Sunday, November 25, 2012

TFDA HIZI SIYO HABARI NZURI KWENU NA KWA WATANZANIA...


TFDA ibomolewe, isukwe upya, wahujumu wa madawa ya umma washitakiwe.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MSIMAMO WA JUMUIYA YA VIJANA KWA TFDA NA WAUZAJI WA MADAWA YA KULEVYA NCHINI.
·         
·         Vinara wa Madawa ya kulevya nao watajwe na kufikishwa mahakamani.
Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya, Mamlaka ya Chakula na Dawa, pamoja na Mamlaka ya Bandari vimekuwa mawakala wakubwa wa biashara haramu ya afya za watanzania. Afya za watanzania zinaendelea kuwekwa rehani na waliopewa mamlaka ya kuongoza.
Wizara ya Afya imekuwa ikiruhusu uwepo wa zahanati na maduka ya madawa yasiyo na wataalamu wa afya ambapo watanzania wengi wamekuwa wakipewa dawa zisiendana na magonjwa wanayoumwa. Hali imesababisha madhara makubwa kwa wagonjwa. Utafiti uliofanywa na Youth Initiative Tanzania (yiTa) na TWAWEZA kuanzia Novemba 2011 hadi Agosti 2012 ulibaini kuwa zaidi ya 93% ya huduma zinazotolewa katika zahanati na maduka binafsi ya dawa jijini Dar es salaam, hutolewa bila kutumia utaalamu wa afya. Je, wizara ya Afya ina mpango gani wa kukomesha hali hii?.
Pamoja na hali kuwa mbaya kiasi hicho, TFDA imekuwa ikpata kashfa kubwa za kuhatariasha maisha ya watu kila kukicha lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya mabosi wa TFDA. Watanzania watakumbuka kuwa mwishoni mwa mwaka 2011 watafiti wa ugonjwa wa Maralia toka Uingereza wakiongozwa na Dr. Washington walitoa ripoti juu namna ambavyo Serikali za Afrika zimekuwa zikipokea madawa bandia toka China na namna ambavyo madawa hayo yanavyoathiri afya za watu. Lakin cha ajabu TFDA ilikana kupokea madawa bandia, lakini baada ya miezi miwili madawa bandia ya Maralia yakakamatwa Mwanza na Kilimanjaro. Ndipo baadaye viongozi wa TFDA walipojitokeza kwa aibu na kukiri kuwapo kwa madawa hayo bandia nchini. Lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao.
Hivi karibuni, kumepatika dawa feki za kuongeza nguvu za waathirika wa VVU, lakini pia hakuna hatua zozote zilizokwisha chukuliwa.
Na cha kusikitisha zaidi, ni pale Watanzania wanaambiwa kuwa hakuna dawa katika hospitali za umma wakati hospitali za binafsi zina shehena ya dawa zilizoandikwa “NOT FOR SALE”. Na cha ajabu zaidi TFDA wanakili kuwa wameibiwa dawa zilizotakiwa zitolewe bure kwenye zahanati na hospitali za serikali lakini zimepotea na zinapatikana katika hospitali na maduka binafsi ya dawa zikiwa zimefutwa nembo ya NOT FOR SALE. Wakati haya yanatendeka, hospitali za umma ziko taabani, hakuna dawa. Imebaki kwenda hospitali na kupima, kisha unaambiwa nenda ukanunue dawa katika dawa Fulani. Lakini serikali imekaa kimya dhiti ya mamlaka hizi.
Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF), inatambua kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, kunahatri kubwa ya kuwapoteza watoto wengi ambao ndio vijana wa kesho. Akina mama na Vijana nao wako hatarini kupotea. Hivyo tunaitaka serikali kuwaachisha kazi wakurugenzi wote wa TFDA ili hatua za kisheria zichukue mkondo wake.
Nalo suala la watuhumiwa wa madawa ya kulevya limewekwa kwapuni kwa sasa. Serikali ilishahidi kutoa orodha yao lakini haitaki kutoa hadi sasa. Hili ni suala linaloathiri maisha na nguvu kazi ya vijana moja kwa moja. Vijana wengi wanapotea kwa kuathirika na madawa ya kulevya.
JUVICUF inaitaka serikali iwataje wauzaji na wasambazaji wa madawa ya kulevya nchini bila kujali vyeo na haiba yao katika jamii. Na baada ya kuwataja, wafikishwe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Endapo serikali haitachukua hatua za kuisafisha TFDA na kuwataja pamoja na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wa madawa ya kulevya kama ilivyoahidi, na kwa kuwa waathirika wakubwa madawa ya Kulevya na madhara ya kuuzwa kwa dawa kiholela pamoja hospitali za umma kukosa dawa ni Vijana, JUVICUF itafanya maandamano ya amani hadi wizara ya afya kushinikiza hatua za uwajibikaji na kisheria zichukuliwe.
Imeandaliwa na:
Thomas D.C Malima
Naibu Katibu
Jumuiya ya Vijana ya CUF (JUVICUF)-Taifa.
MATAMKO HAYO YANAJENGA AU KULINGANISHAJE NA HABARI HII KATIKA MAMLAKA NYETI KWA UHAI KAMA HII, SOMA HII YA FEBRUARY MWAKA HUU.......... 

Dawa feki za malaria zaingizwa nchini

25th February 2012
Mamalaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)
Mamalaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), imebaini kuwapo kwa dawa bandia ya kutibu ugonjwa wa Malaria katika soko iitwayo ‘Eloquine’, ikiwa katika makopo ya vidonge 1,000 kila moja.



Dawa hiyo imebainika kuwa ni bandia, kutokana na maelezo yaliyopo katika lebo kuonyesha imetengenezwa na kiwanda cha Elys Chemical Industries Ltd cha nchini Kenya, wakati kiwanda hicho hakitengenezi dawa yenye jina la biashara la ‘Eloquine’. 

Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa, hadi sasa jumla ya makopo 155 ya dawa hiyo bandia yaliyokuwa yakisubiri kusambazwa, yamekamatwa jijini Dar es Salaam.
Alisema kati ya makopo hayo, moja lenye vidonge 115 lilikamatwa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Pia mtuhumiwa mmoja amefikishwa mahakamani na upelelezi wa chanzo na wasambazaji wa dawa hiyo unaendelea kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Alisema kiwanda cha Elys Chemical Industries Ltd kimesajili dawa ya Quinine Sulphate 300mg B.P isiyo na jina la kibiashara.
Sillo alisema kiwanda hicho kimebainisha tofauti mbalimbali zilizopo katika lebo ya dawa bandia ikilinganishwa na dawa halisi.
Dawa halisi ya ‘Eloquine’ hutengenezwa na Elys Chemical Industries Ltd  na imesajiliwa na TFDA na hivyo kuthibitisha kuwa kiwanda hicho hakitengenezi dawa hiyo bandia.
Alisema uchunguzi wa dawa bandia katika maabara umebaini kuwa vidonge hivyo havina kiambato hai kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa Malaria na hivyo matumizi yake ni hatari kwa afya ya binadamu.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TFDA alisema pia maelezo ya kina yanatofautisha dawa halisi iliyosajiliwa na dawa bandia.
Alisema kwa mfano, jina la dawa halisi iliyosajiliwa linasomeka: ‘Quinine Sulphate 300mg B.P’, tofauti na lile la dawa bandia ambalo linasomeka: ‘Quinine Sulphate 300mg U.S.P’.
Tofauti nyingine ni dawa halisi iliyosajiliwa kutokuwa na jina la biashara, wakati dawa bandia ikiwa na jina la biashara la ‘ELOQUINE’.
Pia rangi ya lebo ya dawa halisi ni nyeupe na kahawia, wakati lebo ya dawa bandia ni ya rangi ya njano na nyekundu.
Tofauti nyingine inahusu muda wa matumizi, ambapo dawa halisi iliyosajiliwa ni miaka minne wakati dawa bandia ni miaka mitano.
Vilevile, namba ya toleo la dawa halisi iliyosajiliwa huanzia na namba, lakini dawa bandia huanzia na herufi.
“Kwa mfano, namba ya toleo ya dawa halisi iliyosajiliwa inaanzia ‘2167E’, namba ya toleo ya dawa bandia inaanzia ‘GE410’,” alisema.
Alisema katika kuwakanganya watu zaidi, anuani ya mtengenezaji wa dawa bandia imetumiwa ileile ya mtengenezaji wa dawa halisi iliyosajiliwa.
Anuani hiyo ni: Elys Chemical Industries Ltd, Road B, Off Enterprise Road, P.O. Box 40411, 00100 Nairobi, Kenya.
Kutokana na hilo, amewatahadharisha wafanyabiashara wote wa dawa na wananchi kutozitumia dawa hizo bandia.
Pia amewaelekeza wale wote waliouziwa dawa hizo bandia kuzirudisha katika ofisi za TFDA, vituo vya afya vya serikali au vituo vya polisi vilivyo jirani nao.
Vilevile, amewakumbusha wafanyabiashara wa dawa, wasafirishaji wa vifurushi na wananchi kwa jumla, kutoa taarifa haraka iwezekanavyo pale wanapohisi kuuziwa dawa duni, bandia au zilizoisha muda wa matumizi.
“Taarifa zitolewe ofisi za TFDA makao makuu zilizopo Barabara ya Mandela, EPI Mabibo External, Dar es Salaam na Ofisi za Kanda zilizopo mtaa wa Nkurumah, Mwanza, Mtaa wa Sakina – Arusha, Hosptali ya mkoa wa Dodoma na Jengo la Ofisi ya Mifugo Mkoa wa Mbeya,” alisema Sillo.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema aliyefikishwa mahakamani, ameshtakiwa kwa mujibu wa sheria namba 1 ya mwaka 2003 ya TFDA. Alisema mtu huyo anatuhumiwa kukutwa akiuza dawa ambayo haijasajiliwa na TFDA ambayo pia ni bandia.
Simwanza alisema sheria hiyo haizungumzii dhamana, bali inazungumzia adhabu kwa yeyote anayepatikana na hatia; ikiwamo kutozwa faini, kutumikia kifungo jela au yote mawili kwa pamoja.
“Dhamana ni haki ya mtu, sababu yawezekana mtu akakutwa anauza dawa bandia bila kujua kuwa ni dawa bandia.
Tunachokifanya sisi (TFDA) ni kupeleleza kujua amenunua wapi dawa hiyo,” alisema Simwanza.
SOURCE: NIPASHE