Saturday, August 3, 2013

KATAVI WAOMBA KUADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI


MKOA wa Katavi umeanza mchakato wa kuomba maadhimisho ya siku ya
Mazingira dunia mwaka 2014 zifanyikie mkoani humo ili kupata wigo wa
kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi wa mkoa huo

Hayo yalibainika katika kikao cha mkuu wa mkoa wa Katavi Dr Rajabu
Rutengwe na wanahabari kilichofanyika katika ofisi yake mwishoni mwa
wiki kikao kilichokuwa kikilenga kuwashukuru wananchi wa mkoa huo na
wana habari namna walivyofanikisha mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani
kwake

Alisema katika mkoa wake kumekuwa na kasi kubwa ya uharibifu wa
mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu hasa ufugaji holela
na uingizaji mifugo kiholela unaoendelea katika mipaka ya mkoa huo na
kusababisha kupotea kwa uoto wa asili katika mmisitu mbalimbali ya
mkoa huo

“Mtakubaliana name kuwa hakuna mkoa wenye uoto wa asili na misitu
minene katika nchi yetu zaidi ya hapa Katavi, tuna mashaka mandhari ya
Katavi itatoweka mapema kama hatujachukua hatua kwani uingizaji mifugo
kiholela imekuwa na utamaduni na watu wengine wanaona kuvamia misitu
kwa shughuli za kilimo ni haki yao” alisema mkuu wa mkoa

Alifafanua kuwa ofisi yake inapochukua hatua baadhi ya wafugaji
wanahisi kuonewa badala ya kuangalia namna wanavyoathiri mazingira na
kuharibu uoto wa asili kwani wafugaji wote walioingia mkoani humo kwa
kipindi cha miaka mitano iliyopita waliingia kinyemela na kupata
uhalali kwa njia ya udanganyifu

Alisema hivi sasa ofisi yake imeanzisha program maalumu ya kuhakikisha
inazuia uingiaji holela wa mifugo na kuanza kuwachukulia hatua
viongozi wa vijiji, kata na vitongoji wanaowapenyeza wafugaji kwa njia
zisizo halali na kuwapa hifadhi kutokana na rushwa
Dr Rutengwe alisema watendaji na viongozi wa vijiji walioshiriki
kuwaingiza kinyemela.

wafugaji wameshaanza kuchukuliwa hatua na hawatasita kuwashughulikia
wala rushwa mkoani kwake bila kujali nafasi zao katika jamii kwani
kumekuwa na mtindo wa kupokea pesa kutoka kwa wafugaji na kuingiza
mifugo kinyemela  katika maeneo mbali mbali mkoani humo na kusababisha
uharibifu wa mazingira

Akizungumzia suala la elimu ya mazingira mkuu wa Mkoa alisema mpango
huo unaendelea na hivi sasa mkoa unajiandaa kuomba maadhimisho ya siku
ya mazingira duniani mwaka 2014 zifanyikie katika mkoa wake

“Tunaomba ofisi ya Makamu wa Rais baada ya kuandaa mkoa wa Rukwa,
maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani mwakani tuandae sisi hapa
mkoani Kwetu ili kuweza kupata uwanja mpana zaidi wa kutoa elimu na
hamasa ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa wananchi wetu” alisema
Dr Rutengwe

Maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani mwaka huu 2013 yalifanyikia
katika mji wa Namanyere wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa ambapo mgeni
rasmi alikuwa makamu wa Rais Dr Mohammed Gharib Bilal