Wednesday, November 21, 2012

ADHABU MBADALA ZAWEZA KUBADILI SURA YA MAGEREZA

ADHABU MBADALA KATIKA KESI ZA JINAI NA FAIDA ZAKE KATIKA JAMII


UTANGULIZI
Tangu awali kumekuwepo na aina mbalimbali za adhabu ambazo zimekuwa zikitolewa kwa watu waliokuwa wakiikosea jamii. Baadhi ya adhabu zilizokuwa zikitolewa ni kama kukatwa kichwa, kuchomwa moto hadi kufa, kukatwa mokono, kutelekezwa kwenye visiwa vya mbali na kuachwa huko n.k. 
Ili kuondokana na adhabu hizi za kinyama na kikatili, adhabu ya kifungo gerezani ilibuniwa. Kuanzishwa kwa adhabu ya kifungo kulienda sambamba na uanzishwaji wa magereza kwa ajili ya kuwahifadhi wahalifu waliokuwa wanahukumiwa adhabu za kifungo.
Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi yaliyokuwa yanaendelea katika Jamii, uhalifu nao uliendelea kukua kwa kasi na magereza yaliyokuwapo yakashindwa kuhimili wimbi hilo. Msongamano ulianza kujitokeza magerezani na kufanya Huduma magerezani kuanza kuzorota, hivyo Jamii ikaona kuwa kuna umuhimu wa kuanza kutafuta adhabu Mbadala ya kifungo hasa kwa wahalifu wa makosa madogo madogo, na kifungo gerezani kikabaki kwa wahalifu sugu ambao wanaonekana kuhatarisha usalama wa Jamii. 
Kutambua umuhimu wa kuwepo kwa adhabu mbadala, Umoja wa Mataifa katika Azimio lake Namba 45/110 la tarehe 19 Desemba 1990 ulitoa toleo maalum lililohimiza nchi wanachama kuanzisha utaratibu wa kuwa na adhabu Mbadala wa kifungo na kuona umuhimu wa kuhusisha Jamii zaidi katika utekelezaji wa adhabu za makosa ya Jinai.Katika jitihada za utekelezaji zilizofuatia azimio hilo duniani kote, ikaridhia kwamba adhabu mbadala wa kifungo zina gharama nafuu zaidi, ni za kiutu zaidi na zinafanikiwa zaidi katika urekebishaji wa wahailifu.
Hata hivyo, katika kusisitiza umuhimu wa kuwa na adhabu mbadala itakayoweza kuwafanya wahalifu watumikie adhabu zao katika Jamii badala ya kwenda magerezani,aliyekuwa Rais wa Jamuhuri Muungano wa Tanzania wa awamu ya tatu Mhe. Benjamini W. Mkapa katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kufungua mkutano wa wakuu wa Magereza nchini uliofanyika Capricon Hotel, Marangu Moshi tarehe 19 Aprili, 2001 alikuwa na haya ya kusema. (ninamnukuu)
“Ninafurahi kuwa hapa nchini kama ilivyo duniani kote,maswali yanaulizwa iwapo adhabu ni Jela tu. Na takwimu zinaonyesha kuwa si wahalifu wote wanaogopa jela. Maana, kati ya asilimia 12 – 15 ya wafungwa wote wanarudia uhalifu, na kujikuta wanarejea jela kila mwaka. Takwimu pia zinaonyesha kuwa wengi wao ni wale wenye vifungo vifupi chini ya miaka 5. Hawa ni wale wenye makosa madogo madogo ambao wangeweza kutafutiwa adhabu nyingine badala ya kulundikwa gerezani ambako inaelekea wanapazoea,na pengine kujifunza uhalifu zaidi badala ya kujirekebisha……”
Lazama sasa tubuni utaratibu wa kuadhibu wahalifu kwa njia itakayosaidia zaidi kuwarekebisha, si kuzidi kuwatumbukiza kwenye uhalifu, na bila kuibebesha serikali gharama kubwa mno. Ningependa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, na kwa kuzingatia uzoefu wa nchi nyingine, walete haraka Serikalini mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria yatakayowezesha wahalifu ambao hawana hatari yoyote kwa Jamii watumikie vifungo vyao nje, na watumikie Jamii kama sehemu ya adhabu zao…..”
Napenda nitumie fursa hii kutoa wito kwa Wananchi kwa ujumla kuyakubali mabadiliko tunayokusudia kuyafanya kwani tunayafanya kwa nia njema kabisa ya kuboresha mfumo wetu wa sheria na haki. Serikali itahakikisha kuwa tahadhari zote zinachukuliwa ili kuzingatia kwa ukamilifu lengo kuu la kilinda na kuimarisha usalama wa Jamii…”
MAANA YA ADHABU MBADALA
Adhabu mbadala kimsingi ni adhabu yoyote mbali ya kufungwa gerezani inayotolewa na Mahakama kwa mhalifu aliyetenda kosa la jinai.Hata hivyo kwa kuzingatia mazoea ya muda mrefu adhabu ambayo imezoeleka zaidi ni kuwafunga gerezani  wahalifu waliotiwa hatiani.
Aina ya vifungo/ adhabu mbadala ni pamoja na:
i.                    Kuachiwa kwa masharti
ii.                  Faini
iii.                Extra Mural Labour(GN No.77/1968) Sheria ya magereza inayohusu wafungwa wa  vifungo vya nje ambao hufanya kazi si chini ya masaa 6 chini ya wakurugenzi.
iv.                Watakao achiwa kwa Parole(The parole Boards Act, No.25/1994)
v.                  Huduma kwa Jamii (Community Service Order)        Adhabu hizi mbili zinasimamiwa na  Maafisa Huduma kwa Jamii na maelezo ya namna ya utekelezaji wake kwa kifupi ni kama ifuatavyo hapa chini;                
vi.                Majaribio na ujenzi wa Tabia(Probation Order)     
COMMUNITY SERVICE ORDER
Kwa kifupi Adhabu ya Huduma Kwa Jamii (Community Service) ni aina ya hukumu itolewayo na Mahakama kwa mtu aliyepatikana na hatia kwa kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo kisichozidi miaka mitatu (3), ambapo mtuhumiwa hupewa adhabu ya kufanya kazi ya kutoa huduma kwa jamii bila malipo kwa faida ya jamii badala ya kutumikia kifungo gerezani.
Katika utekelezaji wa adhabu hii mamlaka mbalimbali zimepewa nafasi tofauti kuiwezesha adhabu hii kutekelezeka;
a)      NAFASI YA MAHAKAMA
Utaratibu wa wafungwa kufanya kazi za kuihudumia jamii kama adhabu mbadala unatokana na amri ya Mahakama.
Mahakama chini ya  kifungu cha 3(1) (a) (b) cha  Sheria ya Huduma kwa Jamii Na. 6/2002 imepewa uwezo kisheria wa kutoa amri hiyo kwa wafungwa waliotiwa hatiani kwa makosa ambayo kifungo chake kwa mujibu wa sheria hakizidi miaka mitatu bila kujali iwapo ina faini au la, au wale ambao adhabu iliyowekwa kwa mujibu wa sheria ni zaidi ya miaka mitatu lakini Hakimu, kutokana na uwezo aliopewa kisheria, akaamua kutoa adhabu ya kifungo kisichozidi miaka mitatu.
Amri hiyo vile vile inaweza kutolewa baada ya Hakimu kupata ushauri kutoka kwa Mkuu wa Gereza pale ambapo Mfungwa anayehusika tayari yuko gerezani. (Kifungu cha 52(2) cha Sheria ya magereza Na.34/1967 kama ilivyorekebishwa kwa Sheria Na. 9/2002)
b)     NAFASI YA MAGEREZA
Kifungu cha 52(1) cha sheria Na.34/1967 kinamtaka mkuu wa gereza baada ya kujiridhisha kuwa mfungwa aliyeko gerezani kwake ametimiza sifa na vigezo vya kumfanya atumikie adhabu yake chini ya utaratibu wa Huduma kwa jamii, kufanya yafuatayo;
(i)                 Amshauri mfungwa juu ya uwezekano wa kutumikia adhabu yake chini ya sheria ya Huduma kwa jamii.
(ii)               Kupeleka mapendekezo ya kuridhia kwa mfungwa katika mahakama yenye mamlaka mahali alipo mfungwa tayari kwa kuanza mchakato wa kumfanya atumikie adhabu yake chini ya sheria ya Huduma kwa jamii.
I)                   PROBATION ORDER
Amri hii hutolewa na mahakama kwa kuzingatia kifungu Na.3 (1&2) na 4 cha sheria sura 247(The probation of offender’s Act, Cap. 247) Ni matakwa ya sheria hii pia kwamba amri hiyo itolewe baada ya kujiridhisha kwa taarifa ya uchunguzi wa kijamii(social enquiry report) ambayo itakuwa imewasilishwa mahakamani na ‘Probation Officer’au Afisa Huduma kwa jamii.
FAIDA ZA ADHABU MBADALA KATIKA JAMII
1.   -   Kukabiliana na suala la msongamano wa wafungwa gerezani.
Kupunguza gharama za kuendesha Magereza kwa kupunguza watu wanaotegemea huduma ya magereza ikiwa na maana kwamba wafungwa gerezani wanahitaji chakula,mavazi, matibabu n.k kama binadamu wengine wote na hilo ni jukumu la serikali ambayo sisi sote tunaitumikia.
3.      Kupunguza utegemezi wa kifungo gerezani kama ilivyo sasa.

4.      Kuishirikisha Jamii katika kuwarekebisha wahalifu
5.      Kuiwezesha jamii kunufaika moja kwa moja na kazi watakazofanya wahalifu
6.      Kuwawezesha wahalifu kuendelea kutunza familia zao na hata kujizalishia mali na kujiongezea vipato vyao  huku wakiendelea kutumikia vifungo vyao.

7.      Kuwaepusha Wahalifu ambao sio wazoefu na madhila yatokanayo na maisha ya Gerezani kama vile kujifunza tabia mbaya kutoka kwa wahalifu sugu(core criminals), kuambukizana magonjwa n.k
8.       Kuwaondolea Wahalifu unyanyapaa (prison Stigma)
MAKALA HII IMETOKA KATIKA MTANDAO MWENZA WA BLOG HII UNAOMILIKIWA NA FRANCIS GODWIN - Sumia