Katavi
KAMPUNI ya uwindaji ya Tanzania
Big Game Safaries Ltd imekabidhi
baiskeli ya walemavu kwa walemavu 150 walioko katika mkoa wa Katavi zenye
thamani ya shilingi million 52.5 ikiwa ni mchango wao katika jamii kutokana na
faida wanayopata katika shughuli za uwindaji na utalii mkoani Katavi
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda,
mwakilishi wa kampuni hiyo, Rose Bekker alisema Kampuni ya Big Game imekuwa
ikitoa msaada kwa wana jamii mbali katika maeneo wanayofanyia kazi za uwindaji
kila mwaka tangu 2005 ambapo mpaka sasa kampuni hiyo imeshakabidhi baiskeli za
walemavu za kisasa zipatazo elfu tatu katika maeneo mbali mbali hapa nchini
Alisema kampuni yake pia
imekuwa ikiwekeza katika ujenzi wa madarasa, ujenzi wa makanisa, vifaa vya
shule na misaada kwa walemavu kwa kushirikiana na asasi isiyo ya kiserikali ya
Conservation Foundation Trust Fund (CFT) ya jijini Arusha
Alisema taasisinyake
inawasiliana na asasi ya Kimarekani ya Wheel Chair Foundation katika
matengenezo ya baiskeli kwa ajili ya walemavu kwa gharama ya shilingi laki tatu
na nusu (350,000/=)
Katika hotuba yake mgeni
rasmi wa hafla hiyo fupi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mpanda, Enock
Gwambasa alisema kuwa hivi sasa kumekuwa na tabia mbaya ya unyanyapaa kwa
walemavu katika jamii hali inayosababisha baadhi ya walemavu kuishi kwa sononi
kubwa
Aliwataka walemavu kujiona
kuwa nao ni sehemu ya jamii na hivyo wana uwezo wa kuzalisha mali ndani ya
jamii ikiwa watajengewa uwezo wa kufanya kazi hizo, wasibweteke washiriki
kikamilifu katika shughuli za kijamii kama vile kupiga vita ujangiri kwa kutoa taarifa
serikalini za uwepo wa majangiri katika maeneo yao
Jumla ya walemavu 150
walikabidhiwa baiskeli zenye thamani ya shilingi laki tatu na nusu sawa gharama yote kufikia shilingi
milioni 52.5 zote zikiwa zimetolewa na Tanzania Big Game Safaries kama mrejesho
wa faida kwa jamii inayozunguka maeneo wanayofanyia kazi zake.
Mmoja wa waliopata msaada
huo ambaye amemaliza kidato cha nne mwaka huu katika shule ya Sekondari ya
Mwangaza, Kashindie Kisamvu licha ya kushukuru kwa msaada huo aliiomba serikali
kuangali suala la miundombinu katika maeneo ya maofisini na madarasani kwani hakuna
sehemu ya mlemavu kuingia
Alisema vyoo vya shule
havimfai kabisa mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo alipokuwa akisoma shuleni
Mwangaza alipobanwa na haja alikuwa akilazimika kuomba ruhusa kwenda nyumbani
kwao kwa lengo la kujisaidia na kurudi tena shuleni hali iliyokuwa ikimsababishia
kupoteza muda mwingi na vipindi vya masomo
“Nilikuwa Napata shida sana
shuleni kwani madarasani hakuna sehemu ya kuingia kwa baiskeli, ofisini hakuna
na vyooni nako hakuna pia sehemu ya kupita mlemavu, nilikuwa nikibanwa na haja
nalazimika kuomba ruhusa kwenda nyumbani kujisaidia ndipo nirudi tena shuleni,
nikuwa nachelewa vipindi vingi sana na nilikuwa naathirika sana kitaaluma”
alisema Kashindie