Wednesday, January 9, 2013

KATIBU KOTINI KWA KUTISHIA KUUA

KATIBU WA CCM MUFINDI AFIKISHWA MAHAKAMANI AKITUHUMIWA KUTISHIA KUUA



 .

KATIBU  wa chama  cha mapinduzi (CCM) wilaya ya Mufindi Jackob Nkomola leo amefiishwa mahakamani akituhumiwa  kuua kwa maneno .
Akisoma shtaka hilo  linalomkabili katibu  huyo  mahakamani hapo hakimu  wa mahakama ya mwanzo Mafinga wilayani Mufindi Zakaria Mushi alisema  mtuhumiwa Jackob Nkomola anashtakiwa kwa kosa la kumtishia kumuua  kwa maneno, Alexandel Tweve  kinyume na  sheria kifungu namba 89 kifungu kidogo “A”.

Aidha hakimu huyo alisema mshitakiwa alitenda kosa hilo, Octoba 3 mwaka 2012 katika eneo la Mkombwe, ambapo alimtishia mkazi huyo wa mji  wa Mafinga  wilaya ya Mufindi..

Mtuhumiwa alikana shtaka hilo na hakimu kutoa masharti ya dhamana ya ahadi
ambayo inathamani ya shilingi  200,000 na adhaminiwe na mtu mmoja
atakayetambulishwa kwa barua kutoka katika ofisi ya serikali ya kijiji au
Kata masharti ambayo yalitimizwa na mshitakiwa na kesi hiyo itafikishwa  tena mahakamani hapo Januari 30 mwaka huu.

Hakimu alimtaka mlalamikaji   wa kesi hiyo kufika na mashahidi wake
aliowaorodhesha.
Wakati  huo  huo mwandishi  wa habari  wa gazeti la mtanzania  mkoani Iringa Oliver Moto amenusurika  kupigwa na mtuhumiwa  huyo  wakati akitimiza wajibu  wake kwa  kumpiga picha mtuhumiwa  huyo .
Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya mtuhumiwa huyo  kusomewa mashtaka yake na kusubiri kutimiza masharti ya dhamana na akiwa chini ya ulinzi  ya ulinzi  wa  polisi mahakamani hapo

Hatua hiyo iliwashangaza watu waliohudhuria kesi hiyo katika mahakama hiyo huku  wakihoji mamlaka ya mtuhumiwa kumfuata umbali wa hatua zaidi  ya tano mwandishi, huku mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi kwa kuwa bado alikuwa naashikiriwa na Mahakama hiyo kwa kutokidhi vigezo vya dhamana yake.

Kutokana na tukio  hilo lilimlazimu mwandishi  huyo kukimbilia kwa hakimu wa mahakama hiyo akitaka msaada  wake katika  hilo   huku hakimu Mushi akimtaka  mwandishi huyo kufika kituo chapolisi kutoa taarifa ya tukio hilo ushauri ambao hakuufanyia kazi .

Akiwa njiani Mwandishi alimpigia simu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi
Cosmas Kaguo ambaye alimuomba mwandishi kuonana naye kabla ya kufika katika
kituo cha Polisi cha Mafinga.

Hatua ya mwenyekiti wa CCM Kaguao, - aliitisha kikao cha dharua cha kamati
ya siasa na kuomba radhi juu ya tukio lililotokea, na baada ya muda dakika
20 Katibu wa CCM (Mtuhumiwa) aliingia katika moja ya ofisi ya Halmashauri
ya Wilaya ya Mufindi, iliyopo katika ukumbi wa mikutano na kuomba radhi juu
ya kile alichokifanya kwa  mwanahabari huyo  mahakama.

Ombi la mwenyekiti wa CCM Wilaya, lilikubaliwa na mwandishi huyo kwa
kusitisha hatua yake ya kufungua kesi katika kituo cha polisi Mafinga.

Akitoa utetezi wake, mtuhuimiwa huyo alisema “Ninaomba unisamehe sana
Oliver, unajua kesi yangu hii niya kisiasa, na kukufanyia hivyo ni hasira
baada ya mtu anayenituhumu kutumia njia mbalimbali za kuniangamiza, ninajua
nimekukwaza wewe, lakini pia nimeidhalilisha taaluma yako, ninakuomba
unisamehe,” Alisema Nkomola.

WASIRA: KILIMO KWANZA KUUFIKISHA UCHUMI MIFUKONI MWA WANANCHI

 

                                                              Waziri Wasira

 NA MWANDISHI WETU
UHALISIA wa kukua kwa uchumi hadi mifukoni mwa wananchi walio wengi una matumaini ya kufikiwa kutokana na
utekelezwaji  madhubuti wa kuinua Kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza unayotekelezwa na serikali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera na Uratibu, Steven Wasira alipokuwa akizungumza kwenye
kipindi cha 'Tuongee Asubuhi' cha kituo cha televisheni cha Star Tv, leo, Januari 15, 2013.

Katika kipindi hicho, kilichokuwa na mada ya 'Uhalisia na Kukua kwa Uchumi' pamoja na Wasira wazungumzaji wengine
walikuwa, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo cha SAUTI cha Mwanza, Odas Bilame.

Wasira alisema, kwa sasa wananchi wengi hawaoni uhalisia wanapoambiwa kwamba uchumi wa nchi unakuwa, kwa
sababu, hali ya kukuwa kwa uchumi kwa sasa hakujawagusa waajiriwa katika sekta ya kilimo ambao ndio wengi kiasi
cha asilimia 80.

Alisema, katika kipindi cha kati ya mwaka juzi na mwaka jana uchumi wa Tanzania ulionyesha kuwa umekuwa kwa kati
ya asilimia 6.5 na 6.7, lakini kukua huku kuliwagusa zaidi watumishi waliopo katika sekta nyingine kama za viwanda na
watumishi wa umma.

"Katika hali hii ambayo watumishi wa sekta zote wanategemea lazima wapate chakula na mazao mengine kutoka kwa
wakulima, ambao hawajanufaika vya kutosha na mafanikio ya kukua wa uchumi huu, ni lazima, athari za kutoonekana
ukuaji uchumi katika jamii utakuwepo", alisema, Wasira.

Alisema, kutokana na kutambua kwamba ni lazima sekta ya Kilimo iboreshwe vya kutosha ndipo ukuaji wa uchumi utadhihirika kwa uhakika miongoni mwa wengi, Serikali imeelekeza nguvu zake kuhakikisha mpango wa Kilimo Kwanza unazaa matunda.

Alisema, katika jitihada za kufikia lengo hilo, Serikali imetenga sh. bilioni 300 kwa ajili ya kuwekeza kwenye utafiti katika kilimo, ambapo katika uwekezaji huo, sasa wapo wataalam wengi na maofisa ugani vijijini kwa ajili ya kuwezesha wakulima kufanya kilimo bora na cha kisasa.

Wasira alisema, pia kiwanda cha mbolea cha Minjingu kimejengwa ili kuongeza upatikanaji wa mbolea ili kuhakikisha kwamba kila mkulima anapata mbolea ya kutosha na kuongeza kuwa  pamoja na kiwanda hicho Serikali inao mpango wa kujenga vingine vya mbolea ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa pembejeo hiyo.

Alisema, wakati jitihada zimewekwa kwenye uinuaji sekta ya kilimo, ujenzi na uboreshaji miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara na reli, utafungua milango ya mazao kutoka vijijini kwenda maeneo mbalimbali nchini hata nje ya nchi kwa urahisi, hatua ambayo itachochea kukua kwa kasi zaidi kwa uchumi.

Akielezea historia ya Uchumi wa Tanzania, Wasira alisema, awali hali ya uchumi ilikuwa ikienda vizuri, lakini ilianza kuathiriwa na uhaba wa mafuta miaka uliojitokeza miaka ya 1977 lakini ukaendelea kuathiriwa zaidi na vita vya Kagera, mwaka 1978 na hadi sasa zimeendelea kuwepo changangamoto za kidunia ambapo Tanzania kama moja ya nchi zilizomo haiwezi kuzikwepa.

Kwa upande wake Profesa Lipumba, alikiri kwamba Kilimo Kwanza ni 'muarobaini' wa kukua kwa uchumi wa nchi, lakini akaonya kwamba ni lazima juhudi za makusudi zifanyike kuhakikisha kuwa uhalisia wa kukua wa uchumi ni kuigusa mifuko ya wananchi.

Pamoja na kukiri umuhimu wa mpango wa kilimo kwanza, Profesa Lipumba aliponda kwamba, licha ya mikakati mizuri  kuwepo lakini mingi ipo katika makatarasi tu, haitekelezwi kwa vitendo.

"Sasa kama dhamira ipo, umefika wakati wa watekelezaji kuacha maneno na badala yake kufanya kazi kwa vitendo zaidi", alisema Lipumba.

Kwa upande wa nafasi ya wasomi wanavyoisadifu hali ya kukua kwa uchumi Tanzania, Odax alisema, wasomi wanakubalina kwamba juhudi zikiwekezwa kwenye kilimo uchumi utakuwa.
Waziri mkuu Mizengo Pinda amemtunuku Rpc wa mkoa wa katavi acp Dhahiri Kidavashari Tuzo ya heshima ya mkoa wa katavi ya mwaka 2012 kutokana na uhamasishaji wa jamii kushirikiana na jeshi la polisi katika kupambana na uhalifu yani polisi jamii kulia kwa waziri mkuu ni mkuu wa mkoa wa wakatavi Dr Rajabu Rutengwe na kulia kwa mkuu wa mkoa ni Mbunge wa mpanda mh Saidi Arifi sherehe hiyo ilifanyika usiku wa mkesha wa kukaribisha mwaka mpya mkoani katavi picha na chris mfinanga

WAZIRI MKUU PINDA AZINDUA KITABU CHA WAPIMBWE

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua kitabu cha historia ya kabila la Wapimbwe lililoko mkoani Katavi na kutayataka makabila mengine kuandika historia zao ili waweze kutunza kumbukumbu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Akizindua kitabu hicho hivi karibuni mjini Mpanda, Waziri Mkuu aliwataka watu wa makabila mengine ya mkoa wa Katavi ambayo ni Waruira, Wabende, Wakonongo na Warungwa wafanye tafiti kuhusu mila na tamaduni zao na kisha waandike vitabu vyao.

Kabla ya uzinduzi huo, mtunzi wa kitabu hicho, Bw. Peter Mgawe alisema kitabu hicho kimetokana na utafiti uliofanywa tangu mwaka 2007 ambao ulilenga kukusanya  taarifa na masimulizi mbalimbali kutoka kwa wazee wa Kipimbwe ambao wameishi miaka mingi huku wakiwa na hazina ya mila na tamaduni za kabila hilo ambalo pia ni kabila lake Waziri Mkuu Pinda.

“Hili ni kabila dogo lisilofahamika na wengi, nimekuwa nikitafuta taarifa na machapisho (literature) mbalimbali kuhusu kabila hili lakini sikuwahi kupata chochote… ndipo nikamshirikisha Mheshimiwa Waziri Mkuu juuya kufanya utafiti na kuandika historia yetu naye akalikubali wazo langu,” alisema Bw. Mgawe ambaye pia ni
Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Akizungumza na wakazi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri Mkuu alisema utafiti huo usiishie hapo tu, bali wafanye tafiti nyingine kuhusu mavazi, vyakula, ndege, wanyama waliokuwa wakipendelewa na mababu zao ili kuongeza hazina ya taarifa ya kabila hilo.

“Lengo la kitabu hiki lilikuwa ni kuhifadhi katika maandishi historia ambayo ilikuwa imefichika ndani ya vichwa vya wazee wetu kutoka vijiji mbalimbali vya Mpimbwe… nafurahi kwamba tunao wazee watatu waliokuwa katika warsha ya kwanza kabisa iliyofanyika mwaka 2008. Leo hii wako hapa na wanashuhudia matunda ya kazi yao,” Alisema Waziri Mkuu.

Wazee hao ni Mzee Simba Pangani Kalulu (76) kutoka kijiji cha Mamba, Mzee Valeri Kipande (76)  kutoka kijiji cha Lyangalile na Mzee Moses Kasalani (67) kutoka kijiji cha Mirumba. Vijiji vyote hivyo viko wilaya ya Mlele, mkoani Katavi.

Waziri Mkuu amerejea jijini Dar es Salaam jana mchana (Jumanne, Januari 9, 2013) akitokea kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele, Katavi ambako alifanya ziara ya siku 10 kwenye jimbo lake la Katavi na kisha kuwa na mapumziko ya Krismasi na mwisho wa mwaka.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JANUARI 09, 2013.
Itatoka katika Radio; Uhuru Fm DSM saa 21:00 USIKU leo Januri 10, 2013 kipindi cha Habari na Matukio