WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
kila Halmashauri hapa nchini inapaswa kuweka kwenye mpango wake wa maendeleo kifungu
cha ujenzi wa maktaba ya wilaya ili watu waweze kusoma na kujiendeleza kwa
urahisi.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Novemba 16, 2013) wakati
akiwahutubia washiriki wa mahafali ya 19 ya Chuo cha Ukutubi
na Uhifadhi wa Nyaraka cha Bagamoyo yaliyofanyika
kwenye viwanja vya chuo hicho nje kidogo ya mji wa Bagamoyo.
Jumla ya wahitimu 749 walitunukiwa
vyeti kati yao 244 vikiwa ni vya stashahada na 505 ni vya astahada katika fani
za ukutubi na utunzaji nyaraka.
Alisema ukutubi ni mojawapo ya fani kongwe hapa duniani japo haiongelewi sana
hapa nchini. “Hili ni eneo linalomgusa kila mmoja wetu, kuanzia mtu wa kawaida
awe mkulima, mvuvi, seremala, mjasiriamali ama yeyote ambaye anahitaji taarifa
mbalimbali zimsaidie katika maendeleo yake. Hali kadhalika, mwanafunzi, msomi
na mwanataaluma yeyote hawezi kufikia upeo wa masomi na taaluma yake kama hakusoma
vitabu na machapisho yaliyoko katika maktaba ambavyo vinatunzwa mkutubi.
Alisema kati ya wilaya 133 zilizopo
hapa nchini, ni wilaya 19 tu ambazo zimejenga maktaba katika ngazi ya wilaya. “Hii
ni sawa na asilimia 14.2 tu ya wilaya zote. Upungufu huu unasababishwa na tatizo
la watu kutotambua umuhimu wa kuwa na maktaba na katika hili lawama ni lazima
wabebeshwe Wakurugenzi wa Halmashauri,” alisema.
Waziri Mkuu alisema katika ngazi ya
mikoa hali si mbaya kwani mikoa 22 kati ya 25 ya Tanzania Bara ina maktaba za
mkoa.
“Tunazo Halmashauri 167 lakini ni Halmashauri
19 tu ambazo zina maktaba... nitoe wito kwa wilaya
zote ambazo hazina maktaba zione umuhimu wa kuwa na maktaba zake. Tukifanikiwa kuwa
na maktaba katika kila mkoa na kila wilaya itatuwia rahisi kuisogeza huduma
hiyo katika ngazi ya kata ili iwe karibu zaidi na wananchi,” alisema.
Akisisitiza
umuhimu wa fani hiyo Waziri Mkuu alisema mahitaji ya wakutubi hapa nchini ni
makubwa kwani hapa nchini kuna shule za msingi zaidi ya 16,300 na shule za
sekondari zaidi ya 4,500 za Serikali na za binafsi.
“Tunawahitaji
zaidi hawa wakutubi katika shule zetu kwani wakiwepo kwenye shule zetu watakuwa
karibu na wanafunzi na wataweza kuwasaidia wanafunzi kupanua uelewa wao,”
alisisitiza.
Aliahidi
kufuatilia maombi ya bajeti ya maendeleo ya chuo ili kukisaidia chuo hicho kiwe
bora zaidi.
Mapema akitoa taarifa
ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Zuberi Khatibu alisema chuo hicho
kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa licha ya kuwa udahili umekuwa
ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
“Mwaka 2007/2008
chuo kilidahili wanafunzi 100 lakini katika mwaka 2012/2013 tulidahili
wanafunzi 708 na mwaka huu wa masomo (2013/2014) tumedahili wanafunzi 821,”
alisema.
Naye Mwenyekiti
wa Baraza la Chuo hicho, Dk. Alli Mcharazo, alisema kabla chuo hicho
hakijaanzishwa hapa nchini, wanafunzi waliokuwa wakitaka kusomea masomo ya
ukutubi na uhifadhi nyaraka walilazimika kwenda Makerere, Uganda.
Alisema mbali ya
uwepo wa chuo hicho, changamoto kubwa inayowakabili ni ufinyu wa bajeti, uhaba
wa miundombinu hasa upungufu wa mabweni na madarasa kiasi kwamba wanalazimika
kuwa na shift mbili za masomo (asubuhi na jioni) hali ambayo inaathiri utoaji
wa elimu chuoni hapo.
Katika risala yao, wanafunzi wanaohitimu waliomba wapatiwe
ajira za moja kwa moja kama ilivyo kwa walimu au askari, pia waliomba maktaba
ya chuo hicho ipanuliwe kwa sababu ni ndogo na ikiwezekana chuo kiongezewe
kompyuta kwa sababu zilizopo hazitoshi wanafunzi wote kufanya mazoezi kwa
vitendo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAPILI, NOVEMBA 17, 2013MAJENGO YA SHULE YANAUZWA KAHAMA MJINI
TITTLE No. 37755 Registered Mwanza
LAND plot No. 122
BLOCK 'P' low Density
Mbulu Kahama Urban Area
GURANTEE ; 33 yrs
MMILIKI; BERTHA MABULA KINUNGU
SIMU: +255756 01 83 36
KAMA UNAHITAJI WASILIANA NA MMILIKI WA SHULE: Bertha Mabula Kinungu wa S. L. P 34 Kahama; simu No. +255756 01 83 36
Email: willysumia@gmail.com
BEI NI NAFUU SANA
No comments:
Post a Comment