Monday, November 4, 2013

TUMIENI MATAWI YA OUT KUJIENDELEZA KITAALUMA - KABAGE


MPANDA
WANANCHI wametakiwa kutumia fursa ya kuwepo kwa matawi ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika mikoa yote Tanzania ili kuweza kuinua taaluma zao na kuongeza idadi ya wataalamu katika jamii

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Taaluma katika Chuo Kikuu Huria tawi la mkoa wa Katavi, Joseph Kabage alipokuwa akisoma taarifa ya Chu hicho kwa mgeni rasmi wakati wa hafla fupi ya kufungua mwaka wa masomo kwa msimu wa masomo wa 2013/14 iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo hicho mjini Mpanda

Alisema serikali katika kuhakikisha wananchi walio na uwezo wa kitaaluma kusoma kozi mbali mbali zinazotolewa na vyuo vikuu lakini hawana uwezo wa kufika mahali vyuo viliko wanapata fursa hiyo kupitia program za masomo ya Chuo kikuu huria ambapo hivi sasa serikali imeweza kufungua tawi la Chuo Kikuu huria kila mkoa ikiwa ni pamoja na mikoa yote iliyoanzishwa hivi karibuni.

Akizungumzia mafanikio ya Chuo hicho tangu kufunguliwa katika mkoa wa Katavi, Kabage alisema idadi ya wadahiriwa na wahitimu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo amesema chuo kimekuwa kikipambana na changamoto ya kuwa na wanachuo wanaotoka maeneo ya vijijini kwenye uhaba wa nishati ya umeme na hivyo kuwawia vigumu wanachuo hao kusoma kwa ufanisi kwani masomo yote yanatolewa kwa njia ya kompyuta

Katika hotuba yake Mgeni rasmi wa shughuli hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mpanda hotuba iliyosomwa na Afisa Elimu wa Halmashauri hiyo, Venance Kayombo amewataka wanachuo kusoma kwa bidii na kuhakikisha wanapata ujuzi utakaowasaidia katika kuongeza ufanisi wa majukumu yao katika jamii kwani kipimo cha msomi ni uwezo wake wa kutekeleza majukumu aliyopewa katika jamii

Alisema ujuzi ni ujuzi haujalishi umepatikana wapi bali unapimwa kwa uwezo wa aliyepata ujuzi huo kuutumia katika kutatua matatizo yanayojitokeza katika eneo lake la uwajibikaji na kupata ufumbuzi.

Jumla ya waombaji 83 wamedaihiriwa kuanza masomo katika chuo kikuu huria tawi la Katavi katika fani mbali mbali katika kipindi cha mwaka 2013/14 ambapo bado udahiri unaendelea hivyo idadi ya waliodahiriwa itaongezeka 

KALAMBO 
MICHEZO - UHURU KAPU YAANZA KALAMBO
Na Nswima Ernest, Kalambo
KATIBU wa chama cha mpira wa miguu katika halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa (KLFA) Bonivenute Feruzi ametangaza kuanza kwa ligi ya kuwania zawadi ya vikombe jezi na fedha taslimu itakayozishirikisha timu 17 toka kata zote za halmashauri hiyo kwenye ligi itakayofikia kilele chake siku ya maadhimisho ya sherehe za uhuru wa Tanzania Bara Dec 12 mwaka huu

TAARIFA iliyosomwa na katibu huyo wa KLFA wakati wa uzinduzi wa kuanza kwa ligi hiyo uliyofanywa na mkuu wa wilaya hiyo Moshi Chang’a mjini Matai makao makuu ya wilaya hiyo ilieleza kuwa michuano hiyo inayodhaminiwa na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Rukwa Rosweeter Mushi Kasikila itafanyika kila mwaka na kulenga kukuza vipaji vya mchezo huo kwa vijana wa kiume na pia wa kike kutoka ngazi za vijiji

ALISEMA ligi hiyo iliyoanza mwezi June mwaka huu katika ngazi za kata ambapo vijiji husika vya kila kata vilichuana na kupata wachezaji bora waliounda timu moja ya kata itahitimishwa kwa mshindi wa kwanza kupata kikombe kikubwa jezi na fedha taslimu shs laki tatu mshindi wa pili kikombe na shs laki 2 na wa tatu kikombe na laki 1ambapo pia itaundwa timu moja ya kombaini ya wilaya itakayokuwa chini ya uangalizi wa KLFA katika masuala ya ufundi utaalamu na maslahi ya wachezaji

MGENI rasmi mgeni mkuu wa wilaya Moshi Chang’a aliyezindua ligi hiyo kwa kutengewa mpira wa penati na kufunga goli alisema serikali wilayani humo itaendeleza  utaratibu wa kuyatumia mashindano ya aina hiyo kwa ajili ya kuchagua wachezaji wazuri watakaoshiriki mafunzo ya mchezo huo chini ya kocha mwenye ujuzi na kujenga hamasa kwa wadau wa soka wilayani humo  kuchangia michango yao ya hali na mali

BAADHI ya wapenzi wa mpira wa miguu wilayani Kalambo waliohudhuria mechi ya uzinduzi wa ligi hiyo walimweleza mwandishi wa habari hizi kuridhika kwao na juhudi za serikali na viongozi wengine kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo kukuza vipaji vya mpira wa miguu katika wilaya hiyo mpya iliyozinduliwa takribani mwaka mmoja uliopita