Monday, November 11, 2013

FAIDA HASI KATIKA MAENDELEO KATAVI

Uwanja wa Fisi Mpanda kama Dar kizaazaa kitupu

 

YALIKUWA majira ya saa mbili jioni,Ijumaa wakati nilipopita katika mtaa wa  Majengo maarufu kama Kingspalace. Nilikuwa nimechoka lakini pia nilikuwa na hamu ya kujua usiku Mpanda ikoje na eneo ambalo niliambiwa linaweza kunipa  taswira ya mpanda usiku ni eneo la Majengo.
Mtu aliyenielekeza hakuwa na muda wa kunipa hadhari, aliniona ni mtu wa makamo na ipo haja ya kukutanishwa na watu wa aina yangu katika maeneo ambayo  ni wenye hulka fulani tu wanakuwa na uwezo wa kufika na kuvinjari.
Nilinyoosha miguu yangu kutoka Kenyatta, taratibu kama vile nina muda wote duniani, nikiangalia watu na miondoko yao hapa na pale na katika safari yangu kutoka mtaa wa Kenyatta nasikia harufu ya bangi hapa na pale,lakini ahh nilifikiri huenda si bangi ni majani yanachomwa moto.
Kwa siku ya leo Mpanda imeoneka usiku wake huwa mtulivu ukiachia muziki wa hapa na pale; maduka mengi ya bidhaa za kawaida hufungwa mapema zaidi , lakini maduka yenye bidhaa zinazofanana na maisha ya usiku hubaki wazi mpaka saa nne usiku na mengine kuendelea.
Katika muda huu nanyoosha miguu wamachinga wa mtaa wa Kenyatta walikuwa bado wanaendelea na shughuli zao japo wengijne walikuwa wakifunga mafurushi lakini  maduka ya pombe yalikuwa bado wazi na ya muziki pia.
Katika mji ambao hadithi zake zinamaingiliano makubwa na watu kutoka nje ya Tanzania na yenye uchumi unaonekana kukua kwa sasa, maisha haya ya usiku  yasiyo na fujo  yanaonekana kuwa ndio bora zaidi.
Dakika zilizidi kuyoyoma na kasi ya mwendo ilizidi kupungua kwa jinsi ninavyokaribia mtaa wa Majengo ambao wakazi wa hapa wameupatia jina la Uwanja wa Fisi.
Nilitaka kukuficha ukweli, ukweli kwanini niliamua kufika Mtaa wa majengo, maarufu kama uwanja wa Fisi. Nilipata tetesi kuwa upo ukahaba wa haja katika eneo hili na washiriki wake ni kutoka mikoa ya Singida,Mbeya,Tabora na kidogo Kigoma.
Nikaambiwa tena kwamba wapo wanafunzi walioacha sekondari wakaenda katika kituo kile kikubwa kufanya ukahaba kwani unalipa. Swala kwamba unalipa ni gumu kidogo lakini ukifika eneo unaweza kujua  unalipa kwa kiasi gani.
Naam nilifika eneo lile majira ya saa tatu na nusu kutokana na kutembea kuzembe kwangu, mambo yalikuwa ndio kwanza yanaanza kuchangamka lakini nilichotaka sikukikiona kirahisi vile.
Niliamua kuketi mahala kupata supu, kwa wale tuliozoea kuandika upuuzi kama huu, unapokosa dira supu au pombe husaidia kuvuta muda kuona kuna kitu gani eneo lile.
 
Katika supu maneno yalikuwa zaidi kuhusu madili makubwa, mambo ya machimbo.Watu wanazungumzia madini wanazungumzia utafutaji wa fedha wanazungumzia masoko na mawakala wanaowadhulumu.Lakini katika mazungumzo haya  unaambulia kujua kwamba vijana wa eneo hili ambao ni mchanganyiko kutoka  mikoa na nchi mbalimbali wana fedha za kukutandikia usoni kwa kukosa nidhamu  wanayoitaka wao.
 
Wanachozungumza ni kuishi leo kama vile hakuna kesho, wakati unamaliza supu, wanaokunywa pombe sasa wanaanza kubadilika na hata wewe unaanza kuona kuna mabadiliko, mabinti ambao ulikuwa unawaona wana ustaarabu wanaanza kuvaa nguo zinazoshiria kuwapo kwa biashara.
 
"Hapa pana mambo" nilisema nikitega njia ya maneno ili niweze kuambulia kitu. Kijana mwenye umri kati ya miaka 25 na 30 alinitazama kicha akatabasamu."U mgeni wewe" aliniuliza na mimi nikawambia ndio.
Hapo ndipo alipoanza kutiririka kwani alisema ni eneo zuri hilo kw abiashara mbalimbali, wagumu wanaokaa migodini ndipo huja kuambulia asusa za maisha baada ya kuumia.
Pana pilikapilika sana hapa na kuwapo kwa madalali wa vyumba kuliniashiria kwamba kuna uwezekano mabinti hawa wanaofanya biashara wanamalizia mashauri hayo ya mapatano palepale, kumbe haikuwa hivyo.
Ukimuita binti pale, anataka muende naye ulikopanga, lakini si kutafuta pale ambapo pana madalali wa vyumba vya kupanga na madini,na bei yao waliwazaji hao kwa kukuangalia usoni ni nzuri lakini kimsingi  shilingi 5000 inatosha kwa uliwazaji wa fasta.
 
Uwanja wa Fisi ni uwanja wa Fisi kweli kama tabia za fisi zinavyojulikana kuna kila kitu kinachotakiwa kama  ilivyokuwa katika uwanja wa Fisi wa dar es salaam, tatizo ni moja tu hakuna magodoro ya fasta eneo hilo, hakuna uwazi katika mipira japo baadhi ya gesti zina mipira.
 
Nilipata nafasi ya kuongea na Agness (si jina lake la kweli) ambaye ni mwenyeji wa Mbeya. Aliniambia kwamba amefika hapo kutafuta fedha kwa kuwa mji umeshaanza kuwa na watu ambaow anahitaji pia burudani.
 
Alisema kuwepo kwa wageni wengi hasa wanaofanya mambo mbalimbali kuanzia usakaji wa madini,biashara za madini na vyakula wakiwa vijana wanafanya watu kama wao kuwa na sehemu ya kujipatia fedha.
 
Wanalipa vizuri watu hawa ambao alisema wengi wao ni vijana wa Kisukuma na hivyo na wao wanakuwa na uwezo wa kujisaidia na kusaidia wengine katika familia zao.
 
Agness katika miaka yake ya 20 anapendeza kwa umbile lake lilijoaa sihiri pamoja na kwamba bei yake yeye ni nafuu ya shilingi 5000 tu bado hakuwa  na uwezo wa kutengeneza fedha nyingi kama wenzake wengine, lakini amesema hakuna siku anayolala na njaa, wateja wapo.
 
Kwa watafuta huduma ya kuliwazwa,wanatumia fedha kwa kuwa kesho itatapatikana fedha nyingine, machimbo yalikuwa poa sana, yalikuwa yanatema na biashara ya mahindi ni nzuri pia, fedha zipo Mpanda na mzunguko katika  shughuli za aina hii upo kwa sana.
 
Ofisa maendeleo wa Mpanda , Grace nilipomuuliza kuhusu vijana kesho yake na matatizo wanayokabiliana nayo, alizungumzia mahitaji ya fedha kiurahisi kunachochea mambo mengi ambayo si mazuri ukiwemo ukahaba.
 
Anasema kwamba upo ubishi wa wazi na kutojituma miongoni mwa vijana, ingawa anajua biashara ya ukahaba inayofanyika Mpanda washiriki wengi si wakazi wa Mpanda bali wageni waliokuja kutafuta fedha. Wapo wanaotafuta madini, wapo wanachimba madini na wapo waliokuja kufuata fedha za watafuta na wachimbaji madini.
 
Mpaka sasa hakuna mvutano wa wazi kati ya Polisi na makahaba hawa ambao kuanzia saa 12 jioni hutega mingo zao uwanja wa Fisi wakitarajia biashara hadi usiku wa manane.
 
“Unaweza kuja hata saa nane hapa na kukuta loose “ alisema Jovin (si jina lake) ambaye kazi yake ni dalali wa madini ya shaba.
 
Kwa wanafunzi wanaofanya ukahaba, labda ipo haja kwa taasisi za kiraia kutofumbia macho matatizo yanayoamnza kuchipuka Mpanda kwani jinsi spidi ya madini inavyozidi kuongezeka ni dhahiri biashara ya ukahaba itashamiri na maambukizi ya magonjwa mbalimbali ya ngono yataanza kushika kasi na serikali mwishoni italazimika kutibia watu wake kwa fedha nyingi kutokana na ukweli kuwa mchezo wao ni mauti yetu.
ILITOKA AWALI HABARILEO NA www.lukwangule.blogspot.com