Sunday, November 25, 2012

HIFADHI YA TAIFA YA KATAVI

  HIFADHI YA TAIFA YA KATAVI- introduction


KATAVI National Park kama inavyofahamika zaidi, ni miongoni mwa hifashi za wanyama pori kubwa kabisa zilizopo nchini, na kwa kweli ni fahari ya mkoa wa Katavi, ulioanzishwa majuzi na kulitumia jina la mbuga hiyo.
 
Ni bahati mbaya kwamba Katavi haijatangazwa na kujulikana sawasawa na ndio maana hutembelewa na watalii wachache sana ikionekana ni kama vile imetengwa na ‘mabosi’ wa TANAPA.
Lakini ni kweli kwamba uoto wa asili na hata wanyama wanaopatikana kwenye mbuga hiyo humpa mtalii au mtu yeyote anayetembelea ile ladha halisi ya Afrika, ile iliyokuwapo miaka mia moja iliyopita.
Kwa ukubwa wa eneo, Katavi ni ya tatu Tanzania na inapatikana kusini magharibi mwa nchi yetu katika mmoja kati ya ‘mikono’ ya bonde la ufa, ikijitenga na Ziwa Rukwa.
Ndani ya mbuga hiyo kuna kila aina ya wanyama wenye afya nzuri na maumbo makubwa na si ajabu ukakutana na makundi makubwa ya tembo, nyati, swala, pundamilia na wanyema wengine kadhaa. Sehemu nzuri na ya kuvutia zaidi kwa mwonekano ni Mto Katuma na eneo lake ambao hufurika sana wakati wa mvua pamoja na maziwa ya msimu ya Katavi na Chada ambayo hujazwa na makundi ya wanyama na ndege huku yakiwa ni nyumbani kwa viboko wakubwa na mamba.
Kipindi cha kiangazi huyaacha maeneo mengi makavu na Katavi kubaki pweke huku Mto Katuma ukibaki na vibwawa vya maji kwa ajili ya wanyama kunywa.
Inakisiwa kuwa tembo 4,000 na maelefu ya nyati hutawanyika kusaka maji na malisho wakati wa kiangazi ndaniu ya Katavi huku idadi kubwa ya twiga, punda milia, swala, ngiri na hupatikana kwa urahisikama chakula cha simba na fisi.
Wengi hufurahia kuwaona viboko wanaoishi pamoja na mamba huku mapigano ya mara kwa mara kati ya viboko dume yakitokea kwenye mabwawa yenye kina cha kutosha.
Hifadhi ya Taifa ya Katavi ina ukubwa wa kilomita za mraba 4,471 ikijitandaza mashariki mwa Ziwa Tanganyika huku makao yake makuu yakiwa ni Sitalike, umbali wa kilomita 40 kusini mwa makao makuu ya mkoa wa Katavi, mji wa Mpanda.
Mbuga hii inafikika kwa ndege za kukodi kutokea Dar es Salaam au Arusha huku mtalii au yeyote anayependa kufika huko kwa njia ya barabara akilazimika kusafiri kwa siku nzima umbali wa kilomita 550 kutoka Mbeya au, kwa nyakati za kiangazi tu, njia ya Kigoma yenye kilomita 390 nayo inaweza kutumika.
Viwanja vya ndege vya nyasi vipo Iku na Sitalike na ndege hutumia wastani wa saa tatu kutoka Dar es Salaam na hata Arusha. Mpanda mjini kuna uwanja wa kisasa wa ngege.
Pia njia nyingine iliyozoeleka miaka kadhaa iliyopita ilikuw ani ya treni kutoka Dar es Salaam kupitia Tabora hadi Mpanda na kisha kwenda Sitalike ambako ndiko usafiri wa kuingia mbugani hupatikana. Ni ushauri tu kwamba, anayetaka kusafiri hadi Katavi, anapaswa kutenga mudawa kutosha kuja na kurudi alikotoka.
Ni vyema pia kuwa safari hiyo ikafannywa kipindi cha kiangazi, yaani kuanzia mei hadi Oktoba kwani wakati wa mvua, si tu kwamba ni shida kufika Katavi, lakini pia barabara karibu zote ndani ya mbuga hufurika maji na kutopitika kwa urahisi. Hii ni kati ya Desemba na Februari.
Huduma ya ‘tented camps’ hupatikana kuliangalia ziwa Chada wakati kukiwa na ‘resthouse’ nzuri pale Sitalike huku Mpanda mjini kukiwa na hoteli safi na nzuri za kisasa.
Kumbukumbu zinaonyezha kuwa Katavi ilifanywa kuwa hifadhi ya taifa mwaka 1974 ikiw ana idadi kubwa sana ya wanyama ingawa kwa sasa kuna taarifa kuwa uwindaji haramu, hasa wa kusaka nyama ya kula, umepunguza sana wanyama hao.
Idadi ya wanaotembelea mbuga hiyo kwa mwaka si rahisi kupatikana kwa uwazi lakini ukiifananisha na mbuga nyingine nchini, hakika hii ina watalii wachache sana. Kwa mfano, katika msimu wa utalii wa mwkaa 2005 ilikuwa watu 250 tu na ikaja kudaiwa kuongezeka hadi watu 400 mwaka 2007 na watu  700 mwaka 2008.