TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO rasmi la Ndugu Zitto Z. KABWE
(MB) kuhusiana na kinachoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema"
Ndugu Wanahabari,
NILIPOKUWA katika ziara ya bara la
Ulaya kati ya Oktoba 21 mpaka Novemba 2 mwaka huu (2013), nilipokea kwa njia ya
barua pepe ripoti inayoitwa "Taarifa ya Siri ya Chadema" ambayo pia
ilikuwa imesambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.
“Taarifa ya Chadema inasema
kwamba chama hicho (chama changu) kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu
tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi napokea fedha kutoka Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema.
Ripoti hiyo ilinihusisha pia na
mwananchi raia wa Ujerumani, Andrea Cordes ambaye, kwa mujibu wa ripoti hiyo,
alinisaidia kupokea na kuhifadhi kiasi cha dola 250,000 za Marekani kupitia
kwenye akaunti yake binafsi.
Taarifa hii ya kutunga na iliyojaa
uongo wa kiwango cha kutisha, imenifadhaisha, kunisikitisha na kunikasirisha.
Taarifa hii iliibuliwa katika
kipindi ambacho nilikuwa safarini kutetea haki za Watanzania na Waafrika ambao
utajiri wao wa rasilimali unafaidiwa na watu wachache waliohifadhi mali katika
nje za nje na pia kupigania makampuni ya mataifa tajiri yalipe kodi stahiki
katika nchi zetu.
Pengine lengo la ripoti hiyo
lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya
kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo
waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu.
Nafahamu kwamba mimi ni mwanasiasa
ambaye nimekuwa mlengwa (target) wa mashambulizi kutoka kwa makundi mbalimbali
ya wanasiasa na vikundi vyao. Kama mwanasiasa, niko tayari kupokea changamoto
zozote zinazokuja na uanasiasa wangu.
Hata hivyo, ambacho sitakubali ni
kwa watu kutumia jina langu na uanasiasa wangu kunichafua mimi binafsi na watu
wengine wasiohusika kwa sababu ya kutaka kutimiza malengo yao ya kidhalimu.
Raia huyo wa Kijerumani tayari
amekana kuhifadhi fedha zangu. Kwa maelezo yake kwa baadhi ya viongozi wa
Chadema amekana kuwa na akaunti inayotajwa na amekana pia kuwepo nchini
Ujerumani katika siku na wakati uliotajwa kwenye ripoti hiyo.
Ripoti hiyo imemtaja pia mtu kama
Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB ikidai kwamba
nilikutana naye na alishiriki kwenye igizo hilo la kunipa fedha.
Niseme mapema kwamba tangu kuzaliwa
kwangu sijawahi hata mara moja kukutana na Dk. Kimei popote pale ndani
au nje ya nchi. Kumuingiza mtu ambaye amejenga jina lake kwenye taaluma ya
kibenki kwa sababu tu ya lengo ovu la kumchafua Zitto Zuberi Kabwe si uungwana
bali ni unyama.
Kutokana na uchafuzi huu wa wazi
dhidi ya taswira yangu binafsi na watu wengine walioingizwa kwenye mkumbo huu,
nimeandika rasmi kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa kumwomba
athibitishe kwamba kinachoitwa Taarifa ya Siri ya Chadema ni kweli ni taarifa
ya chama au kiikanushe ili niweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi
wa hekaya hiyo.
Cha ajabu, nimepokea ujumbe wa
kutishiwa maisha kutoka kwa mtu anayejiita Theo Mutahaba na kuahidiwa KUPOTEZWA
endapo nitaendelea na jitihada zangu za kupambana na ufisadi na kutafuta
haki kwa Watanzania wote pasipo kujali tofauti zao za kiitikadi, kikanda,
kikabila na kidini.
Natarajia kuchukua hatua kali za
kisheria dhidi ya wote ambao wamehusika na utungaji na uenezi wa taarifa hii.
Nitahakikisha kwamba wahusika wanatafutwa na kufunguliwa mashitaka stahiki ya
upotoshaji na kuchafuana.
Ni matarajio yangu kwamba wale wenye
mapenzi mema na Tanzania, mimi binafsi na utawala wa sheria, wataelewa nia
yangu ya kutafuta haki katika suala hili.
Nimeamua kujitolea maisha yangu kwa
ajili ya Watanzania na kama alivyopata kusema Rais Mstaafu wa Afrika Kusini,
Nelson Mandela; “Struggle Is My Life.”
Forward Ever, Backward Never- Kwame
Nkrumah
Zitto Kabwe (Mb)
10/11/2013