Monday, July 22, 2013

SUMU YA NYAMONGO IKO KATUMA, POLISI WASEMA TUMEKAMATA WATATU






















AFYA za watumiaji wa maji ya bonde la mto Katuma katika wilaya za Mlele na Mpanda mkoani Katavi ziko hatarini kutokana na matumizi ya kemikali yenye sumu inayotumika kuyeyushia mawe yenye madini na kutiririsha katika mto Katuma  
                                                                                                     
Hayo yalibainika katika kikao cha wanajumuiya ya watumiaji wa bonde dogo la mto katuma jana baada ya wakazi wa kijiji cha Katuma wilaya ya Mpanda kulalamikia kitendo cha mwekezaji mmoja wa uchimbaji madini kuyeyusha mawe ya madini kwa kutumia maji ya mto huo na kemikali inayodaiwa kuwa ni sumu

Walidai kuwa mwekezaji huyo anatumia kemikali iliyokatazwa kutumika katika mgodi wa North Mara mkoani Kagera kuyeyushia mawe ambapo amejenga matanki makubwa anayojaza maji na mawe na kasha kumwagia kemikali ambayo inachemsha mawe na maji kama maji yanavyochemka na kuruka katika sufuria la chai hadi mawe yanapoyeyuka na kubaki kama uji

Myeyuko huo una poozwa na kuchujwa ili kubakisha uji wenye madini aina ya dhahabu na masalia yenye sumu yanatupwa ovyo hali inapelekea tope hilo lenye sumu kutiririkia mto Katuma ambao unatumika kwa kazi za kilimo, kunyweshea wanyama na matumizi ya binadamu 

Imebainika kuwa hata maji yanayotumika katika shughuli za kuyeyushia mawe na matumizi mengine ya uchimbaji yanatoka katika mto Katuma licha kuwa kampuni hiyo ambayo haijafahamika jina lake haina kibali cha kutumia maji kutoka Wizara ya Maji

Mkuu wa wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema kuwa ofisi yake imelipata na kuanza kulifanyia kazi kikamilifu na baada ya kukamilisha uchunguzi ofisi yake itatoa taarifa na kuchukua hatua stahiki ili kulinda afya za wananchi na viumbe hai katika bonde la mto Katuma na mto  mto Katuma wenyewe.












WANOLEWA KULINDA MTO KATUMA

OFISI ya Bonde la Ziwa Rukwa imeanza kuwajengea uwezo wananchi watumiaji wa maji ya bonde dogo la mto Katuma katika wilaya za Mlele na Mpanda mkoani Katavi ili waweze kulisimamia bonde hilo, kulitunza na kulinda rasilimali ya maji  ya mto Katuma kwa manufaa ya wananchi wenyewe

Mafunzo hayo yanawashirikisha wanajumuia watumia maji ya bonde la mto Katuma kutoka vijiji vya Sitalike, Kakese, Mwamkulu, Katuma, Bugwe, Mnyagala na Kambaga katika wilaya za Mlele na Mpanda mkoani Katavi yanaendeshwa na kusimamiwa na Bonde la Ziwa Rukwa ili kuunda jumuiya ya kulinda vyanzo vya maji vinavyoutengeneza mto Katuma 

Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Bonde la Ziwa Rukwa, Thadeus Ndeseiyo alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wanajumuiya wa bonde dogo la Katuma ambao ni watumiaji wa rasilimali ya maji ya  bonde hilo ili waweze kusimamia, kulinda na kuendeleza uhifadhi wa mazingira ya bonde la Mto Katuma na mto Katuma wenyewe.

Alisema shughuli ya kuunda jumuiya ya watumiaji maji wa bonde la Katuma itachukua mwezi hadi kukamilika ikiwa ni pamoja na kuunda katiba itakayowawezesha kufanya kazi kisheria na kulinda vyanzo vya rasilimali ya maji katika bonde dogo la Katuma ambalo liko hatarini kutoweka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira ulioko katika vyanzo vya maji ya Mto Katuma

Alisema ofisi yake inategemea jumuiya hiyo kuweza kusimamia, kuzilinda na kuhifadhi rasilimali za maji kwani kutokana na mafunzo hayo jumuiya iatweza kuibuka na kanuni, taratibu hatimaye katiba yake yenyewe itakayowaongoza kusimamia rasilimali za maji kwa pamoja itakayosaidia kuondoa migogoro ya mara kwa mara katika maeneo yote ya bonde la Katuma

Mafunzo hayo yanayotolewa na wataamu wa maji na uhifadhi wa mazingira kutoka halmashauri za wilaya ya Mpanda na Halmashauri ya Mji wa Mpanda yalianza Julai 20, 2013 kwa lengo la kuhakikisha kuwa matumizi ya rasilimali ya maji katika bonde la Katuma yanakuwa endelevu na kwa manufaa ya wananchi wote.




 WAWILI WAKUTWA NA SMG SITALIKE

WATU wawili wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Katavi kwa kukutwa na silaha ya kivita aina ya SMG na risasi ishirini na moja kinyume cha sheria

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Katavi, Dhahir Kidavashari aliwataja waliokamatwa kuwa ni Bosco Mpangwa (48) mkazi wa Mpandahoteli mjini Mpanda wilaya ya Mpanda na Frank Sabuni (21) mkazi wa kijiji cha Sitalike wilaya ya Mlele

Alisema watuhumiwa walikamatwa Julai 20, 2013 majira ya saa sita usiku katika kijiji cha Sitalike wilaya ya Mlele wakiwa na silaha aina ya SMG ikiwa na namba tofauti ya vifaa vilivyounda silaha hiyo huku mwili wa silaha hiyo ukiwa umeundwa kwa sehemu tatu yaani mwili wa bunduki yenye namba BD17B804, Coocking Handle yenye namba H7092 na Kipokeo (receiver) yenye kava namba 685 na risasi 21 za SMG/SAR

Alifafanua kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema baada ya kupata taarifa hizo askari wa hifadhi ya Katavi (TANAPA) na askari wa polisi waliweka mtego  wa kuwakamata katika eneo la shule ya Msingi Sitalike ambapo watuhumiwa walifika eneo hilo huku mtuhumiwa Bosco akiwa amvaa silaha huku akiwa amifunika kwa koti kubwa zito walipokuwa wakielekea katika hifadhi ya wanyama ya Katavi kufanya ujangili

Kamanda Kidavashari alisema mtuhumiwa Bosco pia ana kesi nyingine ya Uhujumu uchumi Economy Namba 15/2008 na mwenzake ana kesi ya kupatikana na Nyara za Serikali CC Namba 293/2012 katika mahakama ya wilaya ya Mpanda

Kamanda Kidavashari alisema  uchunguzi umekamilika hivyo watuhumiwa watafikishwa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma zinazowakabili

Katika tukio lingine Dickson Petro Ntaali anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa mke wake tukio lililotokea Julai 15, 2013 majira ya saa nne usiku katika kijiji cha Mwamkulu wilaya ya Mpanda mkoani Katavi

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Katavi Dhairi Kidavashari alisema mtuhumiwa alikamatwa kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa mke wake, Solile Elikana (35) kwa kukatwa katwa na kitu chenye ncha kali kichwani, usoni na kwenye mikono ya mwili wake.

Alisema tangu wanandoa hao kuhamia katika kijiji cha Mwamkulu wakitokea wilayani Magu mkoani Mwanza April 2013 walikuwa na ugomvi wa ndani baina yao hadi wakafikishana kwa mwenyekiti wa kijiji hicho na kuvunja ndoa yao mbele ya uongozi wa kijiji mnamo Julai 12, 2013 na kugawana vyombo vyao.

Alisema Julai 15, 2013 mtuhumiwa alionekana siku ya tatu Julai 15, 2013 tangu kuvunja ndoa yao katika maeneo ya Centre-John kijijini hapo majira ya saa nne usiku na kuondoka alipofika jirani na nyumba ya marehemu alimvizia marehemu na kumkata visu sehemu za mwili na kumuua marehemua.