MWENGE wa Uhuru umekamilisha mbio katika mkoa wa
Katavi kwa kutembelea, kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kukabidhi miradi 36
yenye thamani ya shilingi Bil 2.
Hayo yalibainishwa na mkuu wa mkoa wa Katavi, Dr
Rajabu Rutengwe alipokuwa akikabidhi mwenge huo kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa,
Mhandisi Stella Manyanya makabidhiano yaliyofanyikia katika kijiji cha Kizi
wilayani Nkasi.
Dr Rutengwe alisema ukiwa katika mkoa
wake Mwenge wa Uhuru umekimbizwa umbali wa kilometa 518, wilaya 2, halmashauri
nne zote zikiwa na miradi 36 yenye thamani ya shilingi 2,044,059,281/= ambapo
mchango wa wananchi ni shilingi 188,875,472/= na
kiasi kilichosalia kimetolewa na Serikali kuu na Halmashauri.
Aliwataka wananchi kuanza
kuufanyia kazi ujumbe wa Mwenge mara baada ya kukamilisha mbio hizo katika mkoa
wake na kuahidi kuwa ofisi yake itazichambua hotuba za Mwenge zilizotolewa
katika kipindi cha siku tatu na kutengeneza utekelezaji wake ikiwa ni
maandalizi ya Sherehe za miaka hamsini ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar
Januari 12, 2014.
Akizungumza katika
makabidhiano hayo Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka 2013, Juma Ali Simai
aliwataka wananchi kuilinda amani iliyopo Tanzania kwa kuwaepuka watu
wanaojenga chuki baina ya jamii kwa misingi ya utofauti wa kiitikadi, kiimani,
kimaeneo, kikabila au kwa misingi ya rasilimali za Taifa kwani kumeibuka watu
wanatumia majukwaa ya kijamii kuhutubia sera za kuwagawa Watanzania kwa
makusudi
Alisema rasilimali zilizopo
mahala popote Tanzania ni mali ya Watanzania wote na kipato kinachopatikana
kutokana na rasilimali hizo kikagawanywa kwa Watanzania wote kupitia shughuli
za Maendeleo na huduma za jamii kama vile
hospitali, maji, miundombinu, elimu, kilimo, ufugaji, n.k
Aidha Simai aliwakumbusha
Watanzania kuanza maandalizi ya kusherehekea miaka hamsini ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya Januri 12, 1964 ambapo sherehe hizo zitafanyika nchi nzima Januari
12, 2014 katika ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa na Taifa ikiwa ni ishara ya
kuenzi Mapinduzi hayo yaliyopelekea kupatikana kwa Muungano wa Tanzania
uliafanyika miezi mitatu baadae Aprili 26, 1964 na kuunda Taifa moja la
Tanzania.
Alisema bila Muungano hakuna Tanzania hivyo kila Mtanzania popote alipo
anatakiwa kuulinda Muungano kwani atakuwa anailinda nchi yake ya Tanzania
na amali zake zilizoasisiwa na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Abeid Amani Karume enzi za uhai wao.
Mwenge wa uhuru ulianza mbio
zake mkoani Katavi Julai 16,2013 baada ya kukabidhiwa mkoa huo kutoka mkoani
Kigoma na kukamilisha mbio hizo Julai 19, 2013 baada ya kutembelea wilaya za
Mpanda na Mlele.
mwisho