ya Techno yenye thamani ya shilingi 45,000/= na ndugu Sisilia Ezekiel (49) aliyeporwa simu aina ya Oking yenye thamani ya shilingi 60,000/=
Aidha Kamanda wa polisi mkoani hapa aliwataja wengine waliioporwa kuwa ni Regina Ezekiel (37) ambaye aliporwa fedha taslimu shilingi 6,000/= na simu aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 40,000/=, ndugu Cosmas Mathia (42) aliyeporwa shiligi 70,000/= na simu aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 40,000/=, Ndilanha Charles (40) aliyeporwa simu aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 30,000/= na ndugu Dotto Peter (29) aliyeporwa simu aina ya Nokia yenye thamani ya shilingi 35,000/=
Alisema katika tukio hilo ni dhahiri kuwa majambazi walifikia katika hali mbaya kwani wamevamia kitongoji kizima ingawa hawakujeruhi mtu yeyote lakini bado ipo haja kwa jeshi la polisi na wananchi kuchukua hatua za makusudi ili kuutokomeza kabisa uhalifu wa namna hiyo na uhalifu mwingine wowote mkoani Katavi
Pamoja na kuwashukuru wananchi waliotoa ushirikiano uliopelekea kukamatwa kwa watuhumiwa wa uvamizi huo wapatao wanne wanaodaiwa kushiriki katika kuvamia kitongoji na kuwapora wananchi ambapo kamanda aliwataja waliokamatwa kufuatia tukio hilo kuwa ni ndugu Sengwa Mojo (43) , ndugu Amosi Ngasa (43), Barabashi Kasomi (43) na ndugu Mojo Nsengwa (43) wote kabila lao ni Wasukuma wakazi wa kitongoji cha Ilebula wilaya ya Mpanda.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia taarifa za baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho zilziopelekea kupata baadhi ya simu zilizoporwa majumbani kwao baada ya kupekuliwa na askari polisi ambapo upelelezi unaendelea na watuhumiwa hao watafikishwa mahakani ingawa maelezo yanaonesha kulikuwa na mpango wa muda mrefu wa kutaka kuvamia kitongoji hicho kwa kutumia silaha lakini wananchi hao hawakuona umuhimu wa kutoa taarifa polisi hadi walipovamiwa kweli
Aliwataka wananchi mkoani humo kuwa makini na nyendo za baadhi ya wananchi wenzao wanaotafuta utajiri kwa njia zisizo halali na kutoa taarifa mapema ili kuweza kuzuia tukio badala ya kuwa maarufu wa kutoa taarifa za uhalifu baada ya kutokea kwani dhana ya jeshi la polisi ni kuzuia uhalifu kabla ya kutokea
POMBE YA GONGO YAUA
POMBE ya moshi maarufu kwa jina la pombe ya gongo inadaiwa kusababisha kifo cha ndugu Aloyce  Alfredy Sali, ( 32) ambaye alikutwa akiwa amefariki dunia chumbani kwake kwenye nyumba aliyokua amepanga baada ya kunywa pombe hiyo na kulewa chakali jana yake.
Taarifa zilizopatikana mjini Mpanda zinadai kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 3, 2013 majira ya saa kumi na moja jioni marehemu alikwenda katika eneo maarufu kwa kuuza pombe haramu ya moshi maarufu kama pombe ya gongo liitwalo Mpandahoteli katika baa ya  MWANDOSYA na kuanza kunywa pombe moshi aina ya gongo.
Ilielezwa kuwa baadaye marehemu alilejea nyumbani kwake anakoishi peke yake bila familia na kuingia ndani na kulala hadi kesho yake tarehe Agosti 4, 2013 majira ya saa sita mchana ambapo  Marehemu hakuonekana kuamka ndipo majirani walipopata wasiwasi na kufatilia kwa karibu ambapo walibaini marehemu alisha fariki na kuamua kutoa taarifa kituo cha Polisi Mpanda. 
Kamanda wa polisi mkoani Katavi, Dhahiri akizungumza na gazeti hili alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa Uchunguzi wa tukio hilo unaonesha chanzo cha kifo cha marehemu ni kutokana matumizi ya pombe ya moshi aina ya gongo yaliyokithili pasipo kula chakula.
Akizungumzia matukio mengine kamanda wa polisi Kidavashari alisema kuwa Agosti  3, 2013 majira  ya saa mbili usiku katika kijiji cha Ikaka kwenye barabara ya Mpanda kwenda Karema gari yenye namba za usajiri T707AFQ aina ya Canter inayomilikiwa na Bwanali  Kondowe mkazi wa Makanyagio mjini Mpanda  lilipinduka  na kusababisha kifo cha mtu mmoja ambaye haijafahamika.
Alisema katika tukio hilo watu watano walijeruhiwa na kupelekwa hospitali kuu ya Mpanda na kwa matibabu na baadaye waliruhusiwa kutoka hospitali kutokana hali yao kuwa njema ambapo aliwataja majeruhi kuwa ni Cletus Isack(21), Erick Itala (21), Juma Yasini (20), Digas Elisha (25) na Musa Elisha (20) wpte wakazi wa wilaya ya Mpanda mkoani Katavi
Aidha kamanda Kidavashari alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa  dereva ambapo bado anaendelea kutafutwa
mwisho