KATIKA hali isiyo ya kawaida mtu mmoja alifariki dunia mbele ya duka lake akiwa
amekaa katika kiti cha kienyeji cha mti katika soko kuu la mjini Mpanda mkoa wa
Katavi
Tukio hilo ambalo limethibitishwa na jeshi la
polisi mkoa wa Katavi lilitokea Julai 17, 2013 majira ya saa kumi jioni, Isack
Malisele Mandevu (58) alifariki dunia ghafla akiwa ameketi katika kiti chake
cha kienyeji dukani kwake katika soko kubwa la mjini Mpanda kata ya Kashaulili
Marehemu ambaye kabila lake ni
Muhutu mkazi wa Kanoge “A” katika makazi ya wakimbizi Katumba alikuwa
mfanyabiashara katika soko kuu mjini Mpanda alikuwa amefungua maduka mawili katika eneo hilo akiuza bidhaa
mbalimbali ambapo alikuwa amenunua kiti cha kienyeji kilichotengenezwa kwa miti
ikiwa ni kiti chake cha kukalia kwa kipindi kirefu sasa
Siku ya tukio marehemu alikuwa
dukani kwake akiwa anaendelea na kazi yake ya kuuza duka, majira ya mchana
alifika dukani hapo majira ya mchana saa tisa alasiri mwanafunzi wa chuo cha
ufundi stadi VETA Mpanda ambaye ni mwanaye anayeitwa Mlema Issack Malisele (18)
kumsalimia baba yake na kuondoka
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoa
wa Katavi Dhahir Kidavashari alisema jana kuwa marehemu alifariki majira ya saa
kumi jioni mara baada ya mwanae kuondoka wakati taarifa za hali ya afya ya
marehemu kwa muda wa siku za nyuma unaelezewa kuwa alikuwa hana tatizo lolote
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu
ambaye ni mwanafunzi wa VETA, marehemu hakuwa na historia ya kuugua ugonjwa
wowote zaidi ya kuwa na kisukari na shinikizo la damu ingawa kwa siku za hivi
karibuni hata hayo magonjwa yalikuwa hayamsumbui.
WATATU MBARONI KWA UTAPELI
WATU watatu wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Katavi kwa tuhuma
za kujifanya maafisa wa Serikali idara ya ardhi mkoa wa Katavi na kujipatia
kiasi cha shilingi mil. 7 kwa njia ya utapeli
Kwa mujibu wa Kamanda wa jeshi la
polisi mkoa wa Katavi, Dhahir Kidavashari waliokamatwa ni Isambi Edwin Yalamda Mnyiha
mkazi wa Makanyagio mjini Mpanda, Amosi Jeremiah Mwanawima na mfanyakazi mmoja
wa steshenari ambapo imebainika kuwa mtuhumiwa wa kwanza Isambi Edwin Yalamda
anatumia majina mawili kwani katika vyeti alivyoonesha vya taaluma ya upimaji
ardhi ametumia jina la Sambuli Tegemeo
Kamanda Kidavashari alifafanua
kuwa mtuhumiwa Isambi Edwin anatuhumiwa kufanya utapeli wa kuuza viwanja isivyo
halali kwa kujifanya afisa wa serikali ambaye ni Kamishina wa ardhi mkoa wa
Katavi, kughushi nyaraka za serikali kama risiti na muhuri wa kuonesha kuwa
yeye ni kamishina wa ardhi mkoa wa Katavi
Kamanda Kidavashari aliwataja
wahanga wa utapeli huo kuwa ni walimu kumi, watumishi wa idara ya afya na
wananchi wasio watumishi wametapeliwa kiasi cha shilingi 7,410,000/=
zilizolipwa kwa mpesa na malipo ya fedha taslimu kwa nyakati tofauti tangu
Novemba 2012 hadi Julai 20, 2013
Imefafanuliwa kuwa watuhumiwa hao
wawili wanatuhumiwa kushirikiana na mtuhumiwa wa kwanza Isambi Edwin Yalamda
katika maandalizi ya shughuli hiyo kama
uandaaji wa mihuri ya ardhi na uchapaji wa nyaraka feki zinazofanana na nyaraka
halisi za Serikali
Katika hatua nyingine Menso
Kobakusha (38) mbende mkazi wa kijiji cha Majalila Mpandandogo wilaya ya Mpanda
mkoani hapa anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Katavi kwa tuhuma za
kumiliki silaha aina ya gobore kinyume cha sheria na risasi iliyotengenezwa
kienyeji na mnyama pori
aina ya mbawala.
Kamanda wa jeshi la polisi
aliwaeleza waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa mtuhumiwa alikamatwa pia
na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogramu 2.5 ambapo vitu hivyo
mtuhumiwa alikwenda kuvikabidhi mwenyewe kwa mwenyekiti wa kijiji cha Majalila,
Frank Kibigisa.
Alisema mtuhumiwa aliamua
kuvikabidhi vitu hivyo kwa mwenyekiti muda mfupi baada ya askari polisi
kuondoka kijijini hapo walitoka kupekuwa nyumbani kwake na kuvikosa kufuatia
taarifa ya raia wema kuwa mtuhumiwa anamiliki silaha isivyo halali taarifa
zilizowafikisha askari nyumbani kwa mtuhumiwa huyo kupekua na kuvikosa.
Alisema kitendo cha askari kufika
nyumbani kwake na kupekua ingawa walivikosa kilimfanya mtuhumiwa kuchukua
silaha, risasi, nyama ya mbawala na bangi na kuvikabidhi kwa mwenyekiti wake wa
kijiji kwa kujisalimisha vyote vikiwa vimeviringishwa katika begi dogo jeusi la
maungoni ndani ya nyumba yake.
Kamanda Kidavashari alitoa shukrani kwa
wananchi wanaotoa ushirikiano kwa jeshi lake hadi
kufanikisha kupatikana kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali mkoani humo mara kwa
mara.